
WIKIENDI hii zinachezwa mechi 16 za
raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Lakini macho ya Afrika
nzima yapo Dar es Salaam ambapo mabingwa watetezi wa mashindano hayo, Al
Ahly, itacheza na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa.
Afrika inafuatilia kwa karibu mechi
hiyo kutokana na kupepesuka kwa Ahly kwenye ligi yao ya ndani katika
siku za hivi karibuni huku Yanga ikionekana kupania kuangusha mbuyu
uliowashinda Waafrika wengi.
Yanga imesisitiza kwamba itapambana
kwa namna yoyote ile kuhakikisha inaidhalilisha Al Ahly jijini Dar es
Salaam na kurahisisha kazi ya mchezo ujao ambao utakuwa ugenini Cairo.
Si wachezaji tu, hata kocha Hans
Pluijm amepania kuweka historia ya aina yake akiwa na Yanga kwani ana
uzoefu mkubwa na mashindano hayo. Mechi hiyo itakayoanza saa 10:00
jioni, itashuhudia ushindani wa aina yake huku Yanga ikipania
kushambulia kwa nguvu na kubana sehemu ya kiungo na beki.
Yanga kabla ya kufika katika mchezo
huo utakaochezeshwa na mwamuzi kutoka Ethiopia, Bazezew Belete,
iliiondoa Komorozine ya Comoro kwa mabao 12-2. Yanga imekuwa ikijinoa
kwenye Uwanja wa Boko Beach Veteran ulioko Tegeta, nje kidogo ya jiji
huku ikipiga kambi kwenye hoteli ya Bahari Beach.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara
wamekuwa wakipiga tizi asubuhi na jioni huku kocha akisisitiza zaidi
umakini na kutumia nafasi pamoja na kuwajenga kisaikolojia wachezaji
wake.
Kwa mujibu wa mazoezi yake, Yanga
huenda ikaanzisha kikosi hiki; Deo Munishi 'Dida'/Juma Kaseja, Mbuyu
Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Frank
Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa, Emmanuel Okwi na
Hamis Kiiza. Katika nafasi ya kipa, Dida, ameonekana kuwa chaguo la
kocha, lakini Juma Kaseja pia ana nafasi ya kuanza.
Okwi atashuka uwanjani kuichezea Yanga
kimataifa kwa mara ya kwanza baada ya Shirikisho la Kimataifa la Soka
(Fifa) kubariki usajili wake Jangwani.
Yanga huenda ikatumia mifumo miwili ya 4-3-3 na 4-3-2-1 ambayo hutumiwa pia na Ahly ambayo huenda ikajilinda zaidi.
Pluijm aliishusha Yanga mazoezini kwenye Uwanja wa Taifa jana Ijumaa jioni na baadaye wakafanya wapinzani wao.
"Hatuwezi kuwaogopa kabisa Ahly,
nafurahi kuona kila kitu kipo sawa morali kwa wachezaji iko juu kwa
kiwango cha kutosha, tutawashangaza wote wanaotubeza wakifikiri Yanga ni
timu ndogo. Lakini tunawaheshimu Ahly kupitia rekodi yao katika
mashindano haya," alisema kocha huyo.
Wachezaji wa Yanga wameshatangaziwa
zaidi ya Sh100 milioni na matajiri wa timu hiyo wakiongozwa na
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa, Seif Ahmed 'Seif
Magari' na Makamu wake, Mussa Katabaro na Abdallah Bin Kleb, ambao
wamepania kuweka historia katika uongozi wao chini ya Yusuf Manji.
Ahly tayari imepatwa na wasiwasi kwani
juzi Alhamisi iliwatimua madereva wa magari waliyoyakodi wasishuhudie
mazoezi yao kwa hofu ya kufanyiwa mizengwe. Pia katika hoteli ya Hyat
Kempinski walipofikia, Waarabu hao wanafanya mambo kwa machale.
Yanga inatakiwa kuwa makini na
washambuliaji wa Ahly, Mohamed Nagy 'Gedo' anayevaa jezi namba 15 na
Amri Gamal wa jezi namba 17, ambao hawana masihara katika eneo la hatari
kwa umahiri wao katika umaliziaji wa pasi za mwisho, hivyo ni wazi
Cannavaro na Yondani wanatakiwa kuhakikisha wanawanyima nafasi ya
kusogea karibu na eneo la 18. Lakini pia kuhakikisha hawaruki peke yao
kutokana na shabaha ya vichwa vyao.
Ahly ni hatari kwa mashambulizi ya kutoka katikati ya uwanja, lakini pia hata mawinga wake hasa wa kulia huzalisha mabao yao.
Wakati akitua Jumatano kocha wa Ahly,
Mohamed Youssef, alisema: "Tunawaheshimu Yanga, ni moja ya timu bora
Tanzania kama ilivyo Simba. Lakini tumejiandaa vizuri kabla ya mechi
hii, tunataka kuwaondoa ili tuendelee na mashindano haya, tunataka
kupata ushindi hakuna shida katika hilo."
Minziro aonya mabeki
Kocha Msaidizi wa zamani wa Yanga
ambaye sasa anainoa JKT Ruvu, Fred Minziro, ameonya kuwa mabeki
wanapaswa kuacha uzembe na kufanya kazi ya ziada.
Minziro aliyekuwa akiifundisha Yanga
kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, alisema: "Yanga wana
washambuliaji wakali, tatizo lipo kwa mabeki ambao mara nyingi huwa
wanaigharimu timu kwa makosa ya kizembe.
"Kama watatumika akina Cannavaro,
Kevin Yondani, Mbuyu (Twite) na Oscar (Joshua) basi wapangiwe majukumu
maalumu wasiingiliane. Beki ya Yanga inahitaji kuwa na mawasiliano
mazuri na kipa, wasimpoteze kipa na kumfanya abebeshwe lawama."
Kibadeni atoa ufundi
Kocha mkongwe wa Ashanti United,
Abdallah Kibadeni, amemwambia Mholanzi, Hans Pluijm na wachezaji wake
kuwa kama wanataka kusonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika basi
wasiruhusu bao nyumbani.
"Ninawashauri Yanga kushambulia goli
la wapinzani wao dakika zote 90 na siyo kulinda goli lao, kikubwa
wanachotakiwa ni kujiamini na kutoihofia Al Ahly. Kweli wapinzani wao ni
timu bora, lakini ninaamini Yanga nao wapo vizuri wana washambuliaji
wenye uwezo mkubwa," alisema Kibadeni.
Logarusic aipa mbinu
Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic,
amewataka Watanzania wote wakiwamo wa timu yake, kuishangilia Yanga
dhidi ya Al Ahly bila kujali itikadi zao za kisoka, lakini akaipa onyo
klabu hiyo ya Jangwani kwamba isiidharau mechi hiyo.
"Yanga ina nafasi kubwa ya kushinda
kwani imetoka kupata matokeo mazuri katika ligi yetu, timu za Kiarabu
sasa zinaweza kuwa sawa na za Afrika Mashariki kwani uwekezaji wa soka
umekua mkubwa kama Afrika Kaskazini na Magharibi," alisema.
"Yanga wacheze kwa kujiamini na
kutodharau hata nafasi moja wanayopata, ni vyema wakashinda kama bao 1-0
au 2-0, wasiruhusu bao kwani faida ya bao la ugenini kwa Ahly inaweza
kuwaweka mahali pabaya, wawachunge mawinga wa jamaa, maana ni hatari na
wanajua wanachofanya."
Chanzo:Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment