KWA mara ya kwanza tangu lilipoibuka
sakata la watu maarufu kujihusisha ama na utumiaji au usafirishaji wa
dawa za kulevya, jina la mwanamuziki anayeaminika kuwa na ukwasi mkubwa
kwa sasa hapa nchini, Nasseeb Abdulmaliki, maarufu zaidi kwa jina la
Diamond, limeanza kutajwa kuwa ni miongoni mwa vigogo wa ‘unga.’
Tayari mjadala mkubwa wa chini chini
umeibuka kwa watu mbalimbali wakiwemo mashabiki wake, na taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zimedai kuwa,
mwenendo wa maisha ya Diamond sasa unachunguzwa na baadhi ya maofisa wa
vyombo vya dola vya ulinzi na usalama.
Kutajwa kwa jina la Diamond katika
sakata hili, kunatiwa nguvu zaidi na mwenendo binafsi wa maisha wa
msanii huyo maarufu wa muziki wa kizazi kipya, unaokwenda sambamba na
ukwasi mkubwa alioupata katika kipindi kifupi.
Kama hiyo haitoshi, safari za nje ya
nchi za mwanamuziki huyo unaohusisha ziara zake nchini Afrika Kusini na
Uingereza, pia ni mambo ambayo yamechochea wingu la mashaka lililofikia
hatua ya jina lake kuingizwa katika mtandao huo ambao katika siku za
karibuni, umewagusa pia baadhi ya watu wenye majina makubwa katika
jamii.
Kuhusu ziara hizo, kilicholeta
mshtuko na dukuduku dhidi yake ni kuwapo kwa taarifa kwamba, katika moja
ya ziara hizo za nje ya nchi, Diamond alifikia hatua ya kusafiri
akitumia chumba kinachotumiwa na wageni mashuhuri (VIP), badala ya njia
ya wasafiri wa kawaida.
Mbali na hilo, taarifa nyingine
zinaeleza kwamba, mizigo ya msanii huyo ambaye mara kadhaa amekuwa
akisafiri na kundi la wacheza shoo wake, imekuwa ikipita pasipo
kupitishwa katika hatua za ukaguzi kwa namna ile ile ilivyokuwa kwa
mabinti wawili wa Kitanzania walionaswa nchini Afrika Kusini baada ya
kuruka mfumo wa ukaguzi wa Julius Nyerere International Airport(JNIA).
Aidha, ukaribu wa kimahusiano kati ya
Diamond na baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini Afrika Kusini na ambao
majina yao pia yameanza kuhusishwa na biashara hiyo ya mihadarati, ni
jambo jingine ambalo limechochea harakati za kufuatiliwa kwa karibu kwa
nyendo za Diamond.
Taarifa zaidi kutoka JNIA zinaeleza
kwamba, miongoni mwa watu wanaoweza wakawa wamemponza Diamond ni wale
ambao walionekana kuwa karibu na Agness Gerald ‘Masogange’ (25) na
Melisa Edward (24), siku walipokuwa wakisafiri kwenda Afrika Kusini
kabla hawajanaswa katika uwanja wa Ndege wa Oliver Thambo jijini
Johannesburg nchini Afrika Kusini, wakiwa na shehena ya dawa za kulevya.
Mwenendo wa watu hao unatiliwa shaka
kuwa huenda ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya
wenye maskani yao nchini Afrika Kusini, kwa sababu mbali na ukaribu na
wasichana hao, pia walihusika kwa karibu kuusafirisha mwili wa
mwanamuziki Albert Mangwair, aliyefia huko huko Afrika Kusini ambaye
taarifa za kufa kwake ziligumbikwa na matumizi ya dawa za kulevya.
Alipoulizwa jana na gazeti moja kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu taarifa hizo na iwapo
amekwishahojiwa na vyombo vya dola baada ya jina lake kuanza kutajwa
kuwa miongoni mwa orodha ya wasanii wa muziki wanaosafirisha dawa za
kulevya, Diamond alikiri kuwa na pesa za kutosha kuishi maisha
anayoyataka, lakini akakana kujihusisha na biashara hiyo.
Akifafanua tuhuma moja baada ya
nyingine kwa mpangilio aliokuwa akiulizwa na gazeti hilo, Diamond
alisema katika maisha yake, hajawahi kujihusisha na utumiaji au
usafirishaji dawa za kulevya, lakini madai hayo yamekuwa yakitolewa
dhidi yake na watu ambao hawajui siri ya mafanikio yake.
“Kazi ngumu siku zote inalipa, sasa
napata matunda ambayo yanatokana na kile nilichokifanya, iweje watu
wanitilie mashaka, Watanzania ni mashahidi wangu wananiona navyochumia
juani, nitaendelea kulia kivulini tu kwani nakula kwa jasho langu.
“Siyo kweli kwamba mizigo yangu
haikukaguliwa na kama haikukaguliwa na ingekuwa na kasoro, basi
Uingereza wangenitia hatiani, nilipita na nilikaguliwa.” Alisema
Diamond.
Alipoulizwa kuhusu taarifa za kuwa
mwanamtandao wa kundi la Masogange, pia alikanusha kwa kueleza kuwa hata
siku aliyosafiri kwenda Afrika Kusini alikwenda peke yake uwanja wa
ndege na kuongeza kuwa alikwenda huko kwa shughuli za kimuziki, ambapo
safari nzima iligharimu zaidi ya Dola 30,000 za Kimarekani.
“Afrika Kusini nimekwenda kufanya
kazi zangu na safari hiyo imenigharimu zaidi ya Dola 30,000, nilikwenda
kurekodi nyimbo yangu mpya inayoitwa namba moja ambayo itaanza kusikika
hivi karibuni.
“Unajua Watanzania sasa hivi wanajua
mtu hawezi kufanikiwa au kupata maendeleo bila kuuza ‘unga’, hili si
sawa juhudi za mtu ndizo zinamfikisha alipo, na mimi juhudi zangu ndio
zinanifikisha hapa, watu waache kunijadili vibaya.” Alisema Diamond.
Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja
ikiwa ni takribani miezi miwili sasa tangu Watanzania wawili, Agness
Gerald ‘Masogange’ (25) na Melisa Edward (24), waliokuwa na uhusiano wa
karibu na baadhi ya wanamuziki maarufu hapa nchini, kukamatwa nchini
Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine
zenye thamani ya Sh bilioni 6.8.
Mbali na kuwa na uhusiano wa karibu
na wanamuziki, Edward anadaiwa kuwa alikuwa mfanyakazi katika mgahawa
mmoja maarufu jijini Dar es Salaam, unaomilikiwa na mmoja wa vijana
matajiri hapa nchini ambaye hata hivyo gazeti hili halijafanikiwa
kumpata ili kufanya naye mahojiano.
Wakati huo huo, tayari hatua za
kinidhamu zimekwishaanza kuchukuliwa dhidi ya wafanyakazi wa JNIA
waliohusika kupitisha kilo 150 za dawa za kulevya, ambao Waziri wa
Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ametaja majina yao hivi karibuni na
kuonyesha kwa waandishi wa habari ushahidi wa kuhusika kwao.
No comments:
Post a Comment