Polisi mkoani Mwanza wamefanikiwa kuipata simu ya upepo ‘radio
call’ iliyokuwa ikitumiwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,
marehemu Liberatus Barlow ambayo ilichukuliwa baada ya kuuawa kwa kupigwa
risasi usiku wa manane eneo la Minazi Mitatu Kitangiri.
Mbali na
simu hiyo, jeshi hilo pia limefanikiwa kupata ufunguo wa gari la marehemu
Barlow ambaye aliuawa wakati akimsindikiza mwanamke mmoja aliyeitwa Doroth
Moses walipokuwa wakitoka kwenye kikao cha harusi ya ndugu yake.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lili Matola, alisema jana kwamba vitu hivyo
vilipatikana vikiwa vimefichwa katika shimo la majitaka katika nyumba moja
iliyopo maeneo ya Nyashanya.
Pia jeshi
hilo limefanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wengine wawili wanaodaiwa kuhusika
katika mauaji hayo na Kamanda Matola alisema wataunganishwa kizimbani na
wengine watano Novemba 15, mwaka huu.
Alisema
watuhumiwa hao wawili (majina tunayahifadhi kwa sasa), mmoja wao akiwa ni ndugu wa mtuhumiwa namba
moja katika mauaji hayo, ndio waliotaja sehemu vilikokuwa vimefichwa vitu hivyo
baada ya kuhojiwa.
“Baada ya
kuonyesha vilipokuwa vimefichwa, ilibidi kumtaarifu mwenye nyumba ambaye alitoa
idhini ya kubomolewa kwa shimo hilo la majitaka na mmoja wa watuhumiwa aliingia
na kutoa ‘radio call’ pamoja na funguo za gari la marehemu,” alisema Kamanda
Matola.
Alisema kuwa
baada ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa namba moja alitoa maelekezo ya wapi
pa kuficha vifaa hivyo. Kabla ya kuficha simu hiyo, waliitenganisha na betri
yake.
Kamanda
Matola alisema katika msako waliofanya nyumbani kwa watuhumiwa hao, pia
walikuta sare za moja ya kampuni ya ulinzi
pamoja na magwanda ya mgambo.
Alisema kuwa
vitu vingine vilivyokamatwa ni kofia mbili, moja ikiwa ya polisi na nyingine ya
kampuni ya ulinzi pamoja na vifaa mbalimbali vinavyotumika kwa ajili ya kufanyia
uhalifu.
Alisema
mmoja wa watuhumiwa aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela,
alichokitumikia kuanzia mwaka 2006 baada ya kukutwa na makosa ya unyang’anyi
kwa kutumia silaha. Hata hivyo, alisema aliachiwa huru mwaka 2010 baada ya
kukata rufani Mahakama Kuu na kuachiwa huru.
Alisema
katika mahojiano na polisi, mtuhumiwa huyo alisema alishawishiwa na kaka yake
kufanya kazi hiyo ya ujambazi.
Mbali na
watu hao, Matola alisema polisi pia inamshikilia mtu mmoja (jina tunalihifadhi)
mkazi wa Nyakabungo akituhumiwa kufadhili kundi hilo la majambazi.
No comments:
Post a Comment