Thursday, July 30, 2015

TUMEJIPANGAJE KULINDA KURA, KUZUIA GOLI LA MKONO NA SIASA ZA HOVYO HOVYO?


Denis Mpagaze
Sioni ajabu yoyote wewe kuwa mwanachama wa CCM na yule kuwa mwanachama wa UKAWA kwani wote mnatekeleza demokrasi ndani ya vyama vyenye tabia za hovyo hovyo zilizosheheni majungu, kejeli, usengenjaji na vijembe badala ya kushughulikia maslahi ya Taifa. Leo akisimama mtu wa UKAWA ataichambua CCM kiasi kwamba kama unafikiri kwa kutumia kichwa siku hiyohiyo utahama chama. Lakini pia akisimama mwana CCM kuichambua UKAWA, walahi unaweza kusema ni bora niachane na siasa. Ukiwa ndani ya CCM hakika huwezi kuona lililojema ndani ya UKAWA na kadhalika ukiwa ndani ya UKAWA yote ndani ya CCM ni ubatiri mtupu. Lakini pia sioni ajabu kwa mwana UKAWA kuhamia CCM na mwana CCM kuhamia UKAWA kwa sababu lengo kuu ni kutimiza haja zao huku wanajamii wakiendelea kufedheheka kwa sababu ya umaskini.
Ni jioni moja katika matembezi ya jioni na baba yangu mdogo, mwalimu wa somo la hisabati shule ya msingi mwenye umri miaka 57. Mara nashangaa mwalimu anatimua mbio kurudi tulikotoka kwa kasi na kutokomea kusiko julikana. Sikuamini macho yangu, mwalimu wa hisabati alitoa wapi nguvu za kutimka namna ile wakati siku zote alikuwa akilalamika kiuno na miguu vinamuuma. Kumbe mwalimu alimkimbia jamaa aliyekuwa anamdai shilingi 10,000 ikiwa ni mkopo wa kilo mbili za nyama ya ng’ombe. Sina uhakika kama baba yangu mdogo mpaka anaaga dunia aliweza kulipa deni lile. Haya ndiyo matunda ya siasa za hovyohovyo ambazo zimeshamiri nchini. Mzee wa miaka 57 kuchapa mbio kuogopa deni mbele ya mtoto wake ni fedheha na aibu. Ndiyo maana nasema kuhama chama siyo dhambi, dhambi ni kama taifa kukosa mtu wa kutuokoa na aibu hii.
Katika siasa za hovyo hovyo mwenye pesa muite “power” na asiyenazo muite mbuzi wa machinjioni asiyejua saa kuchinjwa kwake.
Leo hii kupata ridhaa ya kugombea kupitia chama chochote cha siasa lazima uwe vizuri kifedha ili kupata tiketi ya kugombea ndani ya chama. Lakini pia unatakiwa ukate mshiko wa kutosha ili uweze kutangazwa mshindi kabla hata kabla ya kura hazijapigwa vinginevyo utaishia kuwasindikiza wenye pesa. Mtu wa namna hii hawezi kuisaidia jamii kwa sababu uongozi kaupata kwa jasho lake na wala siyo kura za wananchi ndiyo maana wapiga kura hawaishi kutukanwa. Wenye kiwango cha baba yangu mdogo wataendelea kufedheheshwa kwa mikopo ya nyama ya ng’ombe ndani ya nchi yenye maziwa na asali. Wakati wenye neema wanachukua mikopo ili kuwekeza, wewe unachukua mkopo ili kukata kiu ya nyama maana kwa mshara wako nyama hainunuliki vinginevyo utafukuzwa kwenye nyumba uliyopanga.
Katika siasa za hovyo hovyo usijidanganye kwamba unawatu wengi hivyo utapewa ridhaa ya kuendesha nchi. Katika historia ya nchi hii hakuna aliyevunja rekodi kwa kuwa na watu wengi kama Dr. Wilbroad Slaa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, lakini kwa sababu ya goli la mkono Dr. alibaki kuichungulia Ikulu ya Magogoni mithili ya panya aliyebanwa na mlango. Ndiyomaana kusema kwamba mgombea flani anawatu wa kutosha haitoshi, tunatakiwa kwenda mbele zaidi na kujiuliza ni kwa namna gani tutafanya kura za hao watu zifanye maamuzi? Maana nakumbuka Lenin, Dikteta mshenzi sana Duniani aliwahi kusema, “ acha watu wapige kura namna wawezavyo kwani mwisho wa siku anayeamua nani awe mshindi ni anayehesabu kura, hivyo sisi tukomae na wanaohesabu”. Goli la mkono ni ishara ya kuuenzi ushenzi wa Lenin.
