Amiri
Jeshi mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,Dk. Jakaya Mrisho
Kikwete akiwasili katika Uwanja wa Uhuru akiwa kwenye gari maalumu la
Kijeshi sambamba na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,Jenerali Davis
Mwamunyange walipokuwa wakitoa salamu kwa wananchi na wageni mbalimbali
waliofika uwanjani kwa ajili ya sherehe za maadhimisho ya Miaka 51 ya
Uhuru wa Tanzania Bara (Tanganyika).
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete
leo ameongoza Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania
Bara (Tanganyika) yaliyofanyika kwenye Uwanja vya Uhuru jijini Dar es
Salaam na kuhudhuriwa na viongozi na wageni mbalimbali kutoka nje na
ndani ya nchi.
Rais Kikwete aliwasili katika uwanja huo majira ya saa nne kamili na
kuwasalimu Watanzania na viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe hizo
kabla ya kupigiwa mizinga 21 ikiwa ni heshima kama Amiri Jeshi Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa nchi.
Baadaye Rais Kikwete alikagua gwaride rasmi la maadhimisho hayo kisha
gwaride hilo lililoundwa na askari anuai kutoka majeshi ya ulinzi na
usalama wa nchi. Gwaride pia lilipita mbele ya rais kutoa heshima kwa
mwendo wa pole na haraka ambapo lilikuwa ni kivutio kingine kwa wageni
waalikwa waliofika katika sherehe hizo.
Katika maadhimisho ya mwaka huu Rais Kikwete alilazimika kusimama na
kuzungumza ikiwa ni tofauti na sherehe zilizopita za uhuru, ambapo
alifanya hizo ikiwa ni kutoa shukrani kwa wageni mashughuli 12 kutoka
nchi mbalimbali ambao wamehudhuria sherehe hizo.
Viongozi
mbalimbali wakiwa katika maadhimisha hayo, kutoka kulia ni Rais wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Joseph Kabila, Mama Maria Nyerere,
Rais wa Msumbiji, Armando Guebuza, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
ya Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal na Rais Mstaafu wa Awamu ya pili,
Mzee Ali Hassan Mwinyi. (Picha zote na Full Shangwe Blog)
Miongoni mwa wageni hao wamo marais watatu, yaani Rais wa Msumbiji,
Armando Guebuza, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph
Kabila, pamoja na Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba.
Wengine ni Makamu wa Rais wa Malawi, Khumbo Kachali, Makamu wa Rais
Zambia, Dk. Guy Scott, Makamu wa Rais wa Angola, Manuel Vicente, Makamu
wa Rais wa Visiwa vya Shelisheli, Waziri Mkuu wa Lesotho, Thomas
Motsoahae Thabane, Waziri Mku wa Swatzland, Waziri Mkuu wa Rwanda,
Waziri wa Mambo ya Nje ya Zimbabwe, Katibu Mkuu Mtendaji wa SADC na
viongozi wengine kutoka nje na ndani ya nchi.
Sherehe hizo za mwaka huu zilizopambwa na vikundi vya halaiki, maonesho
ya sura ya kitabu, vikundi vya ngoma na sarakasi yaliudhuriwa pia na
viongozi wa juu wa Serikali ya Tanzania Bara na Visiwani, viongozi anuai
wa vyama na Serikali pamoja na viongozi wa dini.
Katika mazungumzo yake mafupi kwa umma huo, aliwapongeza Watanzania kwa
kutimiza miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara huku wakiendelea kudumisha
amani na utulivu na mafanikio tele katika nyanja anuai. Kivutio kingine
katika maadhimisho hayo ambacho kiliwainua viongozi mbalimbali kwenye
viti ni ngoma ya kikundi cha Utandawazi kutoka Ukerewe ambayo ilichezwa
kiumahiri na mvuto na watoto wadogo wenye umri wa miaka mitatu kitendo
ambacho kiliwavutia wengi. Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Mwaka huu ni
“Uwajibikaji, Uadilifu na Uzalendo ni nguzo ya Maendeleo ya Taifa letu”.
No comments:
Post a Comment