MNYIKA APENDEKEZA MGAWANYO WA MANISPAA ZA JIJI LA DAR ES SALAAM
Nimepokea mwaliko wa kikao maalumu cha kikao cha fedha na uongozi wa
tarehe 3/01/2014 kikao kufanyika tarehe 06/01/2013 saa nane mchana
kujadili mapendekezo ya kuongeza maeneo mapya ya utawala katika Mkoa wa
Dar es Salaam pamoja na ajenda zingine.
Nimeonelea tija
kuwasilisha mapendekezo yangu kwa maandishi kwa umma na baadae katika
kikao tajwa. Kwa hatua hii, ni fursa kwa kila mwananchi kutoa maoni yake
juu ya haya;
Kwa ukuaji wa kasi wa Dar es Salaam ambao ndiyo
mji mkubwa nchini Tanzania, jiji kitovu cha biashara na viwanda ambalo
kadiri ya takwimu linakadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni nne na
nusu. Jiji hili limeshika nafasi ya tatu katika miji inayokuwa kwa kasi
nchini Afrika na miongoni mwa miji kumi inayokuwa kwa kasi duniani.
Ifahamike pia, Jiji la Dar es Salaam ndilo linashikilia asilimia
themanini na tatu (83%) ya mapato ya serikali kitaifa na takribani
asilimia sabini (70%) ya kodi zote zinazokusanywa nchini Tanzania.
Yafuatano ndiyo mapendekezo yangu ya wasilisho la nyaraka ya
mapendekezo yaliyoletwa katika ofisi yangu toka Manispaa ya Kinondoni;
Mosi, Pendekezo la kutumia “Manispaa” badala ya “Wilaya”:
Kadiri ya wasilisho, imetumika pendekezo la “wilaya”. Ningeshauri na
kupendekeza kutokana na uhalisia na ukuaji wa kasi kutumika kwa
“Manispaa” badala ya wilaya.
Pili, Pendekezo bora la mgawanyo wa Manispaa:
Katika wasilisho lenye uwepo wa mapendekezo saba. Ninaungana na kuafiki
utumiaji wa pendekezo la pili lililowasilishwa la kuwa na Manispaa tano
(5) ambazo ni; i. Manispaa ya Ilala ii. Manispaa ya Temeke iii. Manispaa ya Kinondoni iv. Manispaa ya Kigamboni v. Manispaa ya Ubungo
Sababu muhimu:
1. Ukubwa kijiografia: Kwa kuongeza wilaya mbili mpya yaani Manispaa ya
Kigamboni na Manispaa ya Ubungo hii itasaidia wilaya hizi kuweza
kuhimili ukubwa wa eneo wa kijiografia ambalo kwa sasa inaelemea wilaya
hizi za sasa yaani Manispaa ya Kinondoni na Manispaa ya Temeke. 2.
Ukuaji wa kasi wa jiji: Katika ukuaji wa kasi unaoendelea jiji la Dar es
Salaam maeneo yaliyopo katika wilaya hasa ya Kinondoni na Temeke ndiyo
ambayo yanaongoza pia katika ukuaji huo wa kasi wa kimakazi na shughuli
za kiuchumi kama viwanda na uwekezaji. Hivyo kwa kuwa na Manispaa mpya
mbili(Manispaa ya Ubungo na Manispaa ya Kigamboni) zitasaidia kwa kiasi
kikubwa kuweza kusimamia vyema mipango miji, kuujenga vyema mji na
kusimamia kihuduma. 3. Uwepo wa mipango ya kuimarisha ukuaji wa jiji
kupitia miji ya pembezoni “satellite cities”: tayari serikali imeweka
dhamira ya kuimarisha ukuaji wa jiji kupitia satellite cities. Hivyo
uwepo wa wilaya mbili yaani Kigamboni (Satellite city Kigamboni) na
Ubungo (“Luguruni Satellite City” ndani ya Kata ya Kwembe na Kata ya
Kibamba) zitamudu kusimamia vyema ujenzi imara wa satellite cities na
pia kuwezesha wilaya zitakazoachwa kama wilaya ya Kinondoni kuwa na
ahueni ya kuelemewa na kazi hivyo nazo kusimamia vyema mipango ya ujenzi
wa satellite cities zilizomo ktk maeneo hayo
Tatu, Ugawaji wa kata ndani ya Manispaa mpya na kusimamia kata zilizopo:
Katika mapendekezo yaliyowasilishwa, kumekuwa na mgawanyo mpya
unaonyang’anya kata ambazo tayari zilikwisha kuwapo katika baadhi ya
maeneo mathalani ndani ya Manispaa ya Kinondoni. Mfano wa maeneo kama
Kisopwa, Mloganzila. Maeneo tajwa yamekuwa yakihamishwa toka Manispaa ya
Kinondoni na kupelekwa Mkoa wa Pwani. Hivyo kukizana hata na dhamira ya
kujaribu kuchukua baadhi ya kata na maeneo ambayo yapo katika miji
inayokaribia jiji la Dar es Salaam katika dhamira ya kupanua jiji.
Pia, kwa nyakati tofauti tumeshuhudia viongozi wa kitaifa wakitaja mara
kwa mara katika hotuba zao na matamko yako maeneo yaliyopo ndani ya
Manispaa ya Kinondoni kama eneo la Mloganzila kuyataja kuwa katika Mkoa
wa Pwani. Jambo hili si sahihi. Jambo hili limekuwa likiacha maswali
mengi kwa wananchi. Ifahamike tu, wananchi hawa wanatambulika chini ya
mifumo rasmi tuliyojiwekea inayowatambua kama wakazi wa Manispaa ya
Kinondoni.
Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha ufafanuzi
mpana unawekwa na kusimamia uwepo wa maeneo haya yaendelee kuwapo katika
wilaya za Dar es Salaam.
Sambamba, kuna hitaji la haraka na
muhimu katika mchakato huu kuhakikisha migogoro ya ardhi ndani maeneo ya
Kisopwa na Mloganzila yapatiwe ufumbuzi wa kudumu. Pia kuhakikisha
maeneo hayo yanabaki katika kata ya Kwembe kwenye Manispaa
inayopendekezwa ya Ubungo.
Nne, Kujifunza toka miji na nchi zingine:
Kuna umuhimu mkubwa wa kupanua wigo wa miji na nchi ambazo tunaweza
kuchota uzoefu katika zoezi la kugawa wilaya mpya na kupanua jiji la Dar
es Salaam. Mifano minne kadiri ya wasilisho pekee haitoshi. Napendekeza
na kushauri kuongeza miji iliyopo katika nchi ifuatayo, miji ambayo
inashabihiana na sifa za jiji la Dar es Salaam la ukuaji wa kasi, mifumo
wa kiutawala, hali za kiuchumi na kimaendeleo ; i. Lagos-Nigeria ii. Johannesburg-South Africa iii. London-Uingereza iv. New Delhi-India v. Shangai, China
Katika kusoma na kuchukua uzoefu toka katika miji iliyowasilishwa
katika pendekezo na hii mingine, tusiishie kuangalia mifumo ya ugawaji,
ukuzwaji na usimamizi bali pia twende hatua ya kuangalia muundo wa
utendaji wa miji hii ambayo yatasaidia sana katika kuboresha muundo wa
kiutendaji wa jiji la Dar es Salaam.
Tano, Mapendekezo katika Muundo wa Kiutendaji wa Jiji la Dar es Salaam:
Nakubaliana na hitaji la kuwepo kwa Jiji la Dar es Salaam kama chombo
kikuu juu ya Manispaa zote tano zinazopendekezwa zitakazokuwapo Dar es
Salaam.
Pia, nakubaliana na kuunga mkono hitaji la Meya wa
Jiji la Dar es Salaam kuchaguliwa na wananchi. Hii itatoa fursa katika
utendaji na uwajibikaji imara ambayo unaweza kupimwa na wananchi.
Hivi ndivyo majiji ambayo yamepiga kasi ya kimaendeleo kama London
(Uingereza) yanajiendesha. Pia hata majirani zetu kama Kenya; nao
wametambua mfumo huu na kuuchukua katika Katiba yao mpya.
Pendekezo muhimu; kuna haja ya Jiji la Dar es Salaam likawa juu ya
manispaa zote tano zinazopendekezwa na hivyo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa isiwe
na mamlaka na nguvu kulinganisha na Jiji la Dar es Salaam.
Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha pia Jiji la Dar es Salaam
linapatiwa mamlaka na madaraka ambayo hayaingiliwi na kuzuiwa na wilaya
nyingine zozote zilizopo chini yake.
Sita, Kuunganisha mapendekezo ya Muundo wa Mkoa wa Dar es Salaam na mchakato wa Katiba Mpya ya Tanganyika:
Kwa kutambua nchi ipo katika mchakato wa kuandika katiba mpya ya
Tanzania. Mchakato ambao utatoa fursa ya uandishi wa katiba mpya ya
Tanganyika kuna umuhimu mkubwa wa kuanza kuandaa kisheria hoja za kuwapo
ndani ya katiba ya Tanganyika zenye kusimamia Muundo wa Jiji la Dar es
Salaam. Huu ukawa ni mfumo wa mfano “modal” katika ngazi za jiji zenye
kuhitaji kuwapo katika mfumo wa kikatiba. Hii ikiwamo na suala la Meya
wa Jiji kubwa kuchaguliwa na wananchi na mengineyo muhimu.
Kuna
umuhimu pia wa kuwepo wa hoja ya kikatiba katika upanuzi na ukuaji wa
Manispaa na ngazi nyingine za miji ndani ya Katiba. Hivyo, Katiba ya
Tanganyika inahitaji kuwa nguzo muhimu.
Hitimisho: Naomba
wananchi wa Jimbo la Ubungo na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwa
ujumla kutoa maoni yenu ili hatimaye tupate mfumo bora wa kiutawala kwa
maslahi na ukuaji wa Jiji letu.
Wenu katika utumishi,
John J. Mnyika Mbunge wa Jimbo la Ubungo 06 Januari, 2013
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.