Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amepokea kwa mfadhaiko, mshituko na huzuni kubwa taarifa za shambulio la
mlipuko lililotokea katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) mjini Arusha jioni ya leo, Jumamosi, Juni 15, 2013, tukio
ambalo limesababisha vifo vya watu wawili na majeruhi ya Watanzania
kadhaa.
Aidha,
Rais Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa jamaa na ndugu wa wafiwa
wote na pia ametuma pole nyingi kwa majeruhi ambao wameumizwa na
kujeruhiwa katika tukio hilo ovu na katili.
Vile
vile, Rais Kikwete amewatumia salamu za pole viongozi wa CHADEMA
kufuatia tukio hilo la woga mkubwa na pia kuviagiza vyombo vya ulinzi na
usalama kuchukua hatua stahiki za kuchunguza kwa haraka, kubaini,
kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria wote waliohusika na tukio
hilo, wawe watu wa ndani ya nchi ama nje ya nchi.
Katika
salamu zake za rambirambi na za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Mheshimiwa Magesa Mulongo, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa
mfadhaiko, mshituko na huzuni kubwa shambulio la mlipuko lililotokea
katika mkutano wa CHADEMA mjini Arusha jioni ya leo, tukio ambalo
limesababisha vifo na majeruhi ya Watanzania wenzetu.”
Amesema
Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Magesa
Mulongo salamu zangu za rambirambi kufuatia vifo na pole nyingi
kutokana na majeruhi katika tukio hilo na naomba kupitia kwako
unifikishie salamu zangu za rambirambi kwa jamaa na ndugu wa wafiwa na
pole nyingi sana kwa majeruhi.”
“Kadhalika
naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa viongozi na wanachama wa
CHADEMA kutokana na tukio hilo. Naomba uwajulishe kuwa uchungu wao ni
uchungu wetu sote na msiba wao ni msiba wetu pia. Nataka
wajue kuwa tupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi na
huzuni mkubwa,” amesema Mheshimiwa Rais Kikwete.
Rais
Kikwete amemwambia Mkuu wa Mkoa wa Arusha: “Kadhalika, nimeviagiza
vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za haraka kuwasaka wahusika,
kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Aidha, nawataka
viongozi wa Serikali ngazi ya kitaifa, Mkoa wa Arusha na Wilaya ya
Arusha mjini kuhakikisha kuwa majeruhi wote wanapata matibabu ya haraka
na huduma za tibabu stahiki.”
Aidha,
Rais Kikwete ametoa wito maalum kwa wananchi akisema: “Kwa wananchi
wenzangu, Watanzania wenzangu, napenda kutoa wito wa kuviachia vyombo
vya ulinzi na usalama kufanya kazi yao vizuri ili tuweze kuwabaini waovu
waliofanya kitendo hiki.”
“
Natambua kuwa yatakuwepo maneno mengi na hisia mbali mbali
zitakazojaribu kulielezea tukio hilio ovu na katili kwa njia mbali
mbali. Nawasihi tujiepushe na kuchukua dhana na hisia zetu au maneno ya
watu wengine kuwa ni ukweli wa tukio hili. Tujipe nafasi ya kutafakari
vizuri na kufanya uamuzi ulio bora.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Mimi siamini kuwa Watanzania au wafuasi wa vyama vya
siasa wanachukiana kiasi cha kufanyiana matendo ya unyama wa aina hii.
Naamini kuwa hiki ni kitendo cha mtu ama watu wasioitakia mema nchi
yetu, watu ambao wanatafuta kila sababu ya kupandikiza chuki miongoni
mwa raia ama makundi ya raia, ili nchi yetu iingie kwenye machafuko
makubwa.”
“Ndugu zangu, Watanzania wenzangu, naomba tuzinduke, ili
tusiwape nafasi watu hawa waovu ya kuweza kutimiza malengo yao ya
kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu kwa kuleta mifarakano baina yetu.
Mungu Ibariki Tanzania, Munfu Ibariki Afrika.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment