Saturday, March 16, 2013

ODINGA KUTUA MAHAKAMANI LEO.

Muungano wa CORD unaoongozwa na Raila Odinga umesema kuwa leo utawasilisha malalamiko yake katika Mahakama ya Juu kupinga ushindi wa Uhuru Kenyatta aliyetangazwa mshindi katika uchaguzi wa machi 4.
Mwanasheria wa Cord,  James Orengo alisema  kwamba  Muungano huo umepokea sehemu kubwa ya nyaraka na maelezo uliyohitaji kutoka  Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Alisema nyaraka hizo ndizo ambazo zinawawezesha kuwasilisha malalamiko  ya kupinga kuchaguliwa kwa Uhuru Kenyatta kuwa Rais.
Alisema miongoni mwa yaliyokabidhiwa CORD ni karatasi zilizotumiwa kuhesabu kura, Fomu 34, 35 na 36 na pia sajili ya wapigakura.
Jaji Isaac Lenaola anayesikiliza kesi hiyo aliagiza wahusika warudi Jumatatu kuthibitisha ikiwa wote wametii matakwa na kwa maagizo zaidi. CORD ilikuwa imeshtaki IEBC na Safaricom lakini Safaricom ikaondolewa baada ya kuitikia matakwa yote ya muungano huo.
Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa na Eliud Owallo ambaye ni mkuu wa kampeni wa muungano huo.
Hivyo Rais Mteule Uhuru Kenyatta hataweza kuapishwa hadi Mahakama Kuu isikilize na kuamua kesi zote zinazopinga kuchaguliwa kwake.
Kamati inayoshughulikia kuapishwa kwa Rais mteule imeweka mpangilio kabambe wa sherehe hiyo, ikitilia maanani aina tofauti za uamuzi utakaotolewa na mahakama katika kesi ambayo muungano wa Cord uliwasilisha  katika Mahakama ya Juu.
Kamati hiyo, inayosimamiwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Kimemia imeweka mpangilio wa kuapishwa kwa Rais kwa kuzingatia uamuzi wa kesi hiyo.
Kimemia alisema mpangilio huo mpya utatolewa na unahakikisha hakuna pengo litakalotokea katika ubadilishanaji wa mamlaka.
Kamati hiyo imeweka Aprili 16 kuwa tarehe ya kuapishwa kwa Rais mteule, endapo kesi ya Cord itatupiliwa mbali na Mahakama ya Juu.

No comments:

Zilizosomwa zaidi