Mamlaka ya Uthibiti
Usafiri wa nchi kavu na Majini SUMATRA, imewataka abiria na wananchi wote
wanaotumia vyombo vya usafiri wa majini kupitia Bandari zote za Ziwa Victoria ,
kuwa na kitambulisho kinachoonyesha taarifa zao mhimu wakati wa kukata tiketi.
Akitoa taarifa hiyo
hiyo hii leo Mkoani Mwanza, Mhandisi Japhet Loisimaye Ole ambae ni Afisa
Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Ziwa kwa niaba ya Msajili wa Meli SUMATRA, Amesema
kwamba utaratibu huu unalenga kuwa na taarifa sahihi kwa kila abiria katika
meli ama boti, sambamba na kuzuia abiria kusafiri kwa kutumia tiketi yenye jina
la mtu mwingine.
Amesema kwamba
utaratibu huo kwa kanda ya ziwa utaanza kutumika rasmi kuanzia septemba tisa
ambayo ni jumatatu ya wiki ijayo, ambapo wamiliki wa Meli ama Boti watalazimika
kujaza taarifa sahihi katika orodha ya wasafiri kwa mujibu wa vitambulisho
vyao.
Mhandisi Ole amebainisha kwamba kupitia
utaratibu huo, Maafisa wa Bandari na Mialo yote iliyoko ndani ya Ziwa Victoria
watawaruhusu abiria wenye tiketi halali na vitambulisho husika pekee kuingia
bandarini ama melini.
Ameainisha
vitambulisho vinavyoweza kuwasilishwa ni pamoja na Kitambulisho cha uraia,
Kitambulisho ukaazi,Hati ya kusafiria (Passport), Kitambulisho kupigia
kura,kitambulisho cha kazi, leseni ya udereva pamoja na barua ya utambulisho
inayotolewa na serikali za mitaa yenye picha.
Amefafanua kwamba kwa upande wa watoto wadogo
ambao wengi wao hawana vitambulisho vya aina yoyote, watatumia barua za
utambulisho zinazotolewa na serikali za mitaa, barua ambazo sharti ziwe na
picha ya mhusika.
Aidha amebainisha
kwamba agizo hilo halitawahusu abiria wanaotumia usafiri wa meli ama boti
zinazosafiri umbali usiozidi maili za majini 20 kati ya bandari moja na
nyingine sambamba na vivuko kwa maana ya Ferry.
Katika hatua nyingine
Mhandisi Ole amesema kwamba suala la kuonyesha vitambulisho halina gharama
yoyote na hivyo kuwataka kuonyesha ushirikiano wao, huku akitoa onyo la
kuwachukulia hatua kali wamiliki wa vyombo vya usafiri wa majini watakaokuwa
wanasafirisha abiria kinyemera bila kufuata utaratibu huo.
Agizo hili limekuja
ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kanuni za Kuhakiki na Kusajiri Abiria
(Mechant Shipping Counting and Regstration of Person on Board Passenger Ships)
kama zilivyoainishwa na tangazo la serikali Na: 142/2011, likiwa na lengo la
kupata idadi na taarifa kamili za abiria, taarifa ambazo husaidia katika wokozi
pindi chombo cha usafiri kinapopata dharura majini.
No comments:
Post a Comment