Mikoa mitano nchini inakabiliwa na uhaba
wa chakula na serikali imesema inajipanga kufanya tathmini
itakayobainisha hali halisi. Tathmini hiyo inayotarajiwa, itaangalia ni
kwa kiwango gani sanjari na kaya zilizoathirika katika mikoa hiyo ya
Arusha, Dar es Salaam, Manyara, Shinyanga, Simiyu na Tabora.
Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula nchini,
Karimu Mtambo alitoa taarifa hiyo jana Dar es Salaam kwenye warsha
iliyoandaliwa na mradi wa unaoangalia juu ya usalama wa chakula
ujulikanao Sera.
Hata hivyo, Mtambo alisema ipo mikoa
mingine yenye chakula cha kutosha kutokana na kuzalisha ziada. Nayo ni
Rukwa, Katavi, Ruvuma, Mbeya, Kigoma, Iringa, Kagera, Mtwara, Lindi na
Morogoro.
“Takwimu hizo ni za awali ambazo
tumezipata juzi jioni ingawaje bado serikali itafanya tathmini ya kina
kuona maeneo hayo yameathirika kwa kiwango gani na kaya ngapi ambazo
zitakuwa zimekosa chakula,” alisema Mtambo na kuongeza kuwa mikoa
mingine, imezalisha kwa kiwango cha kujitosheleza.
Mradi huo unaoendeshwa na Shirika la
Marekani la Feed the Future chini ya udhamini wa Shirika la misaada la
Marekani (Usaid), ulikuwa ukiwasilisha utafiti mbalimbali kuhusu usalama
wa chakula.
Katika warsha hiyo, Mtambo alifafanua kwamba uwiano wa kiwango cha njaa kwa mikoa hiyo kinatofautiana.
Tathmini hiyo imeonesha kiwango ambacho kiko chini ya asilimia 100 huku ikiwepo mikoa ambayo imezalisha zaidi hadi asilimia 120.
Alisema katika tathmini itakayofuatia
wataungana na wadau mbalimbali kujua watu walioathirika na wanahitaji
chakula kiasi gani. Kuhusu hali ya ghala la taifa alisema lengo lilikuwa
kuhifadhi chakula tani 250,000 na kwamba hadi kufikia sasa zipo tani
185,000 za nafaka.
Akizungumzia mradi wa SERA, Mshauri
Mwandamizi wa Sera za Kilimo, Alex Mkindi alisema unawasilisha kwa wadau
tafiti nne zinazohusu usalama wa chakula ikiwemo jinsi ya kuwa na njia
mbadala ya uwasilishaji wa chakula cha misaada kwa wenye upungufu wa
chakula hasa chenye lishe.
Alisema tafiti nyingine ni namna ya
kutazama hifadhi ya chakula ya taifa kujitathmini shughuli zake na
majukumu yake hususan uwezo wa kuhifadhi.
Pia kama hifadhi inaweza kusaidia
mashirika mengine, kuangalia vibali vya kuagiza chakula kama vinaweza
kukidhi matakwa ya usalama wa chakula na kuwa na sera endelevu za kilimo
zitakazoangalia usalama wa chakula.
No comments:
Post a Comment