Saturday, November 2, 2013

TAMBWE AITOSA TIMU YAKE YA TAIFA

Amissi Tambwe akishangilia goli huku wachezaji wenzake wakimkimbiza kwa nyuma, Star huyo tegemeo Msimbazi amepeleka ombi katika timu yake ya taifa nchini Burundi ili asiweze kushiriki michuano ya Chalenj mwaka huu. Picha na Maktaba
AMISSI Tambwe amepanga kuiomba Burundi imuache apumzike asicheze michuano ya Chalenji mwezi huu, lakini straika huyo wa Simba ametamka kwa mdomo wake akisema Coastal Union na Ruvu Shooting zina mabeki wa maana.
Tambwe, ni kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu Bara akiwa ametikisa nyavu mara tisa huku akifuatiliwa kwa karibu na straika Hamis Kiiza wa Yanga mwenye mabao manane pamoja na Juma Liuzio wa Mtibwa Sugar na Elius Maguri wa Ruvu wenye mabao saba kila mmoja.
Mrundi huyo ambaye nchi yake inajiandaa na Kombe la Chalenji litakalofanyika Kenya baadaye mwezi huu, aliliambia Mwanaspoti akisema: “Kwa kweli naweza kusema Coastal na Ruvu Shooting ni timu ambazo zina mabeki wazuri kuliko timu nyingine tulizocheza nazo kwenye ligi hii ya Tanzania.”
Alisema kila alipopata mpira kwenye mechi hizo alijikuta akikabwa na mabeki zaidi ya watatu wa maana na walikuwa hawana papara tofauti na wa timu nyingine ikiwamo Yanga, ingawa katika mechi ya Ruvu alifanikiwa kufunga bao kwa penalti.
Akiizungumzia Simba kushindwa kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa kileleni, alisema: “Nafikiri imesababishwa na matokeo ya mechi mbili zilizopita ingawa naamini tunaweza kufanya vizuri kwenye mzunguko ujao.”
Kuhusu Burundi alisema: “Unajua nipo katika uchovu sana, nataka nikimaliza ligi nipumzike tu. Nasikia kuna Chalenji tena, hivyo nitazungumza na uongozi na kocha, waniache kidogo nipumzike kwa kipindi hiki.
“Unajua sijapata muda wa kupumzika kabisa, nikiwa Burundi nilicheza ligi kabla ya kumalizika tukaenda kwenye Kombe la Kagame na baada ya hapo nikaja hapa na kuanza ligi.
“Nataka kupumzika ili ligi ikianza, niwe vizuri na kasi mpya. Unajua unapofanya kazi sana kuna muda mwili nao unachoka na kushindwa kufanya kazi vile unavyotarajia.”
Mchezaji huyo ambaye amezoeleka kuandikwa ‘Amis’, amesema jina lake kwa usahihi linaandikwa ‘Amissi’.
Mpaka sasa ana mabao manane Ligi Kuu.

No comments:

Zilizosomwa zaidi