Kitengo cha kupambana na Malaria
Zanzibar (ZMPC) kimesema kinatarajia kuanza kampeni ya kuchunguza
malaria kwa wageni wote, watakaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege na
Bandari ya Malindi.
Ofisa mwandamizi wa kitengo cha
kupambana na malaria Zanzibar (ZMPC), Mwinyi Mselem alisema hayo wakati
alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea mikakati ya kupambana na
malaria nchini.
Alisema kitengo kimepanga kutekeleza
mikakati hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha kwamba ugonjwa wa malaria
unatokomezwa na hakuna njia za kuambukizwa kwa wananchi.
“Tunakusudia kuanzisha zoezi la kupima
afya za wageni wote wanaoingia nchini kupitia njia za uwanja wa ndege
pamoja na bandarini ili kujuwa afya za wageni wanaoingia nchini,”
alisema.
Alisema mikakati ya kitengo cha
kupambana na malaria ifikapo mwaka 2017 ni kuhakikisha ugonjwa huo
umetokomezwa na siyo tishio tena kwa afya za wananchi. Kwa sasa Zanzibar
imefanikiwa kushusha maambukizi ya ugonjwa huo kutoka asilimia 32 hadi
kufikia asilimia moja na kupunguza vifo vya akinamama na watoto.
Hata hivyo, Mselem alisema katika
kipindi cha miaka miwili sasa kumejitokeza maambukizi mapya ya malaria
kutokana na kuongezeka kwa uchafuzi wa mazingira na hivyo kupelekea mbu
kuzaliana zaidi.
Alisema kitengo cha kupambana na malaria kinatarajia kuanza kazi ya kupiga dawa majumbani pamoja na sehemu za mazalia ya mbu.
Mselem alisema kazi hiyo inatarajiwa
kuanza katika kipindi cha msimu wa mvua za vuli, ambazo huibuka kwa
mazalia mengi ya mbu yanayosababisha ugonjwa wa malaria.
Zanzibar inatajwa mfano wa kupambana na
ugonjwa wa malaria, ambapo hivi karibuni Rais mstaafu wa Marekani, Bill
Clinton alizindua mradi wa kupambana na ugonjwa huo wa kupima damu hapo
katika uwanja wa Amaan mjini hapa.
No comments:
Post a Comment