Wazazi wilayani Mkuranga wamebuni mbinu
mpya ya kuwaachisha shule watoto wa kike, ambapo wanashirikiana na
baadhi ya walimu kuandika ripoti za uongo kwamba mabinti hao wamefariki
dunia.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa
baada ya wazazi kubanwa na Serikali wanapowaachisha mabinti zao shule
kwa lengo la kuolewa, wengine wamebuni mbinu za kusingizia vifo kwa
mabinti hao.
Kwa mujibu wa uchunguzi gazeti hili kuna idadi
kubwa ya wanafunzi wa kike katika shule za sekondari na msingi, ambao
wameacha shule baada ya kupata ujauzito na wengine kuolewa.
Taarifa za uchunguzi zilibaini katika shule za
sekondari za Kizomla na Mgulani zaidi ya wanafunzi ishirini (majina
tunayo) walipata ujauzito na watano waliolewa kati ya mwaka 2009 na
2012.
Akizungumzia utoro na upungufu wa wanafunzi
shuleni hapo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Frank Mjenga alisema kuwa
wanafunzi wanazidi kupungua kutokana na utoro, kupata mimba pamoja na
kukosekana kwa mazingira rafiki kwa wanafunzi.
“Hawa wanafunzi wanapungua kwasababu ya uzembe…kwa
mfano mwaka huu nimepewa wanafunzi 18 tu, darasa linatakiwa kuwa na
wanafunzi 40,” alisema Mjenga.
Mkazi wa kijiji cha Mgulani, Jafari Jongo alisema
kuwa kuna wazazi ambao wanashirikiana na walimu kuwatorosha wanafunzi na
kuwaoza kwa kutumia njia mbalimbali kuficha ukweli.
“Imetokea mara mbili hapa katika Shule ya Msingi
Mgulani, wazazi walishirikiana na walimu kuwaozesha wanafunzi halafu
wakaandika kuwa wanafunzi hao walifariki dunia, ili viongozi wa juu
wasifuatilie,” alisema Jongo.
Kwa mujibu wa Jongo ‘mchezo’ huo hufanywa kwa
ushirikiano mkubwa kati ya walimu na wazazi ambao huwasafirisha
wanafunzi walioolewa na kwenda kuwaficha katika vijiji vya mbali.
Naye Mariam Amrani mkazi wa Mgulani, akizungumzia
tatizo la kuwazushia vifo mabinti kwamba aliwahi kusikia walimu wakifuta
jina la mwanafunzi wa kike, kwa maelezo kwamba amefariki dunia.
Kauli ya walimu
Mwalimu Frank Manonge ambaye anafundisha Kemia
katika Shule ya Sekondari Kizomla alisema kinachosikitisha zaidi ni
namna baadhi ya wazazi wanawachukia walimu ambao wanapambana na vitendo
vya kuwaoza wanafunzi.
“Tumeshuhudia wanafunzi wakipata mimba na wengine wakiolewa na
kuacha masomo, lakini kitu cha kushangaza baadhi ya wazazi wanavifurahia
vitendo hivyo kwa kuwafanyia sherehe wanafunzi wanaoolewa huku
wakiwaachukia walimu wanaopinga ndoa hizo,” alisema Manonge.
Manonge alisema kuwa katika moja ya mikutano ya
shule, mzazi mmoja alisimama na kuwafokea walimu kwa vitendo vyao vya
kufuatilia watoto wa kike, wanapotoroshwa shule na kupelekwa kuolewa.
“Tuliwahi kushiriki kikao mzazi mmoja alisimama na
kuwatisha walimu wanaofuatilia masuala ya mapenzi kwa wanafunzi.
Akisema “yanawahusu nini mambo yao,” alisema mwalimu Frank Manonge.
Mwalimu anayefundisha katika Shule ya Msingi
Mgulani ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa kuhofia usalama
wake, alisema habari kuhusu kuwepo kwa taarifa za mwanafunzi kuandikwa
kwenye kitabu cha orodha cha wanafunzi kuwa alifiriki ili kwenda kuolewa
zilienea kijijini lakini si za kweli kwa kuwa hakuna anayeweza
kuthibitisha.
“Taarifa hizo zimekuwepo kijijini hapa na hivyo
ndivyo inavyoaminika, lakini hakuna mtu anayeweza kuzithibitisha kwa
kuwa imebaki kuwa siri kati ya wahusika,” alisema mwalimu huyo na
kuongeza kuwa ni kweli wazazi wanashiriki kuwaoza binti zao.
Akizungumzia tatizo la wanafunzi kuolewa na
wengine kupata mimba, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kizomla,
Frank Mjenga alisema wanafunzi wengi wanapata mimba kutokana na
utamaduni wa wakazi wa wilaya hiyo wa kuwacheza ngoma watoto wakiwa bado
wana umri mdogo na hivyo kuchochea kufanya vitendo vya ngono.
Akizungumzia utoro na upungufu wa wanafunzi
shuleni hapo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Frank Mjenga alisema kuwa
wanafunzi wanazidi kupungua kutokana na utoro, kupata mimba pamoja na
kukosekana kwa mazingira rafiki kwa wanafunzi.
