Mamlaka ya Majisafi na Majitaka
Dar es Salaam (Dawasco), imesema inawadai wateja sugu Sh40 bilioni huku
ikiwataka kulipa madeni hayo ili kunusuru utendaji wake.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya mamlaka
hiyo kukatiwa huduma za umeme kutokana na kudaiwa Sh6.3 bilioni na
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Akizungumza ofisini kwake, Mtendaji Mkuu wa
Dawasco, Jackson Midala alisema deni hilo linahusisha baadhi ya taasisi
mbalimbali za Serikali na watu binafsi.
“Kuna Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi na wangine wengi, hatutawakatia
huduma kwa sababu ya madeni ila tunasisitiza kulipa madeni hayo ili na
tuweze kulipa mzigo wa madeni mengine ya umeme,” alisema Midala.
Pia, Midala alisema kuhusu hatua zinazoendelea
kuwashughulikia wateja wanaoiba maji kwa njia za kuharibu mita na
kwamba, mpaka sasa wamefanikiwa kuwakamata watu 284 na kuwafikisha
mahakamani.
Alisema miongoni mwa watu hao, watatu walihukumiwa
adhabu ya kifungo, watatu kesi zilifutwa kwa kukosa ushahidi na wengine
kesi zao zinaendelea.
“Wahalifu hao kuna vigogo na watu wa kawaida
ingawa baadhi yao walikuwa wanakiri mapema na kulipa faini, kwa mfano
Kampuni ya Struberg inayojenga barabara tuliwakamata wakiiba maji yetu
wakakiri na kulipia faini ya Sh27 milioni,” alisema Midala.
Aliwataka wateja kulipa ankara zao kwa muda, lengo likiwa ni kuwezesha mamlaka hiyo kujiendesha na kuendelea kuwapa huduma.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment