Monday, November 10, 2014

WANAFUNZI 47 WAUAWA NCHINI NIGERIA

Kumetokea shambulizi katika shule moja ya upili wakati wanafunzi wakiwa wamekusanyika shuleni humo mjini Potiskum Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.
Duru zinasema kuwa wanafunzi 47 wameuawa katika shambulizi hilo linalosemeklana kufanywa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga ambaye alikuwa amevalia sare za shule.
Shambulizi lilitokea wakati wanafunzi wakiwa wamekusanyika wakati wa asubuhi. Mji wa Potiskum ambapo shule hiyo ipo, umekuwa kitovu cha mashambulizi ambayo yamekuwa yakifanywa na Boko Haram.
Shule hiyo ni ya mafunzo ya sayansi. Mwalimu mmoja alinukuliwa akisema kuwa alisikia mlio mkubwa wa kutisha wakati bomu hilo lilipolipuka.
Kundi la wapiganaji wa kiisilamu Boko Haram huenda ndilo limefanya shambulizi hilo, ila taarifa bado hazijathibitisha hilo.
Kadhalika kundi hilo limekuwa likishambulia shule katika harakati zake za miaka 5 likitaka kuunda dola ya kiisilamu huku likipinga elimu ya kimagharibi.
Wiki jana shambulizi la kujitoa mhanga lilifanyika mjini humo na kuwaua watu 15 wakati wa maandamano ya kidini.

No comments:

Zilizosomwa zaidi