Friday, April 17, 2015

AJARI ZA BARABARANI NCHINI, SIYO UCHAWI NI UTOVU WA NIDHAMU

“Binti mdogo, amekaa chini akilia kwa uchungu, huku kiganja chake cha mkono kimekatika na hakionekani kilipo, damu inachuruzika kwa wingi, nyama zimening’inia, hana msaada, jirani yake analia kwa uchungu, huku amejiinamia” ni taswira unayoipata baada ya kuona picha inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya ajali iliyotokea huko Nzega. Lakini siku chache kabla, ndugu zetu wameteketea kwa moto na kubaki majivu baada ya magari yao kugongana na kuwaka moto. Na zaidi ya yote ni ile ajali ya kontena kuangukia basi na kuua abiria zaidi ya hamsini . Inauma! Inahuzunisha, lakini inatia hasira sana kwa sababu ajali nyingi zinatokea kwa sababu ya utovu wa nidhamu na uzembe wa kiwango cha juu!

Napenda niongee kwa msisitizo, ajali za barabarani zinazoendelea nchini Tanzania siyo kafara kama wengi wetu tunavyofikiria, bali ni matokeo ya utovu wa nidhamu ya kupuuzia misingi ya maadili kazini. Na ikumbukwe miaka mingi iliyopita, Hans Kung, mwanatheolojia wa Kijerumani aliwahi kusema, hakuna maisha pasipo maadili mema, “there is no world survival without ethics’. Ni kitu kidogo lakini madhara yake yanakuwa makubwa sana pale tunapokipuuzia. Matokeo yake, ndugu zetu wanaangamia kila kukicha, wengine wanabaki na vilema vya kudumu.
Ni utovu wa nidhamu madereva kuendesha gari kinyume na sheria za barabarani. Madereva mnafahamu kabisa barabara zetu zinakiwango cha chini kabisa, kila hatua kadhaa kunakona, na baada ya kona kunalori limesinzia hapo kwa ukosefu wa mafuta au vipuli vibovu, lakini bado mnataka kuovertake bila kuwa na uhakika na yaliyo mbele. Haiwezekani, jaribuni kufuata yale mnayofundishwa, harakaharaka haina Baraka.
Madereva mnajua kabisa viongozi dhalimu wameua usafiri wa reli ili malori yao yasafirishe mizigo ambayo ingesafirishwa kwa treni lakini bado mnaendesha kwa mwendo kasi kama vile mnahatimiliki na safari. Matokeo tumekuwa na malori mengi kila hatua kumi za barabara yakiendeshwa na madereva waliochanganyikiwa kwa mishahara finyu inayoambatana na uchovu wa kulala barabarani mwaka mzima. Lori linatoka Dar es Salaam kwenda Songea linatumia mwezi mzima. Yaani kondakta analitengeneza njia nzima mpaka inafika hatua anafanana na oili chafu. Kutumia lori bovu ni utovu wa nidhamu.
Madereva mnajua kabisa vipuli vingi vya magari vinavyoingia nchini ni feki, unakifunga kwenye gari ndani ya muda mfupi kimekwisha lakini bado mnaendesha kwa mwendo kasi wa ajabu sana. Kupuuzia hayo ni utovu wa nidhamu na kwa hali hii mtaendelea kutuua. Lakini na nyie wafanya biashara kwa nini mlete vifaa feki nchini? Mnaona raha kupata faida kubwa kwa kuuza mali feki siyo? Hivyo ni kinyume cha maadili ya Kitanzania na mwisho wa siku mtatuua sana.
Kwenu viongozi mliopewa dhamana ya kusimamia barabara zetu kumbukeni ni utovu wa nidhamu kuruhusu barabara kujengwa kwa kiwango cha chini. Barabara ya lami inakuwa na mashimo mpaka barabara ya vumbi haioni ndani? Basi la Majinja lilipata ajali eneo la Changarawe Mafinga mkoani Iringa baada ya lori lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mbeya kuangukia basi huku kontena likiwakandamiza makumi ya abiria na wengi wao kufariki dunia hapo hapo kwa sababu tu lilikuwa linajaribu kukwepa shimo kubwa kati kati ya barabara. Huu ni utovu wa nidhamu ya kutokagua barabara na wakati wananchi tunalipa kodi kila siku. Ifikie hatua ajali inapotokea wahusika wote wafungwe maisha.
Wamiliki wa magari ya abiria nanyi mnakesi ya kujibu. Kuwasisitiza madereva wenu kuendesha magari kwa mwendo wa kasi bila kuwajali ni utovu wa nidhamu. Haiwezekani dereva yuko barabarani kila siku iendayo kwa Mungu. Je dereva huyu anapumzika saa ngapi? Anasinzia saa ngapi? Basi linatoka Mwanza saa 12 asubuhi na kuingia Dar es Salaam saa nne usiku na siku inayofuata linarudi Mwanza na dereva yuleyule, je kapumzika kweli huyu? Hiki ni kinyume cha haki na binadamu. Roho za abiria siku zote zinawekwa rehani kwa madereva waliojaa usingizi kwa kiwango cha kutoweza kuona mbele kuna nini. Wewe unadhani magari kugongana uso kwa uso chanzo ni nini kama siyo kuendesha wakati wamesinzia? Naona kama ingewezekana na nahisi inawezekana kwa mmiliki/kampuni ambayo gari lake litasabisha ajali ifungiwe hata kama ni miaka miwili au zaidi kwani hii itasaidia kuwafanya waajiri kuwajali madereva wao kama binadamu.



Lakini hata nyie mafundi mnaopewa dhamana ya kukagua magari ni utovu wa nidhamu kufanya kazi zenu kizembe. Muda mfupi wa gari kuanza safari na kuchomoka tairi ni ishara ya kwamba hamjafanya matengenezo vizuri. Kibaya zaidi mafundi muache tabia ya wizi na udokozi wa vifaa vya magari. Muwe waaminifu. Nasema hivi kwa sababu nimeshuhudia mara kadhaa. Unamuachia gari fundi atengeneze lakini gari linakuwa bovu zaidi ya ulivyoliacha. Wengi unapowapa pesa ya kubadilisha spea vilivyochoka, wao wanaacha vilevile vibovu. Au gari lako linaweza kugeuka kuwa spea za magari ya wengine. Hii nimeshuhudia siku moja pale Mwanza. Nimepeleka gari gereji ili wabadilishe kifaa fulani. Alichokifanya fundi, alichomoa kifaa kizima kutoka kwenye gari la mteja mwenzangu na kukipachika kwangu na kunidai hela, na kile cha kwangu kibovu akakipachika kwenye gari la mwenzangu. Nilichokifanya pesa sikumpa na sikuondoka pale mpaka mteja mwenzangu mwenye gari lililochomolewa kifaa aliporudi nakumpa mkanda wote. Palichimbika mwanangu.
Madereva kugomea kwenda shule ni utovu wa nidhamu. Wahenga waliposema elimu haina mwisho hawakuwa wapumbavu. Mambo yanabadilika kila siku. Sasa unakuta dereva kajifunza kuendesha gari miaka kumi iliyopita akidhani magari ni yaleyale. Akiambiwa kwenda shule, anatishia kugoma na jamii nzima inamuunga mkono. Yaani kuunga mkono upumbavu ni wendawazimu wa hali ya juu na madhara yake nikuendelea kutuua. Ni kwa kusoma tu ndiyo kutawapa umahiri wa kazi yao na hivyo kupunguza kiwango cha tatizo la ajali za barabarani zinazotokea takribani kila siku hapa nchini.
Askari wa usalama barabarani kuwahurumia madereva wanaovunja sheria ni utovu wa nidhamu pia. Lakini ni utovu wa nidhamu uliopitiliza nyote kulundikana sehemu moja. Sambaeni barabara zote na kuweni wakali sana kama trafiki wa Iringa. Hawa trafiki wa Iringa ni gumzo kwa madereva wote, hawana mchezo hata kidogo. Karibu kila trafiki anatochi inayorekodi mwendo kasi na ukikiuka tu unapigwa faini hapohapo.
Na mwisho kabisa ni utovu wa nidhamu kwa abiria kukaa kimya na kumlinda dereva anaye endesha gari kama kichaa. Haisaidii kukaa kimya. Abiria ndiyo wanaojua ni aina gani ya dereva waliyenaye na mazingira ya kutoa taarifa kwa dereva anayeendesha kama kichaa kuchukuliwa hatua kali yameboreshwa. Ndugu zangu abiria, safarini siyo sehemu ya kubebana, kama dereva anakwenda mwendo wa hovyohovyo, mlipue tu.
Kumbe sisi ndiyo wachawi wa ajali za barabarani, hivyo naamini kwa kufanya haya ajali za barabarani zitabaki kuwa historia.

No comments:

Zilizosomwa zaidi