Wednesday, December 11, 2013

HUU NDIO WASIFU WA MANDELA

Katika uhai wake mpambanaji dhidi ya ubaguzi wa rangi duniani, Nelson Mandela, aliishangaza dunia alipotangaza msamaha kwa waliomtesa na akiwa marehemu, amekutanisha viongozi mahasimu wa kisiasa duniani katika uwanja mmoja wakimuaga. Hicho ndicho kilichomsukuma mshindi mwenzake wa Tuzo ya Nobel, Askofu Desmond Tutu, kusema Mandela alikuwa wa maajabu na alionesha maajabu akiwa hivi sasa ni marehemu.
Katika hafla ya jana, Rais Robert Mugabe alijikuta akikutana na mahasimu wake kisiasa, Rais Barack Obama na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.
Obama na Cameron waliweka vikwazo vya kiuchumi kwa Zimbabwe wakipinga matokeo ya uchaguzi uliompa Mugabe ushindi wa asilimia 61 dhidi ya wapinzani wake, wakidai kuwa kiongozi huyo alichakachua kura.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Natanyahu ambaye awali aliripotiwa kutokwenda, alifika na kukaa katika uwanja mmoja na Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, licha ya kuwa na ugomvi wa muda mrefu na unaoendelea baina yao.
Pia Rais Obama, alikutana na hasimu wa nchi yake wa siku nyingi, Rais Raul Castrol wa Cuba, ambao uhusiano wao umekuwa ukidorora tangu Mapinduzi ya Cuba ya mwaka 1959.
Kutokana na uhusiano mbovu kati ya nchi hizo, mpaka leo Marekani haina uhusiano wa kibalozi na Cuba, huku nchi hiyo ikiweka katika sheria zake vizuizi kwa kampuni za Marekani kufanya biashara na Cuba.
Nchini Marekani, wachambuzi wa kisiasa walishangazwa na uamuzi wa familia za kisiasa za Obama, George W. Bush na Bill Clinton, kupanda ndege moja kwenda Afrika Kusini kumuaga Mandela.
Rais mstaafu Bush kwa mara ya kwanza alipanda Air Force One, tangu amalize awamu yake ya kuongoza Marekani miaka mitano iliyopita. Kutokana na kutotarajiwa kwa tukio hilo, Obama na mkewe Michelle, walikwenda katika chumba cha Rais kilicho mbele ya ndege hiyo, lakini Bush na mkewe Laura, walilazimika kutumia chumba cha huduma ya kwanza ambacho pia hutumika kufanya operesheni ndege ikiwa angani.
Mkewe Clinton, Hillary alikwenda katika chumba cha maofisa wa ngazi za juu wa Serikali ya Marekani. Kutokana na hali hiyo, chumba cha mikutano kilitumika mara kadhaa kukutanisha vigogo hao wa kisiasa wa Marekani katika safari yao ya kwenda Afrika Kusini, iliyochukua saa 16.
Wachambuzi hao walielezea safari hiyo kuwa ya maajabu, kwamba Rais Obama, aliwakutanisha Rais aliyemtangulia, Bush na mgombea mtarajiwa wa urais wa Marekani, Hillary katika ndege moja, tukio ambalo halijawahi kutokea katika historia ya Marekani.
Mbali na tukio hilo la kihistoria, lingine katika historia ya nchi hiyo kubwa duniani, lilitajwa kwamba ni kuwapo kwa marais wanne wa Marekani kwa pamoja katika ardhi ya Afrika. Kwa mara ya kwanza ilitokea Tanzania, pale marais wawili wa Marekani, Obama na Bush walipokutana.
Lakini jana historia hiyo ilivunjwa baada ya Mandela kuwakutanisha Jimmy Carter, Clinton, Bush na Obama katika ardhi ya Afrika. Obama: Mandela ni shujaa Akizungumza jana kwenye tukio la kihistoria, Obama alisema dunia inaishukuru Afrika Kusini kwa kumtoa Rais Mandela ili atumike duniani kote.
"Ni heshima kuwa nanyi leo, kufurahia maisha ambayo hayana mfano wake. Watu kutoka aina zote za maisha, wanafurahia maisha ya Mandela, mapambano yake yalikuwa mapambano yenu na huzuni yake ilikuwa huzuni yenu," alisema Obama.
Obama alisema Mandela alikuwa shujaa wa mwisho wa karne ya 20 kwa vile alikuwa amedhamiria kuleta demokrasia na utawala wa sheria na alipokea tuzo alizostahili kwa kusimamia suala hilo. Alisema Madiba alikuwa mwepesi wa kukubali alipokosea:
"Tulimpenda sana...alikuwa mtu wa nyama na wa damu, alikuwa mwanamume wa uhakika, ndiyo maana tunajifunza mengi kutoka kwake”.
Obama alisema Mandela alitumia muda wake wa kuwa gerezani kwa kupigania watu wa Afrika Kusini. "Alitumia miongo kadhaa gerezani kwa ajili ya kutetea hoja yake...alijifunza lugha na desturi za wapinzani wake."
Obama aliongeza, kuwa Madiba aliifundisha dunia umuhimu wa kupambana kupitia majukwaa kwamba watu wanaweza kusimama wakapambana na kutetea misimamo yao. Ban Ki-moon na umoja Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) aliwaambia wananchi wa Afrika Kusini kuwa kifo cha Mandela kinapaswa kiwape matumaini na umoja zaidi kama njia ya kumuenzi kiongozi huyo wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini.
"Nina heshima kubwa kushiriki shughuli hii ya kitaifa ya kifo cha Mandela," alisema Ban na kuongeza:
"Kumbukumbu hii ipeleke ujumbe wa muungano wa kitaifa. Naamini kwa siku zijazo tutaona umoja zaidi miongoni mwa wananchi wa hapa kupitia majonzi haya."
Alisema Mandela alijitolea kwa kila kitu, kuhakikisha uhuru na demokrasia vinapatikana.
"Dunia imempoteza rafiki kipenzi na msimamizi. Alikuwa kiongozi mkubwa katika kipindi chetu hiki, alikuwa mwalimu na amekuwa mfano," alisema. Viongozi 90 wamuaga Zaidi ya viongozi 90 wa mataifa mbalimbali jana walishiriki siku ya kitaifa ya kumuaga Mandela.
Shughuli hiyo ya kitaifa ya kumwaga Mandela ilianza saa 5 asubuhi huku maelfu ya watu wakiimba nyimbo na wimbo wa taifa kama njia ya kuomboleza msiba huo mkubwa uliowapata. Naibu Rais wa ANC ambaye alikuwa mshereheshaji katika tukio hilo, Cecil Ramaphosa alianza kusherehesha kwa kusema:
"Uishi maisha marefu Nelson Mandela," kabla ya kuwakaribisha wanafamilia wa Mandela wakiwamo wake zake, Graca Machel na Winnie Madikizela-Mandela. Ramaphosa alitangaza viongozi kadhaa ambao wangewasili katika shughuli hiyo na akasisitiza kuwa hao ni sehemu ya mabilioni ya watu ambao wanashiriki shughuli hiyo ya kumuaga Mandela.
Alisema Mandela alipatwa na mateso wakati anapigania watu wa Afrika Kusini na baadaye akaja kuunganisha taifa hilo kati ya watu weusi na weupe. Kuhusu mvua iliyokuwa inanyesha, Naibu Rais wa ANC alisema ni ishara ya Mandela kuwa mwenye furaha na kwa desturi za kiafrika, mvua ni mibaraka ya mtu kukaribishwa mbinguni.
Viongozi wa dini Viongozi wa kidini waliendesha sala maalumu kwa ajili ya Mandela ambapo Rabbi Warren Goldstein alimlinganisha Mandela na Yosefu wa kwenye Biblia. Alisema kama ilivyokuwa kwa Yosefu, Mandela alikaa gerezani kwa miaka mingi na alipotoka alihubiri kusamehe na akawa kiongozi wa taifa lake. Iman Ebrahim Bham alisema Mandela katika uhai wake alipigania haki, usawa, amani na maridhiano.
"Madiba hakupoteza fursa ya kupatana na watu waliomkosea ." Askofu wa Kanisa la Anglikana la Cape Town, Thabo Makgoba alisema: "Tunasema kwako Madiba, umepigana vita umemaliza...kwa jina la Mungu aliyetuumba, tuliteseka na wewe, na tulifurahi na wewe. Nenda nyumbani Madiba".
Baada ya maombi hayo, Mwenyekiti wa ANC Baleka Mbete alianzisha wimbo wa 'hakuna kama wewe Mandela' hapa Setswana. Graca, Winnie wakumbatiana Winnie alipiga magoti kumsalimia Graca kabla hajaenda eneo alilotengewa kukaa katika shughuli hiyo ya kitaifa.
Wawili hao walijifunika vichwa kwa kofia maalumu na kuvalia makoti meusi nguo zinazovaliwa na watu waliofikwa na msiba. Baada ya kumsalimia, Winnie alikwenda eneo lake la kukaa ikiwa ni kiti cha tatu kwa Graca.
Wake hao wa Mandela walishangiliwa wakati wanawasili uwanjani hapo. Viongozi wa mataifa mbalimbali walianza kumiminika uwanjani hapo saa 5.30 asubuhi na walikuwa wanakaribishwa na Ramaphosa na kutambulishwa.
Viongozi wengine waliokuwapo, ni Makamu Rais wa China, Li Yuanchao; marais wa zamani wa Afrika Kusini , FW de Klerk na Thabo Mbeki na Katibu Mkuu wa UN, Ban na Rais wa Cuba, Raul Castro ambao walilakiwa kwa shangwe.
Hali ilikuwa tofauti kwa Rais Zuma ambaye alizomewa na waombolezaji huku mpinzani wake kisiasa Thabo Mbeki alishangiliwa.
Mbeki aliondolewa madarakani na ANC na Zuma kuchukua nafasi hiyo.
Umati ulianza kuzomea wakati Zuma alipowasili uwanjani hapo hadi alipofika kwenye eneo lake na kuketi. Kuzomea zaidi kuliongezeka baada ya jina la Zuma kutajwa na wakati majina ya marais wa zamani yalipotajwa kama Kgalema Motlanthe, Thabo Mbeki na FW de Klerk walishangiliwa.
Zuma, licha ya kuzomewa alionekana kutulia huku akifuta miwani yake akiwa ameketi katikati ya wake zake, Gloria Bongekile Ngema na Thobeka Stacy Mabhija. Umati pia ulizomea wakati luninga ya uwanjani hapo ilipomwonyesha Rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush.
Wageni wa kimataifa wakiwamo watu mashuhuri walifurika kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho kwa Nelson Mandela. Wageni hao walikuwa miongoni mwa umati mkubwa wa watu ambao waliojifunika miavuli kujikinga jua na hata mvua iliponyesha.
Wageni wengine waliofika uwanjani hapo pamoja na Ban, ni Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair na wengine wengi wakiwamo wanamichezo, wanamitindo na wasanii wa muziki.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroon na Rais wa Marekani, Barack Obama walifika baadaye wakati shughuli zikiwa zinaendelea. Obama aliwasili uwanjani hapo saa 7 mchana baada ya kukwama kwenye foleni barabarani iliyosababishwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wakienda FNB.
Askofu Desmond Tutu alifika uwanjani hapo akifuatana na wazee wengine ambao walishiriki kupinga ubaguzi wa rangi wakiwa na Mandela. Rais Zuma aliwasili akifuatana na maofisa wengine wa serikali yake na viongozi wa ANC.
Viongozi wengine ni Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye alishangiliwa alipotambulishwa, Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan; Rais wa India, Pranab Mukherjee na Rais wa Cuba, Castro Ruz.
Marafiki wa siku nyingi wa Mandela, Ahmed Kathrada na George Bizos pia walikuwa uwanjani hapo. Rais wa Mwisho wa Serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini, F.W. De Klerk alikuwapo na mkewe Elita Georgiades. Rais Jakaya Kikwete alikaribishwa uwanjani kwa Kiswahili “karibu ndugu yetu Kikwete”.
