Wednesday, October 10, 2012

ARVs bandia zang'oa wakuu MSD

SERIKALI imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Joseph Mgaya kutokana na kubainika kuwepo kwa usambazaji wa dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV’s).

Mbali na mkurugenzi huyo,  pia imemsimamisha Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora, Daud Maselo na Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora wa Dawa, Sadick Materu.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni wiki kadhaa  tangu iliporipotiwa taarifa za kuwepo kwa dawa bandia za kupunguza makali ya ugonjwa wa Ukimwi katika mikoa mbalimbali nchini.

Dawa hizo bandia zilibainika mwanzoni mwa Septemba mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime baada ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kufanya ukaguzi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema dawa hiyo yenye jina la biashara TT-VR 30 toleo namba OC.01.85, imegundulika kuwa ni bandia baada ya kuifanyia uchunguzi wa kimaabara.

Alisema baada ya kubaini tatizo hilo walifanya ukaguzi kati ya Agosti 6 hadi 31 mwaka huu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara na mikoa mingine nchini.Waziri Mwinyi alisema baada ya kufanya uchunguzi, walibaini nyaraka zinaonyesha kuwa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI) cha jijini Dar es Salaam kiliiuzia MSD dawa hiyo.

“Wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi kwa sababu wanatakiwa kufanya uchunguzi wa kile wanachokipokea…Tunachoona hapa ni kwamba uchunguzi haukufanyika sawasawa ndiyo maana tumechukua hatua za kuwasimamisha,” alisema Dk Mwinyi na kuongeza kuwa:

“Matumizi ya dawa hiyo inayotengenezwa na TPI yamesimamishwa na imeondolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya na kurudishwa MSD,” alisema.

Alisema tayari makopo 9,570 ya  dawa hiyo yamerejeshwa MSD na kwamba bado wanaendelea na utaratibu wa kuyakusanya makopo mengine 2,600.

No comments:

Zilizosomwa zaidi