Wednesday, September 18, 2013

JOHARI AKIRI KUZICHAPA NA HANSI CHUU KISA PENZI LA RAY

 
 Waigizaji wenye majina makubwa Bongo, Blandina Chagula ‘Johari’ na Chuchu Hans wanadaiwa kuchapana kisa kikidaiwa kuwa ni penzi la mwigizaji Vincent Kigosi ‘Ray’,
 
Kwa mujibu wa chanzo ambacho ni rafiki wa karibu wa wasanii hao, tukio hilo lilijiri mwishoni mwa wiki iliyopita ndani ya Ofisi za RJ Productions, zinazomilikiwa kwa ubia wa Ray na Johari zilizopo Sinza-Mori jijini Dar ambapo Johari alikuwa akimtuhumu Chuchu mambo mazito ya kimapenzi kwa Ray.
Siku ya tukio Johari na wasanii wenzake walikuwa wakirekodi filamu ndani ya hoteli moja (jina tunalo) iliyopo jirani na ofisi hizo ndipo alipofikishiwa habari kuwa Chuchu yuko kwenye ofisi hizo ‘akijiachia’ na bosi mwenzake (Ray), jambo lililotia ganzi moyoni mwa mdada huyo.

‘Kikulacho’ huyo aliendelea kudai kuwa baada ya Johari kupata habari hizo, bila kujiuliza wala kuvuta subira, ‘alisaga soli’ hadi maeneo hayo.
“Alipofika aliingia ndani moja kwa moja na kumvamia Chuchu huku akimshushia kipigo chenye ujazo,” kilidai chanzo hicho.
Alidai kuwa katika timbwili hilo, Chuchu naye alifurukuta ndipo wakazichapa laivu kabla ya Ray aliyekuwa nje kusikia na kuwahi kuokoa jahazi.
“Unajua kilichomshtua Ray ni kilio cha Chuchu aliyekuwa akiomba msaada baada ya kuzidiwa na Johari,” kilidai.
Chanzo kilidai kuwa aliingia ndani akiwa amefura na kufoka lakini alikuwa ameshachelewa kwani tayari Johari alikuwa ameshaugeuza bucha mwili wa Chuchu.
Ilidaiwa kuwa baadaye Ray alimtoa nje Johari akimtaka kuwa mbali na Chuchu.
 
“Ilikuwa ni bonge la soo, watu walijaa sana, baadaye Ray alimtoa Johari nje huku akimfokea.
“Unaambiwa Johari alikuwa akikimbia na Ray kumfukuza, jambo lililovutia watazamaji wa sinema hiyo ya bure,” alisema mpashaji wetu.

Baada ya kuzinyaka taarifa hizo, gazeti hili liliwasaka Johari na Chuchu kwa nyakati tofauti.

Kwa upande wake Johari alikiri kutokea kwa kasheshe hiyo.
“Ni kweli lakini nani amekuambia? Unajua kilichoniudhi mimi ni maneno machafu ya huyu dada (Chuchu) anavyotamba kwa watu kuwa amenipokonya mume, wakati hakuna ukweli juu ya hilo, nilishikwa na hasira sana ndiyo maana nikaamua kumpa somo kidogo.
“Inaniuma kwa sababu mimi na Ray tumetoka mbali sana hadi kuisimamisha RJ. Tulikuwa hatuna kitu kabisa tukaungaunga huku na kule hivyo Chuchu anapaswa kutambua hilo. Asitake kunikumbusha vitu vingi kwa sababu tuliteseka sana,” alisema Johari kwa uchungu.

“Tangu ile ishu itokee sijaenda RJ kwa sababu Ray alinifukuza eti kisa Chuchu. Usiniulize muafaka wa hili jambo kwa sababu hadi sasa sina majibu ya moja kwa moja kuna vitu naviweka vizuri,” alisema mwanadada huyo.


Kwa upande wake Chuchu aliruka kimanga kuwa hakuna ishu kama hiyo.
“Aaah, jamani sina cha kusema juu ya hilo, nikiwa tayari nitawaambia.
“Kinachonishangaza kila Johari na Ray wakigombana huwa natajwa mimi. Yaani sijui hata haya mambo yanatokea wapi,” alisema Chuchu.
RAY
Ray kutaka kujua ukweli wa ishu hiyo, bila kujibu ndiyo au hapana, alimjia juu mwandishi:
“Sikia Brighton (mwandishi), hili jina nimelitafuta kwa miaka mingi. Nakuomba usiandike habari hiyo, sielewi chochote.
“Ugomvi wao siujui na wakigombana waache kunitaja, waeleze sababu zao za kugombana siyo kunitajataja mimi,” alisema Ray na hata alipoulizwa uhusiano wake na wanawake hao aliishia kujiumauma bila kutoa majibu ya kueleweka.

No comments:

Zilizosomwa zaidi