Mganga wa kienyeji mkazi wa Kijiji
cha Nyansincha, wilayani Tarime mkoani Mara, Mwita Nyamankore, anasakwa na Polisi
kwa madai ya kumpa dawa ya kienyeji mgonjwa wake na kumsababishia kuharisha na
kutapika hadi kufa.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime-Rorya, Justus Kamugisha, jana alimtaja mgonjwa huyo kuwa ni Mtongori Momayi (25), mkazi wa kijiji cha Gibaso, ambaye alifariki dunia Jumanne baada ya kunywa dawa hiyo.
Kamanda Kamugisha alisema Nyamankore alifika nyumbani kwa mgonjwa huyo kumtibu maradhi yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu, ambayo hata hivyo hayakufahamika.
Kwa mujibu wa Kamanda, baada ya kupewa dawa, mgonjwa alitapika na kuharisha mfululizo na kuzidiwa nguvu, hali iliyosababisha kifo chake kabla hajafikishwa katika Hospitali ya Wilaya kupewa msaada.
"Tunamsaka Nyamankore ambaye baada ya tukio alitoroka na huenda amekimbilia nchi jirani ya Kenya, tunaomba wananchi watoe msaada kwa kutoa taarifa, ili akamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
"Tunaasa wananchi kupewa matibabu hospitalini ambako watachukuliwa vipimo vya ugonjwa na kupata tiba sahihi, kuliko kwenda kwa waganga wa kienyeji ambao hawana vipimo vya dawa wanazotoa," alisema Kamanda Kamugisha.
No comments:
Post a Comment