Tuesday, September 10, 2013

WAPONEA CHUPUCHUPU BAADA YA KUNYWA TOGWA HUKO IRINGA....

Watu 20, wakazi wa Kijiji cha Image Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, wamenusurika kufa baada ya kunywa togwa inayodaiwa kuwa na sumu wakati wa sherehe za kumuaga binti (send off) wa mzee John Kidava, ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.

Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Ramadhani Mungi, alisema tukio hilo limetokea jana katika kijiji hicho, ambapo watu hao walianza kuumwa matumbo dakika chache baada ya kunywa togwa hilo. 

Alisema baada ya tukio hilo, watu hao walikimbizwa katika zahanati ya kijiji hicho kupata matibabu na kwamba mmoja wao hali yake ilikuwa mbaya, hivyo kupelekwa rufaa katika Hospitali ya Misheni ya Ilula, ambako anaendelea kupatiwa matibabu.

Kamanda Mungi alisema uchunguzi wa awali, umebaini kuwa watu hao walidhurika na dawa iliyokuwa imewekwa kwenye mahindi kwa ajili ya kuua wadudu, kabla ya kusagwa na kutengenezwa togwa.

“Tumegundua kwamba ni dawa ambayo iliwekwa ili mahindi yasiharibiwe na wadudu, japo uchunguzi zaidi wa tukio hili unaendelea,” alisema Mungi.

Wakati huo huo, mtu mmoja amekamatwa na wengine watatu kusakwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumpiga hadi kumuua Johania Msinu (22), mkazi wa Kijiji cha Kibengu.

Kamanda Mungi alisema kuwa tukio hilo limetokea jana katika kijiji hicho na kumtaja aliyekamatwa kuwa ni Chesco Mhenzi (32), mkazi wa kijiji hicho.

Alisema kabla ya tukio hilo, watu hao kwa pamoja walikuwa wakinywa pombe na baadaye wakaanza kugombana, jambo lililosababisha mmoja wao kupoteza maisha baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani.

Alisema polisi inaendelea kuwatafuta wengine watatu, na kwamba watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

No comments:

Zilizosomwa zaidi