Kocha wa
Taifa Stars, Mart Nooij amesema moja ya sababu za kikosi chake kupoteza
mechi dhidi ya Msumbiji (Mambas) ni wachezaji wake kucheza kwa wasiwasi
katika kipindi cha kwanza.
Taifa
Stars iliruhusu bao la kwanza sekunde chache kabla ya kumalizika kipindi
cha kwanza katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano ya
Afrika kutafuta tiketi ya kucheza hatua ya makundi iliyochezwa leo
(Agosti 3 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto hapa Maputo.
Bao hilo
katika mechi hiyo iliyomalizika kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao
2-1, hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-3 lilifungwa kwa kichwa na
mshambuliaji Josemar Machaisse.
Nooij
alisema wasiwasi katika kipindi cha kwanza ndio ulioipa Msumbiji fursa
ya kutawala mechi hiyo katika kipindi hicho na kukimalizia ikiwa mbele
kwa bao hilo la mshambuliaji huyo wa klabu ya Bravos de Maquis ya
Angola.
Alisema
timu yake ilitulia kipindi cha pili baada ya kumuingiza Amri Kiemba
badala ya Khamis Mcha. Pia alilalamikia bao ambalo Taifa Stars ilifunga
dakika ya 16 kupitia kwa John Bocco lakini likakataliwa na mwamuzi
Dennis Bate kutoka Uganda.
Aliongeza
kuwa mchezaji Elias Pelembe aliyeifungia Msumbiji bao la pili dakika ya
83 kwa mpira wa adhabu nje ya eneo la hatari ndiye aliyemaliza mchezo
huo. Pia ni mchezaji huyo aliyebadili matokeo ya mchezo wa kwanza jijini
Dar es Salaam ambapo Msumbiji ilisawazisha dakika tatu kabla ya filimbi
ya mwisho.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, na ambayo ilicheza
vizuri kipindi cha pili ilipata bao lake dakika ya 78 na Mbwana Samata
kwa shuti la pembeni akiwa nje ya eneo la hatari na kumshinda kipa
Ricardo Campos.
Matokeo
hayo yameipeleka Msumbiji katika kundi C lenye timu za Cape Verde, Niger
na Zambia. Mechi za hatua ya makundi kutafuta tiketi ya kucheza fainali
za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco zitaanza kuchezwa
mwezi ujao.
Katika
mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita
timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2. Timu itakayosonga mbele itaingia
kwenye kundi lenye timu za Cape Verde, Niger na Zambia.
Taifa Stars inarejea Dar es Salaam leo (Agosti 4 mwaka huu) saa 8 mchana kwa ndege ya Air Tanzania.
Kikosi cha
Stars kilipangwa hivi; Deogratias Munishi, Said Moradi, Shomari
Kapombe, Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Erasto Nyoni, Mwinyi Kazimoto,
Mcha Khamis/Amri Kiemba, John Bocco/Simon Msuva, Mbwana Samata na Thomas
Ulimwengu/Mrisho Ngasa.
No comments:
Post a Comment