Monday, September 23, 2013

OPERESHENI YA KUWAKOMBOA MATEKA WANAOSHIKILIWA NA AL-SHABAAB HUKO NAIROBI KUKAMILIKA MUDA MCHACHE KUANZIA SASA



 Jeshi la Kenya limefanikiwa kudhibiti sehemu kubwa ya jengo la kibiashara Westgate na wanaendelea vema na operesheni ya kuhakikisha wanawakomboa mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo wa kundi la Alshabab ambao walivamia na kuteka eneo hilo jumamosi mchana.

Msemaji wa jeshi la kenya kanali Cyrus Oguna amethibitisha operesheni ya kuwakomboa mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Alshabab imefikia hatua ya mwisho na inaweza kutamatika muda wowote.

Idadi ya watu waliopoteza maisha imeongezeka na kufikia 69 wakati majeruhi wakifikia 175 kwa mujibu wa serikali nchini Kenya.Misaada ya aina mbalimbali imeendelea kutolewa ikiwemo zoezi la uchangiaji damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya majeruhi ambao wengine wamefanyiwa upasuaji.

Tukio la mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wa Al-Shabab kwenye maduka ya westgate nchini kenya limezusha hofu miongoni mwa mataifa ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi za Maziwa makuu.

Serikali za Tanzania, Rwanda, Uganda na Burundi zimelaani shambulio hili na kutoa pole kwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta pamoja na wananchi wa taifa hilo ambao wamepoteza ndugu zao.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa kenya kwasasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya kiusalama hali ambayo ni lazima nchi jirani ziimarishe usalama kwenye mipaka yao.

No comments: