Sunday, November 11, 2012

FFU WATUPIWA VILAGO NJE.

BAADHI ya wafungwa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wanadaiwa kutumiwa na kigogo mmoja wa Polisi kuwatoa kwa nguvu askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kwenye nyumba walizokuwa wakiishi katika Kambi Kuu ya mjini Moshi.

Tofauti na ilivyozoeleka ambapo hushuhudiwa FFU wakitumika kusambaratisha mikusanyiko ya watu wenye lengo la kuhatarisha amani, askari hao walitolewa kwa nguvu kwenye nyumba hizo na wafungwa hao ambao wanadaiwa kutoa vyombo vyao nje.
Tukio hilo lililowaacha vinywa wazi watu wengi mkoani Kilimanjaro, limewapata FFU waliokuwa wakiishi kwenye nyumba tatu zilizopo katika kambi kuu ya polisi mjini Moshi.
Taarifa zinadai FFU hao ilibainika kuwa   hawakupaswa kuishi katika nyumba hizo, badala yake polisi wa kawaida ndio waliopaswa kuishi, hivyo waliondolewa ili polisi hao waingie.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alikiri kutokea kwa tukio hilo, lakini akasema: “Hayo ni masuala ya ndani ya polisi, siyo ya kuyaandika.”
Habari zaidi zinasema kuwa tukio hilo lilitokea Alhamisi iliyopita zikieleza kuwa kigogo mmoja wa polisi ndiye aliyewatumia wafungwa hao kuvamia na kuvunja milango ya nyumba za FFU hao ili kuwaondoa kwa nguvu, akidai kuwa alitumia njia za busara kuwataka watoke lakini walionekana  kuleta kiburi na kwamba hakuona sababu ya kuwatumia polisi.

No comments:

Zilizosomwa zaidi