Alitoa vitisho hivyo alipokutana na Salome, akiwa na waandishi
wengine, wakiendelea na kazi karibu na lango la kuingia na kutoka ndani
ya ukumbi wa mikutano ya Bunge linalotumiwa na wabunge, bungeni jana.
Akiwa ameshika nakala tatu za magazeti tofauti, likiwamo NIPASHE,
Sadifa alifika walikokuwa wamesimama waandishi hao na kuanza kuhoji
habari alizonukuliwa na NIPASHE na picha yake iliyochapishwa katika
toleo la gazeti hilo la jana.
Baada ya kukumbushwa kuwa alichokisema jana, ambacho ndicho
alichonukuliwa na NIPASHE, Sadifa alikana maneno yake, ambayo hakupenda
yaandikwe gazetini.
Alisema katika siku zijazo hatavumilia iwapo ataona zimeandikwa
habari, ambazo hazimpendezi na kwamba, kama zitaandikwa, atakachokifanya
ni kumpiga mwandishi ngumi.
“Mimi huwa nakung’uta ngumi. Na kwa kweli siku nyingine nitakuchapa,” alisema Sadifa.
Alitoa vitisho hivyo, baada ya gazeti hili jana kuchapisha kauli
aliyoitoa juzi akiungana na wajumbe wenzake wa Bunge Maalumu la Katiba
kutaka posho za kushiriki Bunge hilo ya Sh. 300,000 anazolipwa kila
mjumbe kwa siku ziongezwe.
Sadifa alinukuliwa na NIPASHE kufuatia mahojiano aliyoyafanya na
Salome katika viwanja vya Bunge, muda mfupi baada ya kuzuka bungeni
malalamiko kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kuhusu kulipwa
posho ya Sh. 300,000, tofauti na wenzao kutoka Baraza la Wawakilishi la
Zanzibar, ambao wanalipwa Sh. 420,000 kwa siku.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamisi
Sadifa ndiye aliyemfuata Salome juzi baada ya kumkuta akifanya
mahojiano na mmoja wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na kumuomba
amsikilize yeye (Sadifa), kwa madai kwamba, ndiye alikuwa na taarifa
sahihi za kumueleza kuhusu malalamiko hayo ya posho.
Mbali ya kulalamikia habari hiyo, Sadifa pia alihoji uamuzi wa NIPASHE kuchapisha picha yake gazetini.
Alisema hajui NIPASHE lilikoitoa picha yake iliyochapishwa ukurasa wa
kwanza katika toleo la jana na sababu za kuichapisha bila kuomba kwanza
idhini kutoka kwake.
Sadifa alidai maneno aliyonukuliwa na NIPASHE hayakutoka mdomoni mwake.
Alidai alichokisema ambacho hakikuandikwa ni kwamba, siyo wajumbe
wote wa Bunge Maalumu la Katiba wanaopaswa kuongezwa posho kutoka Sh.
300,000 wanazolipwa sasa, bali ni wale 201 walioteuliwa na Rais.
Katika toleo la jana, NIPASHE ilimnukuu Sadifa akisema kuwa posho ya
Sh. 300,000 wanazolipwa wajumbe kwa sasa ni ndogo, hasa ikizingatia kuwa
wajumbe wengi wanatoka kwenye maeneo yao wameacha kazi zao na hawana
mshahara.
Sadifa alisema iwapo maofisa wa Bunge walioandaa kanuni walitumia
miezi nane na walilipwa fedha ya kutosha, iweje wajumbe ambao wana kazi
kubwa walipwe fedha kidogo isiyotosheleza mahitaji.
Baada ya kutoa vitisho hivyo, Sadifa aliondoka eneo hilo na wakati
anaingia kwenye ukumbi wa Bunge, alikutana na Mbunge wa Arumeru
Mashariki (Chadema), Joshua Nasari, na Mbunge wa Mtera (CCM),
Livingstone Lusinde, ambao aliwaonyesha namna NIPASHE lilivyochapisha
habari hiyo.
Hata hivyo, Nasari na Lusinde walimweleza kuwa hawaoni tatizo kutamka
yaliyonukuliwa na NIPASHE, kwani hata yeye hawezi kukataa kupokea kama
posho hiyo itaongezwa.
Sadifa alijibu na kusema mshahara wa ubunge anaolipwa unamtosha,
yeye, mkewe pamoja na mtoto wake mmoja, hivyo hata kama itatokea posho
hiyo kuongezwa hawezi kuichukua.
No comments:
Post a Comment