Pages

Friday, February 21, 2014

HII NI KUTOKA GAZETI LA NIPASHE; MWENYEKITI UVCCM AMTISHIA MAKONDE MWANDISHI WA HABARI

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma KhamisiMwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamisi, ametishia kumshambulia kwa ngumi mwandishi wa habari wa NIPASHE, Salome Kitomari, kwa madai ya kuandika habari, ambazo hazikumpendeza.
Alitoa vitisho hivyo alipokutana na Salome, akiwa na waandishi wengine, wakiendelea na kazi karibu na lango la kuingia na kutoka ndani ya ukumbi wa mikutano ya Bunge linalotumiwa na wabunge, bungeni jana.
Akiwa ameshika nakala tatu za magazeti tofauti, likiwamo NIPASHE, Sadifa alifika walikokuwa wamesimama waandishi hao na kuanza kuhoji habari alizonukuliwa na NIPASHE na picha yake iliyochapishwa katika toleo la gazeti hilo la jana.
Baada ya kukumbushwa kuwa alichokisema jana, ambacho ndicho alichonukuliwa na NIPASHE, Sadifa alikana maneno yake, ambayo hakupenda yaandikwe gazetini.
Alisema katika siku zijazo hatavumilia iwapo ataona zimeandikwa habari, ambazo hazimpendezi na kwamba, kama zitaandikwa, atakachokifanya ni kumpiga mwandishi ngumi.
“Mimi huwa nakung’uta ngumi. Na kwa kweli siku nyingine nitakuchapa,” alisema Sadifa.
Alitoa vitisho hivyo, baada ya gazeti hili jana kuchapisha kauli aliyoitoa juzi akiungana na wajumbe wenzake wa Bunge Maalumu la Katiba kutaka posho za kushiriki Bunge hilo ya Sh. 300,000 anazolipwa kila mjumbe kwa siku ziongezwe.
Sadifa alinukuliwa na NIPASHE kufuatia mahojiano aliyoyafanya na Salome katika viwanja vya Bunge, muda mfupi baada ya kuzuka bungeni malalamiko kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kuhusu kulipwa posho ya Sh. 300,000, tofauti na wenzao kutoka Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, ambao wanalipwa Sh. 420,000 kwa siku.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamisi
Sadifa ndiye aliyemfuata Salome juzi baada ya kumkuta akifanya mahojiano na mmoja wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na kumuomba amsikilize yeye (Sadifa), kwa madai kwamba, ndiye alikuwa na taarifa sahihi za kumueleza kuhusu malalamiko hayo ya posho.
Mbali ya kulalamikia habari hiyo, Sadifa pia alihoji uamuzi wa NIPASHE kuchapisha picha yake gazetini.
Alisema hajui NIPASHE lilikoitoa picha yake iliyochapishwa ukurasa wa kwanza katika toleo la jana na sababu za kuichapisha bila kuomba kwanza idhini kutoka kwake.
Sadifa alidai maneno aliyonukuliwa na NIPASHE hayakutoka mdomoni mwake.
Alidai alichokisema ambacho hakikuandikwa ni kwamba, siyo wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba wanaopaswa kuongezwa posho kutoka Sh. 300,000 wanazolipwa sasa, bali ni wale 201 walioteuliwa na Rais.
Katika toleo la jana, NIPASHE ilimnukuu Sadifa akisema kuwa posho ya Sh. 300,000 wanazolipwa wajumbe kwa sasa ni ndogo, hasa ikizingatia kuwa wajumbe wengi wanatoka kwenye maeneo yao wameacha kazi zao na hawana mshahara.
Sadifa alisema iwapo maofisa wa Bunge walioandaa kanuni walitumia miezi nane na walilipwa fedha ya kutosha, iweje wajumbe ambao wana kazi kubwa walipwe fedha kidogo isiyotosheleza mahitaji.
Baada ya kutoa vitisho hivyo, Sadifa aliondoka eneo hilo na wakati anaingia kwenye ukumbi wa Bunge, alikutana na Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nasari, na Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, ambao aliwaonyesha namna NIPASHE lilivyochapisha habari hiyo.
Hata hivyo, Nasari na Lusinde walimweleza kuwa hawaoni tatizo kutamka yaliyonukuliwa na NIPASHE, kwani hata yeye hawezi kukataa kupokea kama posho hiyo itaongezwa.
Sadifa alijibu na kusema mshahara wa ubunge anaolipwa unamtosha, yeye, mkewe pamoja na mtoto wake mmoja, hivyo hata kama itatokea posho hiyo kuongezwa hawezi kuichukua.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.