Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametengua tangazo la Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki la kuligawa eneo la Pori
Tengefu la Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha kwa kutenga
kilomita za mraba 1,500 kwa ajili ya uhifadhi na kilomita za mraba 2,500
kuwa chini ya Serikali za vijiji.
Machi 19, mwaka huu, Waziri Kagasheki alitoa tangazo la Serikali la
kuligawa pori hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 4,000 ili Serikali
iweze kuhifadhi eneo la kilomita za mraba 1,500 ambalo alieleza kuwa ni
mapito na mazalia ya wanyamapori, pia kutunza ikolojia ya Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti. Tangazo hilo liliibua mgogoro mkubwa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika eneo la Waso jana baada ya
kutembelea eneo la mgogoro na kufanya kikao na ujumbe wa mawaziri
alioambatana nao na watendaji wa wizara mbalimbali, Waziri Mkuu alisema
amefikia uamuzi wa kuondoa tangazo hilo la Serikali na sasa wananchi wa
eneo hilo wataendelea na utaratibu uliozoeleka.
Mawaziri waliokuwa katika ziara hiyo ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith
Mahenge, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Benedict Ole
Nangoro na Naibu Waziri (Tamisemi), Kassim Majaliwa.
“Mara baada ya lile tangazo kuliibuka mgogoro wa wananchi kupinga na
baadhi ya viongozi walinifuata hadi Dodoma na kuniletea malalamiko yao.
Pia CCM iliunda tume na kunipa taarifa lakini nikasema siwezi kutoa
uamuzi hadi nifike mwenyewe katika eneo hili na sasa nakubaliana na hoja
za wananchi kuwa kuligawa eneo kutakuwa na athari kwenu, naomba sasa
mwendelee na utaratibu wenu kama vile halikuwepo tangazo hilo,” alisema
Pinda.
Alisema miongoni mwa hoja za wananchi zilizosababisha afikie uamuzi huo,
ni kuwa eneo hilo la kilomita za mraba 1,500 ndilo ambalo lina vyanzo
vya maji vinavyotegemewa na vijiji vyote sita ambavyo vingeathiriwa na
tangazo hilo. Vijiji hivyo ni Ololosokwani, Soitsambu, Olorieni
Magaiduru, Arash, Piyaya na Oloipili.
Waziri mkuu pia alisema eneo hilo lililotengwa kwa uhifadhi ndilo
tegemeo la wananchi kwa ajili ya malisho ya mifugo hasa nyakati za
kiangazi, pia kuna makazi ya watu, shule na huduma nyingine muhimu.
Alisema kutokana na uamuzi huo, Serikali inajipanga kuandaa mpango wa
matumizi bora ya ardhi katika wilaya hiyo ili kutambulika maeneo ya
ufugaji, makazi, kilimo na uhifadhi ili masilahi ya kila upande
yaendelee kulindwa.
“Utaratibu wenu mliojiwekea kabla ya tangazo la Serikali uendelee kwani
tunataka shughuli za uwindaji wa kitalii ziendelee, upigaji picha
uendelee, pia ufugaji uendelee na hapa ni vyema kukawa na vikao vya
wadau wote walau kila baada ya miezi mitatu,” alisema Pinda.
Waziri Mkuu aliagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Halmashauri ya
Ngorongoro kuratibu vikao hivyo kwani lengo ni kutatua migogoro na
kurejesha uhusiano.
Wakazi Loliondo vicheko
Mara baada ya Waziri Mkuu kutangaza uamuzi huo, shangwe zilitawala na
Mbunge wa Ngorongoro, Saning’o ole Telele na madiwani wakiongozwa na
Mwenyekiti wa Halmashauri, Elias Ngolisa walieleza kuridhishwa na uamuzi
huo wakisema umezingatia kilio cha mamia ya wananchi wa Tarafa za
Loliondo na Sale.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Ortello Business Co operation (OBC), ambayo
ingebaki katika eneo lililokuwa limetengwa kwa uhifadhi, Isack Mollel
alisema hapingi uamuzi huo lakini anataka mashirika yasiyo ya kiserikali
(NGOs) wilayani Ngorongoro, kukubali mwafaka huo pia kushiriki katika
vikao vya kupanga matumizi bora ya ardhi vijijini muda ukifika.
Hata hivyo, kabla ya kutangazwa kwa uamuzi huo, Mollel alisema Serikali
isipotenga sasa maeneo ya uhifadhi na ufugaji, shughuli za utalii
zitakufa Loliondo sambamba na kuathirika eneo zima la ikolojia la
Serengeti kwani mifugo imeongezeka na imeanza kuingia hadi ndani ya
Hifadhi ya Serengeti.
Profesa Tibaijuka atoa suluhu
Awali, Profesa Tibaijuka alisema suluhu ya migogoro ya ardhi Loliondo ni
kuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi baada ya vijiji kupimwa kazi
ambayo alikwishaianza.
Alisema umefika wakati pia kwa wafugaji wa Loliondo kupunguza mifugo na kuanza kufuga kisasa kwani ardhi haiongezeki.
Chanzo Mwananchi.
No comments:
Post a Comment