Wednesday, October 30, 2013

BUNGE LAHOFIA UGAIDI, LAFUNGA VIFAA VYA KISASA

Matukio ya kigaidi yanayotokea maeneo mbalimbali duniani likiwamo lile la hivi karibuni lililotokea katika maduka ya biashara ya Westgate nchini Kenya yamelitisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuamua kufunga vifaa vingi vya ulinzi.

Majengo mbalimbali ya Bunge hivi sasa yamefungwa vifaa hivyo, hali iliyosababisha usumbufu kwa baadhi ya wabunge, wafanyakazi, waandishi wa habari na watu waliozoea kuingia kwenye ofisi husika pasipo ukaguzi unaofanyika sasa.

Awali vifaa vingi vya ukaguzi vilikuwa vimefungwa kwenye mageti ya kuingilia na katika baadhi ya milango ya ukumbi wa Bunge.

Marekebisho hayo pia yanakwenda sambamba na utoaji wa vitambulisho vya kufungulia milango, ambavyo vinagawiwa kwa watu wanaofanya shughuli katika majengo hayo, huku  wageni wanaotembelea maeneo hayo watapaswa kuongozwa na maofisa wenye vitambulisho hivyo ili waingie wanakotaka kwenda.

Tanzania Daima Jumatano lilishuhudia marekebisho makubwa kwenye ofisi mbalimbali za Bunge, ambazo zimewekewa milango ya kufunguka yenyewe kila mtu anapoikaribia, kuwekwa mazulia mapya, meza na viti vipya.

Tanzania Daima Jumatano liliwasiliana na Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Itifaki, Jossey Mwakasyuka, kujua sababu za marekebisho hayo makubwa, ambapo alisema matukio ya kigaidi yamelifanya Bunge lichukue tahadhari.

Mwakasyuka alisema usalama kwenye maeneo ya Bunge ni jambo linalopaswa kupewa umuhimu wa kipekee, kwa kuwa Tanzania ni sehemu ya dunia inayoandamwa na matukio ya kigaidi.

“Hapa bungeni ni eneo nyeti sana, kuna maofisa wengi wa serikali, mawaziri, wabunge, waandishi wa habari na wageni mbalimbali, Waswahili husema kinga ni bora kuliko tiba, tumeanza kuchukua tahadhari dhidi ya ugaidi,” alisema.

Alisema magaidi wamekuwa wakilenga maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na Bunge ni sehemu inayokusanya watu wa aina mbalimbali wanaohitaji ulinzi mkubwa.

Alisema mashine za ukaguzi zilizofungwa hivi sasa zina uwezo wa kubaini vifaa vinavyoweza kutumika kudhuru watu au mali zilizopo kwenye eneo la Bunge au sehemu nyingine iliyolengwa.

Aliongeza kuwa Bunge limechukua hatua hiyo pia kutokana na kukua kwa teknolojia ya kisasa, ambapo kila wakati wahalifu wamekuwa wakiboresha uhalifu wao kwa kutumia teknolojia.

Mwakasyuka alisema Tanzania imeshaanza kuchukua hatua za kujihadhari, ambapo hivi sasa kwenye maduka, ofisi za umma na mikusanyiko mbalimbali kuna mashine za ukaguzi pamoja na upekuzi wa kina kulingana  na mazingira husika.

“Haya mliyoyaona hivi sasa siku zijazo yatakuwa zaidi, maana tunalenga kuzuia uhalifu ambao unashamiri kila kukicha, wahalifu hatutaki kuwapa fursa ya kupenya kwenye maeneo yetu,” alisema.

Mwezi uliopita watu wanaodaiwa kuwa ni magaidi wa kikundi cha Al- Shabaab cha nchini Somalia walivamia katika maduka ya biashara ya Westgate na kuua kwa risasi watu wasiopungua 70 na kujeruhi 200.

No comments:

Zilizosomwa zaidi