RAIS Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
amesema tatizo la rushwa ndani ya chama hicho lisipodhibitiwa
litakiondoa chama hicho madarakani.
Amesema chama hicho kikishinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na
tatizo la rushwa likaendelea, litakifanya chama hicho kutoshinda tena
katika uchaguzi wa mwaka 2020.
“Tukiendelea hivyo, tukishinda uchaguzi ujao wa mwaka 2015 ni bahati,
lakini tukifanikiwa kupenya uchaguzi wa mwaka 2020 hatutoki,” alisema.
Alisema hayo juzi mjini hapa wakati akifunga mafunzo maalumu ya
watendaji wa wilaya na mikoa wa CCM na kumpa rungu Makamu Mwenyekiti wa
CCM Bara, Phillip Mangula kuwashughulikia viongozi wala rushwa ndani ya
chama hicho.
“Tusipoangalia hili la rushwa tutaiondoa madarakani CCM na mambo yote
mazuri tuliyofanya hayataonekana, hapo lazima wananchi watawauliza je,
ugonjwa huu mmeshindwa kuachana nao, basi tumeamua kuwapumzisha,”
alisema.
Mwenyekiti wa chama hicho kilicho madarakani tangu Tanzania ipate
uhuru, alisema rushwa itaizika CCM kwani hiyo ni hila ambayo itakifanya
chama hicho kishindwe kuongoza kwa muda mrefu.
“Acheni kuvutavuta, mtu anarushiwa Sh 200,000 ya air time (muda wa
maongezi wa simu ya mkononi) hiyo ni nini acheni hicho kitu,” alisema na
kuongeza kuwa tatizo la rushwa limewachosha wananchi na kutishia chama
kuendelea kuongoza.
Alisema wanaotoa fedha ndio wanapokewa kwa shangwe na viongozi hao
ndio wamekuwa wakiwatafutia watu ushindi, kitu ambacho wananchi
wamekichoka na kuwa na chuki na chama hicho.
“Nakupa Mangula (Phillip) rungu la kuhangaika nao,” alisema Rais Kiwete huku akishangiliwa na wajumbe hao wa mkutano.
Alisema dawa ya viongozi kama hao ni kuachana nao kwani kuna makada
wengi ambao hawana makandokando lakini wale wenye maradhi hayo chama
hakiwezi kuendelea nao.
“Njaa taabu sana, ukiendekeza sana njaa ndiyo inakuwa hivyo, utu
unakutoka, tusifanye hivyo chuki ya watu kwa rushwa ni kubwa, kiongozi
kuwa wakala wa kusambaza fedha ni aibu kama unatosha utapita tu,”
alisema.
Alisema mafunzo hayo yatasaidia kuweka sawa ng’we ya pili ya awamu ya
nne ya serikali ya CCM na kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya ushindi
ni hakika katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2014 na uchaguzi mkuu wa
mwaka 2015.
Alisema lengo kuu la CCM kama ilivyo kwa vyama vingine vya siasa ni
kushika dola na CCM ipo kwa ajili ya kutawala lakini mtu akitoka kwenye
lengo hilo akatafute shughuli nyingine ya kufanya sio hiyo kwani dhumuni
kuu ni kushika dola.
Alisema pamoja na majukumu mengine ni lazima kuhakikisha wagombea wa
CCM wanashinda na kuendelea kukamata dola na kama viongozi na watendaji
wakuu ni kutambua na kuhakikisha chama kinakuwa na nguvu ya kutosha ili
kufikia kwenye lengo kuu.
Aliyataja mambo matatu ambayo yakifanyika, CCM itakuwa na nguvu.
Mambo hayo ni kuimarisha chama, tabia na mwenendo mzuri wa viongozi na
wanachama na utendaji mzuri wa viongozi wa CCM.
Alisema wakifanya hayo chama kitakuwa na nguvu na kila mgombea
watakayemweka atasubiri kuapishwa kwani kutakuwa hakuna wa kumpinga na
hilo litawezekana iwapo chama kitakuwa na uhai kuanzia ngazi ya Kata,
Wilaya Mkoa hadi taifa.
Pia aliwataka kutunza wanachama waliopo ambao wataendelea kukaribisha
wenzao ili chama kiwe na nguvu kwani wingi wa wanachama ni mtaji wa
kutafuta ushindi.
“Ukiwa na wanachama milioni sita waaminifu hii itafanya mgombea wako
kuwa na kura milioni sita za kuanzia, kazi yenu ni kuhakikisha
tunashinda kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura,” alisema.
Aliwataka kuweka mikakati ya kutembelea wanachama katika maeneo yao
ya uongozi ili watu wajue wenyewe wapo na kama viongozi wakiogopa
kukutana na wanachama, chama hakitashinda.
“Badilikeni kama matawi yako huyajui mnataka uongozi tu na ingekuwa
mnaitwa kwa usaili siku hiyo ingekuwa ni aibu maana mnaongoza watu
msiowajua,” alisema.
Alisema vyama vya upinzani vimekuwa vikifanya kazi hiyo kwani hata
wakiomba barua kwa makamanda wa polisi ya orodha ya barua ya vyama vya
siasa vilivyoomba kufanya mikutano, CCM haimo.
Alisema wapinzani wanazunguka ndiyo maana hata bendera ziko nyingi na
wamekuwa wakizungumza na watu na wamekuwa wanafanya kazi ya kutembea
ambayo CCM hawaifanyi.
“Mnasubiri wakati wa kampeni wakati watu wakiwa wamejazwa maneno
mengi hata muda wa kujitetea unakuwa hakuna na matokeo yake chama
kinashindwa kwenye uchaguzi,” alisema.
Pia alishutumu baadhi ya viongozi kutumia vibaya rasilimali za chama,
ikiwemo kuuza viwanja na hata kupangisha kwa mikataba yenye utata.
Akitoa mfano alisema kuna mtu kapangishwa jengo la CCM kwa miaka 264
kitu ambacho ni aibu kubwa. Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana alisema jumla ya mada 19 zilitolewa katika maeneo yote muhimu
ndani ya chama na nje ya chama.
Alisema mafunzo hayo yalihusu maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za
mitaa mwaka 2014 na mwakani yatafanyika mafunzo kama hayo kwa ajili ya
uchaguzi mkuu wa 2015.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa( NEC), Itikadi na Uenezi, Nape
Nnauye alisema mafunzo hayo maalumu yalihusisha wilaya 161 za Tanzania
bara na Zanzibar ambapo wajumbe 426 walihudhuria kati ya wajumbe 443
waliotarajiwa ikiwa ni sawa na asilimia 96.2.
Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment