Friday, November 22, 2013

LORI LAUA MADEREVA WA BODABODA WATANO...



Waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda watano wa kituo cha Picha ya Ndege Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, wamekufa baada ya kugongana uso kwa usoni la lori.

Bodaboda hao walipatwa na mkasa huo wakati wakimfukuza mtu anayedaiwa kumpora mwenzao pikipiki.

Waligongwa na lori hilo aina ya Scania juzi saa 2:00 usiku katika eneo la Ruvu Darajani kata ya Vigwaza wakati wa kupishana nalo wakati likitokea Morogoro kuelekea Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Matei aliwataja waliokufa kwa kugongwa na lori hilo lililokuwa likiendeshwa na mkazi wa Kitunda, jijini Dar es Salaam kuwa ni  Saidi Dosa (17), Severine Luoga (19), Philemon Job ( 20),Nassoro Mzalamila  (18) na Sadam Mapunda (21 ).

Majeruhi ni Peter Maswaga (25 ), mkazi wa  Picha ya Ndege Wilaya ya Kibaha.
Kamanda huyo alifafanua kuwa chanzo cha tukio hilo ni mwendo kasi wa waendesha pikipiki watatu kati ya hao zenye namba T.164 CHF, T.953 CQB na T.426 CJZ.
Matei alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Tumbi Kibaha ikisubiri kufanyiwa uchunguzi wa daktari wakati majeruhi anaendelea na matibabu hospitalini hapo.

NIPASHE lilifika  eneo la tukio baada ya ajali hiyo kutokea na kushuhudia miili ya Said Ndosa na Severin Pangaras ikiwa imeharibika vibaya kutokana na kugongwa na lori hilo.

Vile vile lilishuhudia madereva wengine wanne Sadam Mohamed, Filemon Jobu, Nassor Zaramingo na Peter Maswaga wakiwa wamejeruhiwa vibaya kandokando ya barabara hiyo.

Baadhi walionekana kuvunjika miguu na kujeruhiwa vichwani.
Kadhalika NIPASHE lilishuhudia pikipiki tatu kati ya sita zenye namba T 164 CHF,T 953 CQB na T 426 CJZ zikiwa zimeharibika kutokana na kugongwa na lori hilo.

Mwenyekiti wa umoja wa waedesha pikipiki wa kituo hicho, Richard Mwanamalundi, alithibitisha wenzao watano kufariki dunia.
 Alisema ailifika Tumbi na kukuta madaktari wakifanya jitihada za kuokoa maisha ya wenzao bila mafanikio kwa kuwa kila mmoja alikuwa akifariki baada ya nusu saa.
Kuhusu majeruhi mwingine aliyenusurika, alisema alikuwa akiendelea kupatiwa matibabu.

Mwanamalundi alisema kabla ya msafara huo kuelekea Chalinze kumsaka mtuhumiwa wa uporaji wa pikipiki aliyedai ni mtoto wa miaka 16, Novemba 19, mwaka huu majira ya mchana, walipata taarifa kuwa imeonekana Msangani Kibaha.

Alisema taarifa hizo zilisababisha zaidi ya madereva 10 wakiwa kwenye pikipiki zao kufuatilia kuelekea Mlandizi baada ya kuelezwa kuwa mtuhumiwa alikuwa akikimbia kuelekea Chalinze.

“Kundi hilo la kwanza lilirudi na walipofika Kwa Matiasi njia panda ya barabara kuu ya Dar Salaam- Mororgoro ndipo walipopotezana na wengine waliamua kurudia Kibaha,” alisimulia.

Mwanamalundi alisema baadhi walishauriana kuwa warudi Picha ya Ndege, lakini wengine walishikilia msimamo wa kuhakikisha pikipiki hiyo inafuatwa na kupatikana, hivyo wakaanza kukimbizana kuelekea Chalinze na kugongwa na lori hilo katika eneo hilo la Darajani.

Tukio hilo lilivuta hisia za watu wengi na kukusanyika eneo hilo wakiwa katika makundi makundi.

Wengi wao walionekana kuwa na majonzi huku wakielezea kusikitishwa na ajali hiyo ambayo iliua vijana hao ambao ni ndugu, jamaa, marafiki na jirani zao. 
 
Chanzo: Nipashe

No comments:

Zilizosomwa zaidi