Kamati ya bunge inayohusika na ulinzi na uhusiano na
mataifa ya kigeni imependekeza kufungwa kwa kambi za wakimbizi nchini
Kenya, ikisema zinatishia usalama wa nchi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Ndungu Githinji
amesema kuwa wana habari kuwa kambi zilizoko kwenye mipaka ya Kenya
hutumika kuwapa mafunzo wapiganaji wa kiislamu.
Kenya inahifadhi wakimbizi wa kisomali zaidi ya nusu milioni katika kambi za Dadaab zilizoko kwenye mpaka na Somalia.
Mwenyekiti huyo Ndungu Githinji ameambia BBC
kuwa miaka 22 imetosha kwa usaidizi kwa wasomali hao na wanastahili sasa
kurudi nyumbani baada ya amani kurejeshwa nchini mwao.
''Hawa wakimbizi wamekaa miaka ishirini na mbili
Kenya hivyo ningependa kuiomba UN ifunge kambi hizo na iwarudishe wasomali
kwao, maana sasa nao pia wanayo serikali yao ili tuweze kukaa kwa
amani''. Amesema bwana Githinji.
Lazima usalama uimarishwe
Bwana Githinji pia ametoa wito kwa vyombo vya
usalama kuzidisha usalama na doria katika maeneo yanayotishiwa
kushambuliwa na Al shabaab.
''Tunasikia AL shabaab wanasema kwamba bado
wanataka kutupiga. Naomba kuwa zile sehemu zote walizotoshia kushambulia
zipewe ulinzi wa kutosha kwa saa ishirini na nne.''
Wanamgambo wa Alshabaa wamekuwa wakijihusisha na
waislamu katika harakati zao huku wakidai kuwa wanapigania haki ya dini
ya kiislamu nchini Somalia na hata mataifa jirani kama vile Kenya.
Pia wamekuwa wakilenga Kenya kwa mashambulio
kufuatia hatua ya Kenya kuingia nchini Somalia mwaka wa 2011 kuwaondoa
wanamgambo hao kwa madai kuwa wanatishia usalama wa nchi.
Kutokana na hilo wabunge waliozuru eneo la
shambulio kule Westgate wamefurahishwa na hatua ya waislamu nchini Kenya
kujiepusha na kundi hilo la AL-Shabaab.
Mwenyekiti Githinji asema, '' Ningependa
kupongeza viongozi wa waislamu ambao wametoa taarifa yao kuwa hawaungi
mkono mashambulio haya.''
Mwandishi wa BBC jijini Nairobi anasema kuwa
wito huu wa kufungwa kwa kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma,
zimekuwepo kwa muda. Wakenya wengi wanahisi kuwa Kuwepo kwa wakimbizi
hao kumeendelea kuiweka nchi hiyo katika hatari ya mashambulio. Lakinim
bali na hilo.
Pia baadhi wanahisi wakimbizi hao ndio wa
kulaumiwa kwa kupanda gharama ya makaazi hasa katika maeneo ya Nairobi
kama vile Eastleigh, wanakoishi kwa wingi zaidi.
No comments:
Post a Comment