Thursday, June 26, 2014

MUTHARIKA AWAFUTA KAZI WAKUU WA JESHI NCHINI MALAWI

Rais wa Malawi awafuta kazi wakuu wa jeshi Rais mpya wa Malawi Peter Mutharika amewafuta kazi wakuu wa jeshi bila hata kutaja sababu yoyote. Taarifa kutoka Ofisi ya Rais imesema kamanda mkuu wa jeshi Jenerali Henry Odillo na naibu wake Meja Jenerali John Msonthi wameondolewa katika nafasi zao.
Odillo na Msonthi ambao wote pia waliwahi kuwa wanadiplomasia, wanahusishwa na mgogoro wa kikatiba ulioibuka Aprili 2012 baada ya kifo cha ghafla cha Rais Bingu wa Mutharika. Wakati Bingu alipoaga dunia ilitazamiwa kaka yake, Peter, ambaye wakati huo alikuwa waziri wa mambo ya nje, angechukua kiti cha urais badala ya Joyce Banda ambaye kikatiba alitakiwa achukue nafasi hiyo lakini alikuwa amejiondoa kwenye chama tawala. Katika harakati hizo Joyce Banda alikutana na Odillo ambaye alimpa ulinzi kamili na kutangaza kuunga mkono urais wake. Kufuatia uungaji mkono wa jeshi, Banda alitawala hadi Mei mwaka huu wakati uchaguzi wa rais ulipofanyika na Peter Mutharika kuibuka mshindi licha ya kuwepo madai ya wizi wa kura.
Jeshi la Malawi pia limehusishwa na kashfa ya ufisadi ambayo imepewa jina la 'Cashgate' ambapo mamilioni ya dola ya fedha za umma yalipotea mwaka jana.
Chanzo:Swahili Radio Tehran

No comments:

Zilizosomwa zaidi