“Hawa wanafunzi wanapungua kwa sababu ya uzembe…,
kwa mfano mwaka huu nimepewa wanafunzi 18 tu, darasa linatakiwa kuwa na
wanafunzi 40,” alisema Mjenga.
Francis Gewe ambaye mwanafunzi wake anasoma katika
Shule ya Msingi Mgulani, alisema kama hatua za haraka hazitachukuliwa
kudhibiti vitendo vya wanafunzi kupata mimba na kuolewa itafika wakati
wazazi hawatawapeleka wasichana shuleni.
“Ukigeuka huku huyu binti yake kapata mimba,
mwingine kaolewa. Itafika wakati wazazi wataona haina muhimu kuwapeleka
shuleni watoto wa kike,” alisema Gewe.
Kauli ya Serikali
Akizungumzia suala hilo, Ofisa Elimu Utawala,
Wilaya ya Mkuranga, Elizabeth Ngonyani alisema kuwa tatizo hilo limekuwa
kubwa kutokana na wazazi wengi kushindwa kutoa ushirikiano kwa serikali
za vijijini wakati wanapotakiwa kutoa taarifa kuelezea kwa nini watoto
wao wameacha masomo. “Binti anabainika kuwa ameacha shule tena ni
mjamzito, lakini ukimuuliza anasema nilikutana na kijana mmoja kwenye
gulio akanipa mimba.
Ukweli ni kwamba wazazi wanashirikiana na mwanafunzi kuficha
taarifa,” alisema Ngonyani na kuongeza kuwa: “Kama ungetupa taarifa
mapema tungekuandalia orodha ya wanafunzi waliopata mimba.”
Ngonyani alibainisha kuwa kutokana na vitendo vya
wazazi kutotaka kusema ukweli, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Henry
Clemence aliwaonya wazazi ambao watoto wao wamekatiza masomo bila sababu
za msingi kuwa wataanza kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Tatizo ni kubwa sana kiasi kwamba kuna wakati
Mkuu wa Wilaya alitaka wazazi waanze kuchukuliwa hatua za kisheria,”
alisema Ngonyani.
Hata hivyo, Diwani wa kata ya Mkamba, Hassan Dunda
alisema kuna wazazi ambao walifikishwa katika mabaraza ya kata baada ya
watoto wao kupata ujauzito na kuolewa, lakini kesi hizo zinachukua muda
mrefu kutolewa uamuzi kitu kinacholalamikiwa na wananchi.
“Kwa kawaida mzazi ndiye anayetakiwa kumshtaki mtu
aliyempa mimba binti yake, lakini huku wazazi ‘wanamalizana’ na
mhusika. Hata hivyo wale waliofikishwa kwenye mabaraza ya kata kesi zao
zinachukua muda mrefu mno,” alisema Dunda.
Akizungumzia namna tatizo la wanafunzi kupata
ujauzito lilivyo kubwa, Dunda alisema kuwa binti wa mdogo wake aliyekuwa
anasoma Shule ya Sekondari Kizomla aliacha masomo baada ya kupata
ujauzito na kwamba bado yupo nyumbani anasubiri kujifungua.
Wazazi na wanafunzi wanasemaje?
Mkazi mmoja wa Kijiji cha Mkamba Tungi, Salama
Saidi, ambaye binti yake alipata ujauzito na kujifungua wiki kabla ya
kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012, alisema tatizo la mimba ni
kubwa kiasi kwamba jamii inayomzunguka haishangai.
“Hapa hakuna mtu anayeshangaa mwanafunzi kupata
ujauzito, ila wapo wachache ambao wanajua namna nilivyomsomesha binti
yangu kwa shida, hao ndio wanaonionea huruma,” alisema Salma.
Aliongeza: “Namshukuru Mungu mjukuu wangu na mwanangu wanaendelea vizuri.”
Mwanafunzi Omari Mohamed aliyekuwa kidato kimoja
na binti ya Salma (jina tunalihifadhi) alisema wanafunzi walipata shida
kusoma na mwanafunzi mjamzito.
“Tulimshangaa baadaye tukamzoea kwa kuwa kila mtu
alikuwa anajua kuwa yeye ni mjamzito, lakini aliendelea kuja darasa hadi
alipojifunga siku chache kabla ya kufanya mtihani,” alisema Mohamed.
Taarifa zilizopatikana katika kijiji cha Kimanjichana zimebaini
kuwa wazazi huwatoza vijana wanaooa wanafunzi kati ya shilingi laki moja
na tatu.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Shule ya
Sekondari Kizomla ndiyo iliyoathirika zaidi na tatizo la watoto kuacha
masomo kwani tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009 imekwisha wasajili
wanafunzi 254 kati ya hao wanafunzi 127 wameacha masomo kutokana na
sababu mbalimbali.
Kati ya wanafunzi 100 walioingia darasa la kwanza
mwaka 2009 waliomaliza kidato cha nne ni 72. Mwaka 2010 walisajiliwa
wanafunzi 77 ambao hivi sasa wamebaki 33, huku kidato cha pili walioanza
35 wamebaki 20 tu.
No comments:
Post a Comment