Rais wa Zanzibar,Dk.Ali Mohamed Sheni
(kulia) akimtunuku Dkt.Salim Ahmed Salim nishani ya Mapinduzi ya
Zanzibar jana katika viwanja vya Ikulu ya Zanzibar jana.Picha na Michael
Matemanga |
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein
atawaongoza maelfu ya wananchi wa Zanzibar, kusherehekea miaka 50 ya
Mapinduzi ya visiwa hivyo leo.Sherehe hizo zinatarajiwa kuhudhuriwa
pia na Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine kutoka nchi mbalimbali
akiwamo Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Ikililou Dhoinine wa Comoro na
maseneta kutoka miji ya Lamu na Mombasa nchini Kenya, pamoja na
mwakilishi maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake Vuga mjini Unguja jana, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi
Seif Ali Idd alisema kuwa sherehe hizo ambazo ni kilele zitaanza saa
3.00 asubuhi baada ya viongozi wa kitaifa kuwasili, ambapo pamoja na
mambo mengine Dk Shein atalihutubia taifa hilo.
Uchunguzi unaonyesha kuwa, wananchi wa
visiwa hivyo wanamtarajia Rais Dk Shein kuzungumzia hali ya kiuchumi,
kisiasa na kudumisha usalama wa raia kutokana na vitendo vya watu
kumwagiwa tindikali, pia harakati za viongozi wa dini na wanasiasa
kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alipoulizwa kuhusu kualikwa kwa
aliyekuwa Sultan wa mwisho wa Zanzibar, Jamsheed Bin Abdullah, alisema
kuwa sherehe hizo zilikusudia kuwaalika watu mashuhuri kutoka nchi za
SADC na Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), lakini bahati mbaya
viongozi hao hawataweza kushiriki kutokana na kukabiliwa na majukumu
mengine.
Hata hivyo, alikiri kuwa Serikali ya
Awamu ya Tano chini ya Rais Dk Salmin Amour Juma, iliwahi kutoa msamaha
kwa sultani wa mwisho wa Zanzibar ikieleza kuwa mlango uko wazi na
anaweza kuitembelea Zanzibar kama mwananchi wa kawaida.
Maadhimisho ya leo yanafanyika ikiwa
ni miaka 50, baada ya Mapinduzi yaliyofanywa na Chama cha Afro Shiraz
Party (ASP), Januari 12, 1964 chini ya hayati Abeid Amani Karume,
aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ).
Mji wa Zanzibar umepambwa kwa picha za
viongozi kuanzia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tangu awamu kwanza hadi
ya saba, Bendera za Taifa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku mji ukiwa
katika hali ya usafi.
Sherehe hizo zinatarajiwa kupambwa na mambo mbalimbali, ikiwamo vikundi vya ngoma za asili na michezo mbalimbali ya kijadi.
No comments:
Post a Comment