Watumiaji wa simu wapatao milioni nane wapo hatarini kufungiwa
simu zao ifikapo mwishoni mwa mwezi huu, Tanzania Daima limebaini.
Tayari Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeziandikia kampuni za simu
waraka wa kuzitaka zianze kukata kodi mpya ya laini (simu card) mara
moja kuanzia Julai 30, 2013.
Hatua hiyo inatokana na serikali kushindwa kufuta kodi hiyo ya sh
1,000 iliyopitishwa na Bunge kama alivyoagiza Rais Jakaya Kikwete baada
ya kukutana na wadau wa sekta ya mawasiliano.
Kwa maana hiyo kila anayemiliki laini moja ya simu atakatwa sh 3,000;
anayemiliki laini mbili sh 6,000 na anayemiliki laini tatu sh 12,000,
lengo ni kuhakikisha serikali inakusanya sh bilioni 178 zitakazopelekwa
kwenye bajeti kuu ya serikali.
Watumiaji wa simu sasa watalazimika kulipia kodi hiyo ya miezi mitatu ya Julai, Agosti na Septemba kwa wakati mmoja.
Bunge kupitia Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge (CCM) lilitaka kuwapo kwa kodi hiyo ili
kusaidia shughuli za bajeti ya Serikali Kuu.
Kupitishwa kwa kodi hiyo kuliibua malalamiko ya wanasiasa dhidi ya
Chenge anayelazimisha kuwapo kwa kodi hiyo, huku akishindwa kuamini
kwamba kuna Mtanzania anayekosa sh 1,000 kwa mwezi kwa ajili ya laini ya
simu.
Malalamiko hayo yaliendelea hadi kwa wananchi na baadhi ya wabunge wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliotaka posho za wabunge
zipunguzwe ili kuziba pengo hilo badala ya kuwabebesha wananchi mzigo.
Inadaiwa kwamba msimamo wa Chenge unaungwa mkono na Spika wa Bunge,
Anne Makinda, jambo lililosababisha kutojadiliwa kwa hoja binafsi ya
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA) iliyohusu kodi hiyo katika mkutano
wa Bunge lililopita kwa kisingizio cha kukosekana kwa muda wa kufanya
hivyo.
Hata hivyo, takwimu zilizotolewa na kampuni za simu zinaonyesha kuwa
miongoni mwa wamiliki wa laini za simu milioni 22; milioni nane
wanatumia chini ya sh 1,000 kwa mwezi.
Baada ya malalamiko hayo, Rais Kikwete alikutana na wadau wa
mawasiliano ambao ni wamiliki wa kampuni za simu Tanzania (MOAT), Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Waziri
wa Fedha, William Mgimwa, kisha kuwaagiza waiondoe kodi hiyo.
“Rais alisema lengo kuu la mkutano huo liwe kupendekeza jinsi ya
kuziba pengo la sh bilioni 178 zitakazopotea katika bajeti iwapo kodi
hiyo itafutwa.
“Alisema hawezi kuifuta moja kwa moja kodi hiyo, bila kutafuta njia
nyingine za kupata fedha kujazia pengo litakalotokeza huku tayari Bunge
limezipangia matumizi,” alinukuliwa Makamba baada ya kikao hicho na
rais.
Kwa upande wake, rais alikaririwa akiwaambia wadau hao wa mawasiliano
kwamba: “Nakuombeni kaeni pamoja, wekeni bongo zenu pamoja, wekeni akili
yenu pamoja tutafute namna gani tutajaza pengo hili la sh bilioni 178
endapo tutakubaliana kuwa kodi hii inawabebesha wananchi mzigo mzito, na
kuwa pengine menejimenti ya kodi yenyewe ni ngumu.”
Licha ya agizo hilo la rais kutekelezwa kwa MOAT kutakiwa kuongeza
kodi nyingine iitwayo ‘Excise duty’ kutoka asilimia 14 hadi 17 bila
kujali kwamba katika Bunge la bajeti kodi hiyo iliongezwa kutoka
asilimia 12 hadi asilimia 14, tozo hiyo ya laini za simu haijaondolewa.
Wachambuzi wa masuala ya siasa na mawasiliano walisema kutojadiliwa
kwa mabadiliko ya kodi hiyo ya simu ni dalili kwamba Waziri wa Fedha
amezidiwa nguvu na kiti cha spika kinachounga mkono hoja hiyo ya Chenge
na kushindwa kutekeleza agizo la rais.
Wataalamu wa mawasiliano walilieleza gazeti hili kwamba kuongezeka kwa
kodi hiyo kutaifanya Tanzania kuwa na kiwango cha juu cha kodi kuliko
nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ushauri wa wataalamu hao ulibainisha kwamba kuongezeka kwa kodi hiyo
kunaleta nafuu kidogo kuliko ile ya laini za simu inayomuumiza zaidi
mwananchi wa kawaida.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment