Zikiwa zimebaki siku nne kabla ya
kuanza kwa Bunge la Katiba mjini Dodoma, Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), kimesema kitasusia bunge hilo, iwapo mapendekezo
yaliyotolewa na Tume ya Jaji Warioba hayatazingatiwa.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar
es Salaam na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakati alipokuwa
akitoa taarifa ya Mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho uliofanyika juzi,
kuzungumzia Bunge la Katiba, uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kalenga
na uamuzi kuhusu madiwani wake mkoani Arusha.
Mbowe alisema Chadema wanakwenda
kushiriki bunge hilo wakiwa na masikitiko kwa kuwa uteuzi wa wajumbe 201
uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete haukuwa na nia njema kwa taifa, kwani
asilimia 80 ya walioteuliwa ni wanachama wa CCM. "Tunakwenda Dodoma
lakini hatutakubali Bunge limilikiwe na wachache na hatutasita kurudi
kwa wananchi tutakapoona mapendekezo ya Jaji Warioba hayatekelezwi,"
alisema Mbowe.
Aliongeza kuwa Chadema hawaendi
bungeni kugoma ila wananchi wasishangae watakapoona wanatoka ndani ya
Ukumbi wa Bunge hilo, kwa kuwa lengo la uteuzi wa wajumbe lilikuwa ni
kutaka kupata wabunge wengi watakao unga mkono CCM.
"Kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano, CCM tayari wana wajumbe karibu asilimia 80, katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar
wana wajumbe karibu asilimia 68, kwa hiyo wanaweza wakakidhi vigezo vya
mshindi kupatikana kwa theluthi mbili ya kura zilizopigwa kufanya
uamuzi kwa niaba ya Bunge la Katiba," alisema Mbowe.
Hata hivyo, alisema Chadema hakitajali
maoni yatakayotolewa na CCM ikiwa yatazingatia maoni yaliyotolewa na
Tume ya Jaji Warioba.
"Tutafanya kazi na wajumbe wote
walioteuliwa na Rais, hatutawabagua kwasababu wametokea vyama gani,
hapana, ila tunachokitahadharisha ni kwamba wajumbe wote wataweka
masuala ya taifa mbele na hawataendekezwa na itikadi za vyama vyao.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment