WANASIASA wanaotajwa kutaka kuwania urais mwaka 2015 kwa tiketi
ya CCM, Edward Lowassa na Bernard Membe, wanadaiwa kuuvuruga Umoja wa
Vijana wa CCM (UVCCM).
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa umoja huo umegawanyika
katika makundi mawili, ambapo moja linamuunga mkono Lowassa na jingine
Membe.
Inadaiwa uteuzi wa Katibu Mkuu mpya wa UVCCM, Sixtus Mapunda,
uliofanyika wiki iliyopita umelenga kupunguza nguvu ya Lowassa kwenye
umoja huo.
Sixtus aliteuliwa na Halmashauri Kuu (NEC) akirithi mikoba ya Martine Shigela, anayedaiwa kuwa upande wa Lowassa.
Wakati Mapunda akitarajiwa kuidhinishwa na Baraza la Umoja linalofanya
kikao chake leo visiwani Zanzibar, tayari kumekuwa na minong’ono kuwa
wadhifa huo amepewa ili kudhibiti kasi ya Lowassa ndani ya UVCCM.
Mapunda inadaiwa yupo katika kundi linalomuunga mkono Membe ndiyo
maana baadhi ya vijana wanapinga uteuzi wake kwa madai utazidisha
mpasuko ndani ya UVCCM.
Inadaiwa kuwa wakuu wa wilaya, Eribariki Kingu, Mrisho Gambo na
Anthony Mtaka, mmoja wao alitarajiwa kumrithi Shigela aliyedumu kwenye
nafasi hiyo kwa miaka mitano.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa kigogo mmoja ndani ya CCM
tayari alishampigia simu mmoja wa wakuu hao wa wilaya akimtaarifu jina
lake ndilo litakalopitishwa na NEC.
Inadaiwa jina hilo halikuweza kupenya katika vikao vya NEC kwa
sababu kigogo mwingine alifanikiwa kuwashawishi wajumbe wampitishe
Mapunda kwa madai hana makundi kama wakuu wa wilaya hao waliokuwa
wakipigiwa chapuo.
Tanzania Daima Jumapili liliwasiliana na Mapunda, kuhusu uteuzi wake
ambapo alisema ameteuliwa kuongeza umoja, mshikamano na ushirikiano.
Alibainisha kuwa wanaomhusisha na makundi wanafanya hivyo kwa lengo la
kumpaka matope ili asitekeleze malengo ya kuuimarisha na kuuendeleza
umoja huo.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukilumbana wenyewe kwa wenyewe, mimi nataka
hali hii imalizike, nataka kuwaunganisha vijana, sitakubali tuvurugane,”
alisema.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa baadhi ya wajumbe wa Baraza
la UVCCM leo wamejipanga kumng’oa Sadifa kwa madai kuwa ameboronga
katika wadhifa wake huo.
Sadifa alirithi kiti hicho kutoka kwa Hamad Masauni Yussuf,
aliyelazimika kujiuzulu mwaka 2010, baada ya kukumbwa na kashfa ya
kughushi cheti cha kuzaliwa kwa lengo la kudanganya umri.
Mmoja wa wajumbe wa Baraza la UVCCM (jina kapuni) alisema walitarajia
Sadifa angeung’arisha umoja huo lakini amezalisha mizozo inayoizorotesha
Jumuiya hiyo.
“Huyu ndugu yetu kaboronga sana, tunataka ang’oke ili tumtafute mtu
mwingine, si kweli kuwa tunatumika na kundi la watu wanaotaka urais bali
tunataka tusafishe UVCCM,” alisema.
Chanzo kimoja kutoka CCM kimelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa
Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, alikwenda visiwani Zanzibar
kutuliza upepo wa kumng’oa Sadifa.
Nchimbi ambaye alishawahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM inaaminika ndiye
kinara wa kutuliza mambo yanapochafuka ndani ya umoja huo.
Jitihada za Tanzania Daima Jumapili kuzungumza na Nchimbi, hazikuweza
kuzaa matunda kwa kuwa muda mrefu simu yake ilikuwa ikiiita bila majibu.
Tanzania Daima Jumapili pia lilishindwa kuwasiliana na Sadifa kutokana
na muda mrefu simu yake kuonesha ikiongea, hata alipotumiwa ujumbe
mfupi wa maneno (sms) hakujibu.
No comments:
Post a Comment