Saturday, May 31, 2014

UNESCO: ASILIMIA 25% YA WALIMU WANAFUNDISHA MAMBO YASIYOWASAIDIA WANAFUNZI

Wakati Serikali ikiahidi kuboresha elimu nchini kwa kuhakikisha inaajiri walimu wa kutosha, imebainika kuwa asilimia 25 ya walimu huwafundisha wanafunzi mambo yasiyo ya msingi.
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), iliyozinduliwa Dar es Salaam hivi karibuni, imebainisha kuwa wakati wananchi wakilalamika kuwa elimu inayotolewa haimsaidii mwanafunzi kupata ajira nzuri, wanafunzi hawajifunzi mambo ya msingi yatakayowasaidia kupambana na changamoto za maisha.
Akizindua ripoti hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa ripoti hiyo imeweka wazi ukubwa wa tatizo la ufundishaji, akieleza kwamba jumla ya watoto milioni 250, duniani wanakosa mafunzo ya msingi ya kusoma, kuandika na kuhesabu, ingawa wanaingia darasani.
“Tanzania kama sehemu ya dunia, haijakwepa tatizo hilo. Baadhi ya watoto wetu wamekuwa wakimaliza shule za misingi bila ya kuwa na ujuzi huo. Hii ni hali ya kushtua, inayohitaji nguvu za pamoja za wadau wote wa elimu duniani,” alisema Kawambwa.
Alibainisha kwamba ripoti hiyo imependekeza mpango wa elimu mwaka 2015, uzingatie ubora utakaotokana na mipango sahihi inayotekelezeka akitaka tatizo la walimu lipatiwe ufumbuzi wa kudumu kwa lazima ili kuwanusuru wanafunzi.
“Kama suala la walimu halitapatiwa ufumbuzi sasa, tofauti kwenye ufundishaji itakuwepo kwa vizazi vingi huku ikitoa tafsiri mbaya dhidi ya jitihada za kuondoa umaskini duniani na kufikiwa kwa maendeleo endelevu,” alisema Dk Kawambwa.
Aliongeza kuwa kwa namna hali ilivyo sasa, Serikali inalazimika kuhakikisha inaajiri walimu wenye dhamira ya kweli ya kufundisha na kutoa elimu bora.
Ripoti ya Unesco inaeleza kuwa licha ya kuwepo kwa mafanikio ya kuridhisha katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, wananchi masikini ndiyo walioathirika zaidi na tatizo la utoaji elimu mbaya sababu ikiwa kutokuwepo kwa walimu wenye mafunzo ya kutosha.
Unesco ilisema kuwa kutokana na matatizo ya walimu, wanafunzi 130 milioni wanaosoma shule za msingi duniani, hawana uwezo wa kusoma hata sentensi moja, jambo linalowafanya washindwe kujiunga na sekondari.
“Matatizo ya elimu siyo tu yanaathiri malengo ya watoto ya baadaye, lakini pia uchumi wa Serikali hizo. Gharama ya watoto 250 milioni kutosoma elimu ya msingi ni Dola 129 bilioni za Marekani,(Sh 212.85 bilioni), ambayo ni asilimia kumi ya matumizi ya dunia katika elimu,” inasema ripoti hiyo. 
Ripoti hiyo imelinukuu shirikali lisilo la Serikali la Uwezo, linaloeleza kuwa asilimia 26 ya wanafunzi wa darasa la tatu ndiyo wanaoweza kusoma vizuri hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu takwimu hizo, Mratibu wa Uwezo-Taifa, Zaida Mgalla alisema kuwa asilimia 44 ya wanafunzi wa darasa la tatu walifaulu jaribio la hisabati la darasa la pili, huku asilimia 11 pekee wakifaulu kusoma hadithi ya Kiingereza.
Zaida alisema walimu wamekata tamaa ya kufundisha kutokana na Serikali kushindwa kuwatimizia mahitaji ya msingi, huku pia heshima yao ikishuka mbele ya jamii.
“Walimu hawaheshimiwi, wanapigwa na wanafunzi, mtoto akipigwa na mwalimu anapiga simu polisi waje kumkamata mwalimu. Kwa hiyo walimu wamewasusa wanafunzi na wazazi nao wapo bize na kazi,” alisema Zaida.
Pia alisema wanafunzi hawafundishwi mambo ya msingi kutokana na walimu kutojua kitu wanachofundisha.
Hata hivyo, Unesco imeimwagia sifa Tanzania kwa kuongeza idadi ya wanafunzi  waliomaliza shule ya msingi kati ya mwaka 2000 na 2007, lakini ikasema kuwa asilimia 27 ya wanafunzi hao hawakujifunza mambo ya msingi.
Vijana milioni 175 katika nchi zenye kipato cha chini na cha wastani ambao ni sawa na robo ya vijana duniani, hawana uwezo wa kusoma na kuandika. Katika nchi zilizopo chini ya Jangwa la Sahara, asilimia 40 hawajui kusoma wala kuandika.
“Ripoti inathibitisha kwamba lazima mtoto asome miaka minne ili aweze kujua kusoma na kuandika vizuri; kati ya wale waliosoma miaka minne au chini ya hapo, asilimia 77 hawawezi kusoma sentensi,” inasema ripoti hiyo.
Akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka 2014/2015 bungeni, Dodoma, Dk Kawambwa alisema kuwa vyuo vya Serikali na umma vimefanikisha upatikanaji wa walimu wapya 36,000 waliohitimu na kuajiriwa.
“Kati ya idadi hiyo, walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ni 2,364, ngazi ya cheti 17,928, ngazi ya stashahada 5,416 na ngazi ya shahada 12, 994.  Ofisi ya Waziri Mkuu - Tamisemi imewaajiri na kuwapanga katika halmashauri mbalimbali nchini, hivyo kuendelea kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa walimu ngazi mbalimbali,” alisema.
Waziri huyo alisema kuwa baada ya ajira ya walimu hao kufanyika, kwa sasa, taifa litabaki na upungufu wa walimu 30, 949 wa shule ya msingi na walimu 24, 596 wa sekondari katika masomo ya sayansi na hisabati.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya alisema kuwa walimu wanashindwa kuwafundisha wanafunzi mambo ya msingi kutokana na kukosa ubunifu wa kutumia mifano iliyopo kwenye jamii husika.
Pia alisema baadhi ya walimu waliingia katika taaluma hiyo baada ya kufeli katika masomo mengine, hivyo hawana uwezo mkubwa wa kuchambua mambo mapya na muhimu kwa wanafunzi hao.
Chanzo:Mwananchi

No comments: