Sunday, February 9, 2014

MBUNGE AUAWA JAMUHURI YA AFRIKA YA KATI

Mbunge mmoja wa Jamuhuri ya Afrika ya Kati, ambaye alikuwa katika mstari wa mbele kupinga mauaji ya Waislamu nchini humo, ameuawa kwa kupigwa risasi katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui.
Jean-Emmanuel Ndjaroua aliuawa na watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki waliokuwa wakitumia pikipiki, siku moja tu baada ya kutoa hotuba kulaani mauaji yanayoendelea nchini humo.
Msemaji wa shirika la kutetea haki za kibinadam la Human Rights Watch, Peter Bouckaert ameonya kuwa hali nchini humo inaendelea kuwa mbaya kila uchao na raia wote wa nchi hiyo ambao ni Waislamu huenda wakalazimika kutoroka katika kipindi cha wiki chache zijazo.
Maafisa wa kutoa misaada ya kibinadam wamesema kuwa watu tisa wamefariki dunia kufuatia mapigano makali na uporaji uliotokea katika mji mkuu jamuhuri ya afrika ya kati wikendi iliyopita.
Ripoti zinasema kuwa watu wawili wanaoaminika kuwa waislamu waliuawa kinyama wakati wa machafuko hayo.
Vita vikali vilitokea siku ya Jumamosi kati ya wanamgambo wa Kikristo na Waislamu Magharibi mwa mji mkuu wa Bangui ambapo majengo kadhaa yaliharibiwa kwa kuteketezwa.
Mapigano yaendelea katika sehemu kadhaa
Mkaazi mmoja wa Bangui alisema kuwa mtu mmoja ambaye anatuhumiwa kumuua mama mmoja Mkristu aliuawa na mwili wake kuchomwa na umati nje ya ukumbu wa baraza la mji huo.
Wanamgambo wengine wa Kikristu walimuua mtu Muumini mwengine wa Kiislamu na wakati umati ulipokuwa ukijiandaa kuuteketeza mwili wake, wanajeshi wa Rwanda, ambao ni sehemu ya kikosi cha jeshi la kutunza ambani ya Muungano wa Afrika, MISA walifika mahala hapo na kumpiga risasi.
Watu wengine watano waliuawa kati hali isiyojulikana.
Peter Bouckaert wa shirika la kutetea haki za kibinaadamu alithibitisha mauaji hayo na kuongeza kuwa mtu mwingine aliuawa kinyama siku ya Jumapili karibu na soko kuu mjini Bangui.
Bwana Bouckaert alisema kuwa majeshi ya Rwanda wamemueleza kuwa hali katika CAR inawakumbusha mauaji ya halaiki iliyotokea nchini mwao miongo miwili iliyopita.
Jamuhuri ya Afrika ya Kati imekumbwa na mapigano kwa karibu mwaka moja sasa tangu kundi la waasi la Seleka lilipomteua Michel Djotodia kuwa rais wa kwanza Muislamu kufuatia mapinduzi ya kijeshi mnamo machi mwaka wa elfu mbili kumi na tatu.
Mapigano hayo yameendelea hata baada ya Djotodia kujiondoa na bunge kumuidhinisha Catherine Samba Panza kuwa kaimu rais wa nchi hiyo mwezi uliopita na waislamu wamekuwa wakitoroka mapigano hayo kwa maelfu.
Afisa huyo mwandamizi wa shirika la kutetea haki za kibinaadamu ameaema kuwa baada ya siku au majuma machache Waislamu wote wataihama Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Chanzo: BBC

No comments:

Zilizosomwa zaidi