Wednesday, March 5, 2014

AJINYONGA BAADA YA KUTUHUMIWA KUIBA SH,150,000


Watu watatu wafariki dunia katika matukio tofautitofauti mkoani Iringa likiwemo la Perizi Matiku (28) kujinyonga baada ya kutuhumiwa kuiba fedha kiasi cha shilingi 150,000/=.

Akizungumza na mtandao huu wa www.matukiodaima.com ofisini kwake leo Kamanda wa polisi mkoani Iringa Ramadhani Mungi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea mnamo tarehe 2 machi majira ya saa 9 kamili mchana katika kijiji cha Ikungwe, tarafa ya Kiponzero wilaya ya Iringa Vijijini.

Kamanda alisema marehemu alijinyonga kwa kutumia kamba iliyokuwa kwenye nguo huku chanzo kikiwa ni baada ya marehemu kutuhumiwa kuiba kiasi cha fedha za Juma Kapona.

Tukio lingine mtu mmoja aliyefahamika kwa jina Benard Muyemba (24) dereva wa IT amefariki dunia baada ya kuligonga gari kubwa aina ya scania.

Kamanda alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea mnamo tarehe 2 machi katika barabara kuu ya Iringa- Njombe na  kusema marehemu alikuwa akiendesha gari aina ya Mistubishi Canter yenye namba za usajili It.4113 ambapo alimgonga kwa nyuma gari aina ya Scania yenye namba za usajili T.944 AWB na tela lenye namba za usajili T.664 BSJ iliyokuwa ikiendeshwa na Shabani Omary (28) ambapo gari hilo kubwa lilikuwa limeegeshwa barabarani kwa sababu lilikuwa limeharibika.

Aidha Kamanda alisema mtu mmoja jina Mwajuma Kimota (60) alifariki dunia akiwa hospitali ya Mafinga anaendelea na matibabu baada ya kugongwa na pikipiki.

Kamanda alisema tukio hilo lilitokea mnamo tarehe 1 machi majira ya saa 2 kamili usiku katika kijiji cha Makongo, tarafa ya Ifwagi wilaya ya Mufindi hata hivyo dereva na namba za usajili za pikipiki hiyo hazikutambuliwa ambapo dereva alikimbia mara baada ya ajali kutokea.

Mbali na matukio hayo ya vifo Kamanda Mungi alisema JESHI la polisi linamshikilia Riziki Mgatabanhu (19) mfanyabiashara wa Ipogoro kwa kosa la kukutwa na bhangi kete 38 akiwa amezihifadhi kwenye mfuko wa rambo.
Kamanda alisema tukio hilo lilitokea mnamo tarehe 2 machi majira ya saa 3:45 wakati askari polisi wakiwa doria na kusema mtuhumiwa ni muuzaji wa biashara hiyo.

No comments:

Zilizosomwa zaidi