![]()  | 
| Inspekta Jenerali, Ernest Mangu | 
Mkuu Mpya wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu 
ameanza kazi kwa kutangaza mabadiliko ya mfumo wa jeshi hilo huku 
akiunda vitengo vipya kwa lengo kuongeza ufanisi katika kukabiliana na 
uhalifu.
Katika mabadiliko hayo, IGP Mangu amesema polisi 
wameanzisha kamisheni mpya tano ambazo ni Intelijensia, Utawala, Fedha 
na Ugavi, Upelelezi, Uchunguzi wa Kisayansi wa Kesi za Jinai na Polisi 
Jamii.
Mfumo huo mpya wa polisi ndiyo uliowezesha kuundwa
 kwa nafasi mpya ya Naibu IGP, ambayo mteule wake wa kwanza ni 
Abdulrahman Kaniki ambaye kabla ya hapo alikuwa Kamishna wa Uchunguzi wa
 Sayansi wa Makosa ya Jinai. Nafasi hiyo sasa inakaimiwa na watu 
waliokuwa chini yake.
Viongozi wengine katika safu hiyo ni Mkurugenzi wa
 Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Issaya Mngulu, Kamishna wa Operesheni 
na Mafunzo, Paul Chagonja, Kamishna wa Fedha na Ugavi, Clodwig Mtweve, 
Kamishna wa Utawala, Thobiasi Andengenye na Kamishna wa Polisi Jamii, 
Mussa Ali Mussa. Naibu Kamishna wa Polisi, Diwani Athuman yeye anakaimu 
nafasi ya Kamisheni ya Intelijensia.
Mabadiliko hayo yamekuja wakati Tanzania 
ikikabiliwa na matukio ya uhalifu ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi wa 
kiupelelezi, yakiwamo utekaji na utesaji wa watu, ulipuaji mabomu, watu 
kumwagiwa tindikali, wizi kwa njia ya mitandao na mapigano kati ya 
wakulima na wafugaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mangu 
alisema amechukua hatua hiyo kutokana na changamoto ya kukabiliana na 
aina mpya ya uhalifu ambao umekuwa ukijitokeza katika siku za karibuni.
Alifafanua kuwa zamani kazi za Fedha na Ugavi zilikuwa zikifanywa na kitengo cha Utawala na Utumishi.
Mangu alieleza pia kuwa Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi ni kitengo kipya katika jeshi hilo.
Alisema mabadiliko hayo yamelenga kuliwezesha jeshi hilo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi katika mazingira ya sasa.
“Jeshi limepanuliwa kidogo ili kukabiliana na 
changamoto zilizopo na uteuzi huu ambao pia umefanya kuwapo kwa Naibu 
IGP kwa mara ya kwanza una maana ya kuongeza ufanisi,” alisema Mangu, 
akirejea hatua ya Rais Jakaya Kikwete kumteua Abdulrahman Kaniki 
kushikilia nafasi hiyo mpya.
Alieleza kuwa wamepewa dhamana ya kuliongoza jeshi
 hilo kutoka kwa mtangulizi wao, IGP Said Mwema huku kiwango cha uhalifu
 kikiwa cha wastani na kuahidi kuupunguza maradufu.
Alisema wamepokea jeshi hilo tofauti na Mwema, ambaye alipopewa wadhifa huo 2006 kulikuwa na kiwango kikubwa cha uhalifu nchini.
“Tutajitahidi kubuni mbinu mpya za kukabiliana na uhalifu 
kulingana na mazingira kwani uhalifu kila mwaka unabadilika,” aliongeza 
Mangu.
Kuchelewesha upelelezi 
Mangu alikiri kuwapo kwa tatizo la kuchelewa kwa 
upelelezi wa kesi zinazohusu uhalifu, ila alijitetea ni kutokana na 
kujitokeza kwa uhalifu wa aina mpya.
“Tunalazimika kujipanga upya kukabili vitendo vya 
uhalifu, pia katika masuala ya upelelezi,” alisema na kuongeza kuwa 
mkakati wao kwa sasa ni kuandaa vijana kwa ajili hiyo kulingana na 
upatikanaji wa fedha kutoka serikalini.
“Tunatoa mafunzo kwa vijana jinsi ya kukabiliana na uhalifu mpya kama ule wizi kwa kutumia mtandao,” alisisitiza Mangu.
Pia alizungumzia mapigano baina ya wafugaji na 
wakulima, ambayo yametapakaa sehemu mbalimbali nchini kama Ifakara, 
Kilombero na Kiteto.
Polisi na maadili 
Mangu alibainisha kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa askari ambao watakiuka sheria na kanuni za jeshi hilo.
Alisema atajitahidi na timu yake kuhakikisha hatua
 zinazofaa zinachukuliwa kwa askari watakaokiuka misingi ya kazi zao na 
jeshi hilo litaendelea kuwaandaa askari wake kulingana na wakati uliopo.
Pia alizungumzia suala la polisi kutumia nguvu 
katika kukabiliana na uhalifu na kusema kwamba matumizi ya nguvu itakuwa
 ni hatua ya mwisho na kwamba itafanyika pale tu watu watakapokaidi amri
 halali.
“Matumizi ya nguvu ni hatua ya mwisho kwa Jeshi la
 Polisi hivyo naomba ushirikiano kutoka kwa wananchi na ninawaomba watii
 sheria bila shuruti,” alisema na kuongeza kuwa yule ambaye anadhani 
hakutendewa haki kuna njia za kufuata.
Alisema kama sheria ikifuatwa siyo jambo rahisi 
kwa polisi kutumia nguvu, hivyo kuwataka wananchi kuendelea kutii sheria
 bila shuruti.
Chanzo: Mwananchi

No comments:
Post a Comment