Kumekuwepo na madai yanayosambazwa kupitia njia mbalimbali za upashanaji
habari kuhusu baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kuonekana mjini Dodoma au kujisajili kwa ajili ya kuhudhuria
vikao vya Bunge Maalum la Katiba vinavyoendelea mjini humo.
Chama kupitia Idara ya Habari kinatumia fursa hii kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo;
1. Uamuzi wa kuwataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na
CHADEMA kushirikiana na wenzao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA), kutoshiriki vikao vya bunge hilo ili kuepuka kunajisi mchakato
wa Katiba Mpya, ulitokana na maazimio ya kikao cha Kamati Kuu iliyoketi
Julai 18-19 na kuazimia kwamba;
§ Wajumbe wa Bunge Maalum wanaotokana na CHADEMA, kama sehemu ya UKAWA,
watarudi kwenye vikao vya Bunge Maalum endapo tu mamlaka ya Bunge hilo
yatafafanuliwa kuwa ni ya kuboresha, na sio kuibomoa au kuifuta, misingi
mikuu (basic features) ya Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya
wananchi na kuandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoteuliwa na
Rais kwa ajili hiyo;
§ Wajumbe wa Bunge Maalum wanaotokana na CHADEMA, kama sehemu ya UKAWA,
watarudi kwenye vikao vya Bunge Maalum endapo tu, na baada ya, ufafanuzi
uliotajwa katika aya ya 2 utahusisha marekebisho ya kifungu cha 25 cha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, inayohusu mamlaka ya Bunge
Maalum, pamoja na Kanuni husika za Bunge Maalum;
§ Wajumbe wote wa CHADEMA katika Bunge Maalum hawatashiriki katika kikao
chochote cha Bunge Maalum au Kamati zake hadi hapo ufafanuzi wa mamlaka
ya Bunge Maalum uliotajwa katika aya za 2 na 3 utakapofanyika kwa
mujibu wa maazimjo ya Kamati Kuu;
Hadi wakati huu, hakuna jambo hata moja kati ya hayo lililofanyika, huku
mazungumzo yaliyotarajiwa kuokoa mchakato yakiwa yamevunjika, kwa
sababu CCM na Serikali yake wameamua kudharau na kupuuza maoni ya
wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba badala yake kuweka maslahi ya
chama hicho kwenye katiba.
2. Iwapo kuna mjumbe/wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na
CHADEMA wameonekana wakijisajili kwa ajili ya kuhudhuria vikao vya Bunge
Maalum la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma au watashiriki vikao vya
bunge hilo au kamati zake, wataandikiwa barua ya kujieleza kisha chama
kitachukua hatua kwa mujibu wa taratibu zake kupitia vikao.
3. Tunapenda pia kuwakumbusha wanachama wa CHADEMA na umma mkubwa wa
Watanzania kuwa, mji wa Dodoma mbali ya kuwa Makao Makuu ya Nchi pia
inapatikana Ofisi Kuu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba ambako hakujaridhiwa na Watanzania
wengi, hakujazuia shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kufanyika ikiwemo kutoa huduma kwa watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na
wabunge. Suala hilo linakwenda sambamba na ukweli kwamba sehemu kubwa ya
watumishi wa Bunge Maalum la Katiba wanatokana na baadhi ya watumishi
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo kuonekana kwa mbunge yeyote wa CHADEMA mjini Dodoma au kwenye
viwanja au Ofisi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hakuwezi
kutafsiriwa moja kwa moja kuwa mbunge husika amehudhuria vikao vya Bunge
Maalum la Katiba, kinyume na msimamo wa UKAWA.
Imetolewa leo Alhamis Agosti 7, 2014 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari- CHADEMA
No comments:
Post a Comment