Katika hili nawashauri walala hoi wenzangu kama ni kufa tuliisha kufa la msingi baada ya kupiga kura tuchukue hatua ya kulinda kura zetu. Hii kasumba ya kupiga kura then unaoondoka ni kuruhusu goli la mkono. Piga kura, rudi mita kadhaa nyuma, subiri matokeo. Nakwambia wale wanaohesabu wakiona hatuko mbali na tukio nakwambia hawatakuwa tayari kununuliwa. Huwa kuna askari wanakuwa wakatiri kwa raia lakini wema kwa wafungaji wa magoli ya mkono, nadhani hata wao watakuwa wamechoka, bila shaka watakuwa nyuma yetu kuhakikisha tunampata kiongozi tunayemtaka na hakika atakuwa muarobaini wa matatizo ya baba zangu wadogo ya kumkimbia anayewadai mchana kweupe.
Siasa za hovyohovyo zimevurugha na zinaendelea kuvuluga dini zetu nzuri. Yaani zimepenyeza rupia mpaka kujikuta watumishi wa Mungu wakimezwa bila kujijua na kujikuta wakitoa matamko tata yanayotugawa badala ya kutuweka pamoja. Mie navyojua watumishi wa Mungu ni wawakilishi wa Mungu hapa Duniani hivyo mwenye dhambi na asiye na dhambi wote ni wake kwa sharti la kutubu baada ya kufundishwa hivyo. Sasa mtumishi wa Mungu unapoinuka na kuropoka, “Asiyempenda Lowassa basi ameze malimao” hapo ni kutugawa. Lowassa yeye ni nani na hata apendwe na kila mtu? Mungu mwenyewe hapendwi na kila mtu sembuse Lowassa? Wokovu ni akili kichwani, pesa mfukoni, imani moyoni alijisemea Bishop Mpemba wa Kanisa la kwa Neema jijini Mwanza.
Ikumbukwe kwamba lengo la siasa za hovyohovyo ni kudumisha ufalme wa walioko juu na kufunga milango ya matumaini kwa walio chini. Ndiyo maana kila inapokaribia uchaguzi safari za wageni kwenda majimboni zilizosheheni kila aina ya hila zinakuwa nyingi . Utaskia, “Nimeitwa na wazee nije nigombee pamoja na kwamba sikuwa tayari hamba jinsi inabidi niwaheshimu wazee” . Sasa na wananchi tulivyowatu wa ajabu, hata hatujiulizi ni wazee gani hao wa jimbo zima walioamua kumuita mtoto mpotevu aje kututawala? Mtu kaondoka kijijini miaka 10 iliyopita hata likizo hajawahi kuja kwa sababu serikali anayoifanyia kazi haijawahi kumpa nauli atawezaje kutusaidia? Sana atakachokifanya mtu huyu ni kuchukua jimbo na kuhamia Dar es Salaam kwenda kuongeza traffic jam tu kule. Ndiyo maana George Carlin aliwahi husema kama unawananchi wabinafsi na wajinga lazima upate viongozi wabinafsi na wajinga pia.
Nimalizie kwa kusema siasa za hovyohovyo huzaa wanasiasa hovyo hovyo wenye imani ya kwamba wananchi siku zote ni watu wajinga wasio na kumbukumbu ndiyo maana Prof. Lipumba wakati anachukua fomu ya kugombea urais kupitia chama chake alisema, “kunawatu leo hii walitakiwa kuwa jela lakini eti nao wanagombea urais”. Prof. leo anayarudia matapishi yake huku akiamini watanzania tumesahau. Usicheze na siasa za hovyo hovyo, ni hatari. Katika siasa za namna hiyo kila kitu kinawezekana, shetani anaweza kuwa malaika kwa wakati mmoja. Kumbe tuweke pembeni siasa za hovyo hovyo na ili tuikomboe nchi yetu. Ukombozi wa kweli utaletwa na sisi wenyewe.
Na Denis Mpagaze

No comments:

Zilizosomwa zaidi