SERIKALI imesema haitavumilia kwa namna yeyote ile vurugu za
kidini, kikanda na ukabila ambazo baadhi yake zilitaka kulitia doa taifa
mwaka jana.
Pia imesisitiza kwamba haitawavumilia wanasiasa wanaotumia rasilimali za taifa kujitafutia umaarufu kwa gharama za kuligawa taifa.
Pia imesisitiza kwamba haitawavumilia wanasiasa wanaotumia rasilimali za taifa kujitafutia umaarufu kwa gharama za kuligawa taifa.
Akizungumza na mabalozi kwa nyakati tofauti Ikulu, Dar es Salaam; kwanza katika sherehe ya kuukaribisha Mwaka Mpya iliyofanyika juzi na alipokuwa akiagana na Balozi wa Uingereza nchini, Dianne Corner jana, Rais Jakaya Kikwete alisema vurugu zilizotaka kujitokeza mwaka jana zinatosha.
“Serikali haitavumilia vurugu wala ukabila kwa namna yoyote ile…. Mwaka 2012 vurugu zenye sura ya kidini zilianza kujitokeza ila sasa nasema kwamba hatutazivumilia kwa namna yeyote ile, inatosha,” alisema Rais Kikwete.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kiongozi wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Juma Mpango alisema jumuiya ya mabalozi imefurahishwa na namna ambavyo Serikali imekuwa ikishughulikia vurugu za kidini ambazo zilitaka kujitokeza bila kusababisha madhara kwa wananchi.
“Tumeridhishwa na namna ambavyo Serikali imekuwa inashughulikia mambo yake vizuri. Tunaomba mwendelee kushughulikia amani ya nchi hii maana ndiyo mhimili wa nchi za Maziwa Makuu,” alisema Balozi Mpango.
Kuhusu gesi
Rais Kikwete alizungumzia suala la rasilimali za taifa na kusisitiza kuwa pia hatavumilia kuona wanasiasa wakitumia suala la gesi kujitafutia umaarufu.
Wakati Rais Kikwete akitoa kauli hiyo jana, habari kutoka Mtwara zilidai kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene amewekewa magogo barabarani kumzuia asiende kwenye kijiji kinachozalisha gesi hiyo, huku Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Regina Chonjo akizomewa.
Hata hivyo, polisi walikiri wananchi kuweka magogo barabarani kwa lengo la kumzuia waziri huyo, lakini ikaeleza kuwa gari lililozuiwa siyo la Simbachawene.
Akizungumza na Balozi Corner, Rais Kikwete alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kutumia suala la rasilimali za taifa, ikiwamo gesi asilia kujitafutia umaarufu wa kisiasa na kuwapotosha wananchi.
“Ni jambo la hatari na lisilo na tija kwa wanasiasa kujaribu kuigawa nchi vipandevipande kwa sababu ya kujitafutia umaarufu kwa kutumia rasilimali za taifa,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Unawezaje kuwa na nchi moja na taifa moja wakati kila mmoja anadai rasilimali kutoka kwenye eneo moja ibakie na kunufaisha watu wa eneo hilo tu. Huwezi kuwa na nchi moja na yenye umoja wakati kuna nchi ya gesi asilia kule Mtwara, kuna nchi ya kahawa kule Kilimanjaro, kuna nchi ya chai na ndizi kule Bukoba,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kwa sababu kama gesi asilia inatakiwa kubakia na kunufaisha watu wa Mtwara tu, basi wenye haki zaidi ya kudai jambo hili siyo watu wa Mtwara, bali ni watu wa Msimbati ambako ndiko ilipogunduliwa gesi ambako ni maili 60 kutoka Mtwara, kilomita 200 kutoka Newala.”
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment