Tuesday, August 5, 2014

MJUMBE UKAWA AINGIA BUNGENI

  
Wakati wajumbe wa Bunge la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakiendelea na msimamo wa kususia vikao vinavyotarajiwa kuanza leo mjini Dodoma, mmoja wa wajumbe wake jana aliripoti bungeni na kujiandikisha.
Mjumbe huyo, Clara Mwatuka ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), alionekana katika Viwanja vya Bunge saa 6:30 mchana akiwa ameongozana na wabunge kadhaa wa CCM wakiwamo Livingstone Lusinde (Mtera) na Jerome Bwanausi (Lulindi).
CUF ni moja ya vyama vinavyounda Ukawa, pamoja na Chadema na NCCR Mageuzi na tayari viongozi wakuu wa vyama hivyo, Profesa Ibrahim Lipumba, Freeman Mbowe na James Mbatia wametangaza kwamba wajumbe wote wanaotokana na umoja wao hawatashiriki vikao vya Bunge hilo.
Mwatuka baada ya kujaza fomu maalumu za kujiandikisha, alielekea lango la Magharibi na kuingia kwenye gari la Bwanausi.
Awali, alipoulizwa kwenye Viwanja vya Bunge kuhusu kuwapo kwake Dodoma, alikataa kuzungumza lakini alikiri kujiandikisha bungeni.
Baadaye alipoulizwa imekuwaje akajiandikisha ilhali uongozi wa chama chake umesema hawatashiriki, Mwatuka alijibu: “Kwa hapo ni mapema sana kuzungumzia suala hilo, nitazungumza kesho (leo) kule bungeni ukinitafuta.”
Hata hivyo, baada ya dakika kama 30 kupita, Mwatuka alimpigia simu mwandishi na kumwambia: “Sasa kuhusu mimi kuja Dodoma, ni kweli kwamba niko hapa maana nasomesha na nilipofika nimeamua kwenda pale bungeni kuripoti.”
Aliogeza: “Ila mimi pamoja na kujiandikisha, sitashiriki vikao vya Bunge mpaka hapo tutakapokuwa tumepewa mwongozo, maana tuliambiwa kwamba majadiliano yanaendelea kwa hiyo tukiruhusiwa nitakwenda, vinginevyo sitashiriki kabisa, ndiyo hivyo.”
Bwanausi kwa upande wake alisema alimpa lifti Mwatuka kutoka Dar es Salaam baada ya mbunge huyo wa CUF kuomba msaada wa usafiri kwenda Dodoma.
“Ni jambo la kawaida, tulionana Dar es Salaam na akaniuliza iwapo ninakwenda Dodoma na mimi kweli nafasi ilikuwapo kwenye gari, kwa hiyo tumekuja naye hadi hapa, sasa zaidi ya hapo mimi sifahamu,” alisema.
Wajumbe kutoka Zanzibar na wale wa kundi la 201 ndiyo waliokuwa wengi katika usajili wa jana na wajumbe ambao wanatokana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa kutoka Tanzania Bara wakionekana wachache.
Milango yote ya kuingia katika eneo la Bunge ilikuwa imefungwa na kuacha lango moja tu la Magharibi, hali iliyosababisha baadhi ya wajumbe kuhangaika hadi pale walipopata msaada wa polisi waliokuwa wakilinda.
Mkutano wa Bunge Maalumu ambao unafanyika kwa mara ya pili, unatarajia kuchukua miezi miwili ambayo wajumbe wake wanapaswa kuitumia kukamilisha kazi ya kupitia sura 15 za Rasimu ya Katiba zilizosalia na kupiga kura kuamua kuhusu sura mbili zinazohusu Muungano.
Katika mkutano uliomalizika Aprili mwaka huu, wabunge walikuwa wametumia zaidi ya siku 70 na walifanikiwa kupitia sura ya kwanza na sita ambazo hata hivyo, hazikupigiwa kura.
Hadi jana jioni Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta alikuwa akiongoza kikao cha Kamati ya Uongozi, lakini hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu ratiba wala ajenda za mkutano unaotarajiwa kuanza leo.
Chanzo: Mwanzanchi

No comments:

Zilizosomwa zaidi