Wednesday, September 18, 2013

LITA 29 ZA TINDIKALI ZAKAMATWA ZANZIBAR

Siku chache baada ya Padri wa kanisa katoliki, Parokia ya Machui Padri Anselm Mwang'amba kumwagiwa tindikali Zanzibar,Polisi kisiwani humo imekamata lita 29 za tindikali zilizo katika magaloni yenye ujazo tofauti.
 
Kamishna Mkuu Jeshi la Polisi Zanzibar Mussa Alli Mussa alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu mjini humo.
"Jeshi la polisi limekamata watu 15 kwa makosa mbalimbali, wapo tunaowahoji kuhusu kuwa na kundi la mtandao wa Al-shabab na pia wapo tunaowahoji kwa kujihusisha na matukio ya tindikali hawa tunataka kujua wameipata wapi nani kawapa na kwa minajili ipi," alisema Kamanda Mussa.
 
Alisema katika operesheni hiyo jeshi hilo linawahoji waliopata vibali vya kuwa na tindikali wamepewa na nani waweze kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

“Tunawaomba wananchi waendelee kutuunga mkono katika mapambano haya kwa kutupa taarifa za watu wanaojihusisha na uhalifu wa kutumia tindikali kwa kuwadhuru watu wengine.

“Mapambano dhidi ya jinamizi la tindikali ni makubwa na ni zaidi ya wengi wanavyofikiria. Tuvumiliane kwani upo uwezekano mkubwa wa mapambono haya kuwahusu jamaa zetu na wakati mwingine hata viongozi katika serikali,” alisema.

Alisema matukio yaliyopita ya kuwamwagia tindikali watu wasiokuwa na hatia ikiwamo kesi ya Sheikh Soraga, upelelezi wake umekamilika na jalada limefikishwa kwa mkurugenzi wa mashtaka kwa ushauriwa sheria.

Kamanda Mussa alisema suala la raia wawili wa Uingereza upelelezi wake upo hatua za mwisho.

Alisema jeshi la polisi kwa kushirikiana na ofisi ya mkemia mkuu na taasisi nyingine imeanzisha operesheni maalum yenye lengo la kupunguza matumizi holela ya tindikali nchini.

Kamanda alisisitiza kuwa operesheni hiyo itawalenga waingizaji tindikali nchini, wasambazaji, wauzaji na watumiaji holela.

Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto kubwa kuhusu udhibiti wa moja kwa moja wa tindikali ikizimgatiwa inatumika katika viwanda na sehemu nyingine za mitambo.

No comments:

Zilizosomwa zaidi