BAADA ya kufika kwa gesi asilia jijini Dar es Salaam ikitokea Mtwara,
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushirikiana na Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), itaingiza gesi hiyo katika mitambo
yote ya umeme nchini, hivyo kuanzia leo kutakuwa na ukosefu wa umeme
katika mikoa yote inayotumia Gridi ya Taifa.
Hatua hiyo inatokana na kuzimwa mitambo yote ya umeme katika kituo
kikubwa cha kuzalisha umeme cha Ubungo, Dar es Salaam kwa nia ya
kuingiza gesi asilia katika mitambo huo. Imeelezwa kuwa tatizo hilo la
umeme, litadumu kwa wiki nzima ambao umeme utakatika kwa saa kadhaa
usiku na mchana, lakini hali itakuwa mbaya zaidi kwa siku ya leo.
Akizungumza katika kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi One jana,
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema mitambo yote ya
umeme itazimwa ili kuingiza gesi asilia kuanza kuzalisha umeme katika
kituo hicho kikubwa.
“Wiki hii umeme utakatika sana kutokana na kuunganishwa gesi kutoka
Mtwara kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa kuanzia kesho mitambo yote
itazimwa,” alisema Mramba. Alisema kwa saa za mchana na usiku ndani ya
wiki hii itakuwa mikoa yote inayotumia Gridi ya Taifa itakosa umeme.
Alisema baada ya majaribio ya kupitisha gesi asilia kukamilika sasa
wanaingiza kwenye mitambo hiyo ili kuanza kuzalisha megawati 150 za
umeme huku mitambo ya megawati 200 iliyokuwa haifanyi kazi kutokana na
gesi kutotosha nayo itaanza kufanya kazi.
Alisema baada ya kuunganisha bomba hilo na umeme kuanza kuzalishwa
mwishoni mwa wiki Watanzania watakuwa na uhakika wa umeme pamoja na bei
ya umeme ya uhakika kwa muda mrefu.
“Kutokana na kuwa na gesi ya uhakika naamini mdhibiti ataangalia na
bei inaweza kupungua ingawa siyo kesho au mapema,” alisema bosi huyo wa
Tanesco.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Dk James Mataragio alisema kwa sasa
mitambo ya Kinyerezi imejaa gesi na wameishaingiza gesi yenye mgandamizo
wa tatu na inatakiwa kufika mgandamizo 50 hadi 51 ili kuzalisha umeme.
Alisema kwa muda wa wiki watakuwa wamefikisha mgandamizo huo kwa
kuingiza polepole baada ya kufanya majaribio na kuona kuna uwezo wa
kuingiza mgandamizo 90.
“Kuanzia kesho (leo) mpaka baada ya wiki mbili tutakuwa na uwezo wa
kuzalisha umeme kwa gesi kwa kufikia mgandamizo huo wa 50,” alisisitiza
na kuongeza kuwa uzalishaji huo, Serikali itaokoa dola bilioni moja
zilizokuwa zikitumika kwa uzalishaji umeme wa mafuta.
Mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam ulikamilika Julai mwaka huu.
Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment