Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Mwanamrisho Taratibu
Abama jana alianguka ghafla katika Viwanja vya Bunge wakati akijiandaa
kuhudhuria semina ya wabunge ya kujadili rasimu ya Sera ya Gesi asilia.
Mapema asubuhi mbunge huyo alionekana katika Viwanja vya Bunge kabla semina kuanza, lakini ghafla alianza kujisikia vibaya.
“Mheshimiwa leo (jana), alifika kama kawaida,
lakini ghafla alisema hajisikii vizuri, hivyo tulimshauri akae chini
kwanza kabla ya kwenda katika semina,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa
Bunge ambaye hakutaka kutaka jina lake.
Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, mbunge huyo baada
ya kukaa kwa muda alianza kuishiwa nguvu na kuanguka ndipo wafanyakazi
wa Bunge walipomsaidia kwa kumpeleka katika Zahanati ya Bunge.
Baada ya mbunge huyo kuingia katika chumba cha
daktari alipewa huduma ya kwanza na kutundikiwa ‘dripu’ kabla ya kupewa
rufaa kwenda Hospitali ya Mkoa Dodoma.
Tukio hilo lilotokea saa 5.30 asubuhi na kusababisha baadhi ya wabunge na wafanyakazi kupigwa butwaa.
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alipoulizwa
kuhusiana na tukio hilo alisema; “Ndiyo kwanza nimefika na mimi
nimezisikia habari hizo, lakini bado sijapata taarifa rasmi.”
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Dodoma, Zainabu
Chaula alithibitisha mbunge huyo kupokewa hospitalini, lakini alikataa
kueleza kinachomsumbua kwa maelezo kuwa ugonjwa ni siri ya mhusika.
Mapema Machi mwaka huu, mbunge wa Chambani Salim
Hemed Khamis (CUF), alianguka alipokuwa akihudhuria vikao vya Kamati za
Bunge katika Ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam. Mbunge huyo
alipelekwa hospitali kwa matibabu, lakini baadaye alifariki dunia.
Aidha, Aprili 14 mwaka jana, mbunge wa Viti
Maalumu (CUF) Clara Mwaituka alianguka ghafla alipokuwa akihudhuria
vikao vya Bunge mjini Dodoma, ambapo alipatiwa matibabu na kupona.
No comments:
Post a Comment