Hali ilivyokuwa FNB Hali katika uwanja wa FNB ilikuwa ni majonzi na uchangamfu kutokana na maelfu ya watu kuimba wakati wote na kucheza nyimbo za kumtukuza Mandela. "Mandela Rais wangu, Rais wangu!" Waliimba na kucheza nyimbo za ukombozi ambazo ziliimbwa kipindi cha kupigania uhuru wa Afrika Kusini. Baadhi ya waombolezaji walivalia kofia na mavazi ya rangi ya bendera ya Afrika Kusini huku wengine wakibeba picha za Madiba na baadhi ya mabango yaliyoandikwa ‘kalale pema peponi Tata’. "Nelson Mandela, akekho ofana nawe (hakuna kama wewe)," waliimba waombolezaji hao. Watu wakubwa kwa wadogo walikusanyika katika uwanja huo na Peter Diale ni mmoja wa watu ambao walikwenda na watoto wake wanne. "Ningependa watoto hawa wakumbuke kile ambacho Mandela alitufanyia sisi na aliyolifanyia Taifa lake. Ni kupitia kwake ndiyo maana tuna umeme, maji na nyumba bora," alisema Diale. Alikwenda na watoto wake kwa vile alitaka wawe na kumbukumbu nzuri ya tukio hilo na ukuu wa Mandela kwa watu wake. "Wamezaliwa chini ya Afrika Kusini huru. Kamwe hawatambui machungu ya ubaguzi tuliyopitia, ahsante sana Mandela." Wageni mbalimbali akiwamo Rais mstaafu Benjamin Mkapa, Rais Kikwete waliwasili uwanjani hapo saa 6.04 mchana. Treni ambayo ilibeba waombolezaji kuwapeleka katika uwanja wa FNB ilichelewa kwa dakika 30 kutokana na msongamano mkubwa wa abiria. Msemaji wa treni, Lilian Mofokeng alisema ilichelewa kutokana na msururu wa abiria kuliko ilivyotarajiwa. "Hii imetokana na umati mkubwa uliokuwapo na zaidi tuliangalia suala la usalama kwanza kwani watu wengi wamejitokeza kutaka kwenda kushuhudia shughuli hiyo ya kitaifa ya kumuaga Mandela. "Tumetafuta njia nyingine ikiwa ni pamoja na kuweka treni ya ziada ili kumudu kusafirisha umati huu." Milango ya uwanja wa Ellis Park wa Johannesburg pia ilifunguliwa ili kuwapa fursa watu kwenda na kufuatulia siku ya kitaifa ya kuaga mwili wa Mandela. Waziri anayehusika na Jeshi la Polisi, Nathi Mthethwa alisema alifarijika kuona mataifa duniani yakiungana na Waafrika Kusini katika kipindi hiki cha msiba wa Mandela na kuongeza: "Tutawapa ulinzi wa uhakika katika kipindi chote cha maombolezo haya." Familia ya Mandela ilielezwa kuwa iko imara katika kipindi hiki cha maombolezo, Meya wa Jimbo la Gauteng, Nomvula Mokonyane alisema jana.
"Familia ya Madiba ni familia ambayo iko imara na kipindi chote hiki cha msiba imeendelea kuimarika," alisema Mokonyane.
Shughuli katika uwanja wa FNB ilianza saa 5 asubuhi na Mokonyane ndiye alitoa neno la shukurani kwa wageni waliofika Afrika Kusini kuhani msiba wa Mandela. Mandela kama Musa Mmoja wa mawaziri katika serikali ya Zuma, Sibusiso Ndebele alimfananisha Mandela na Nabii Musa wa kwenye Biblia.
"Kupitia kwa Mandela, Mungu aliwapa watu wa Afrika Kusini kama ilivyo kwa Musa awavushe watu wake kutoka ubaguzi wa rangi hadi uhuru kamili," ilisema taarifa ya Waziri huyo.
Musa ni kiongozi anayetajwa katika Biblia kuwa aliyewatoa Wana wa Israel katika utumwa nchini Misri na kuwaanzishia safari ya kwenda Kanani. Ndebele ambaye alikuwa na Waziri wa Afya, Aaron Motsoaledi alisema Mandela alikuwa ni kwa Afrika Kusini na alikuwa ni kwa ajili ya Afrika hivyo ni lazima wajivunie kuwa naye.
Chanzo: Habari Leo

No comments:

Zilizosomwa zaidi