Siku moja
kabla ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwasilisha
bungeni, ripoti ya uchunguzi wa IPTL kuhusu ufisadi katika akaunti ya
Escrow, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe amesema amekuwa akipata
vitisho ili kuzuia ripoti hiyo.
Akizungumza jana, Zitto alisema pamoja na vitisho hivyo haogopi kwa kuwa maisha yake ameshayaweka nadhiri siku nyingi.
"Kuna
kundi la wahuni kutoka Musoma limeletwa Dodoma likiongozwa na mtu (jina
tunalihifadhi) mwenye rekodi ya ujambazi. Hivi sasa anashikiliwa na
polisi kwa kukutwa na nyaraka zilizoibwa Ofisi ya Bunge. Usalama wa
wajumbe wote wa PAC upo shakani," alisema Zitto.
Aliongeza
kuwa kuna vipeperushi vimesambazwa mjini Dodoma kumkashifu lakini
havitamsumbua kwa kuwa yeye anataka ukweli ujulikane.
Baadhi ya
wabunge jana walionekana na kitabu kilichoandikwa 'mjue Zitto Kabwe
kama mtetezi wa wanyonge,' lakini ndani yake kikiwa na mambo ya
kumchafua mbunge huyo.
Vitabu
hivyo vinaelezwa kusambazwa kwa wabunge katika nyumba zao vikilenga
kuonyesha kwamba Zitto hafai kusimamia PAC ambayo hivi sasa
inashughulikia escrow.
Wakati
Zitto akisema hayo, suala hilo la vitisho jana pia liliibuka bungeni
baada ya Mbunge wa Ole (CUF), Rajab Mbarouk Mohamed kueleza kuwa hali ni
tete kuhusu usalama wa wabunge kutokana na escrow.
Akiuliza
swali la nyongeza, Mohamed alisema usalama wa wabunge uko shakani
kuanzia maeneo wanayofanyia kazi na makazi yao na hasa kipindi hiki
tangu kuanza kwa sakata la escrow.
"Je, nini
tamko la Serikali juu ya ulinzi na usalama wa wabunge katika maeneo ya
kazi, pia katika maeneo yao ambayo wanaishi?" alihoji.
Kabla ya
majibu kutolewa na Serikali, Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye jana
alianza kuongoza vikao baada ya safari yake nje ya nchi, aliingilia kati
akisema ofisi yake inakusudia kujenga kijiji cha wabunge ambako
watalindwa kwa pamoja.
Akijibu
swali hilo, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari
Makamba alisema Serikali inafanya tathmini ya vitisho vyote vya viongozi
nchini wakiwamo wabunge ili kuhakikisha wanakuwa salama.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment