Sunday, December 29, 2013

VIBAKA WAIBA MAFUTA KWENYE MALORI

 
Vijana wakimimina mafuta kutoka kwenye tenki la mafuta katika eneo la Nakonde mpakani mwa Tanzania na Zambia ambapo magari ya kubeba mafuta yanakuwa kwenye foleni yakisubiri kuruhusiwa kuvuka mpakani na kuingia Tunduma-Tanzania.
 Kijana akiwa na spana mkononi inayotumika kufungulia vizibo katika matenki huku mwingine akiwa amebeba mfuko wa plastiki wenye mafuta akisubiri kumimina mafuta mengine.
 
Haba na haba hujaza kibaba, kijana akijaribu kumiminia mafuta kwenye mfuko wa plastiki kutoka kwenye tenki mojawapo la mafuta kisha mafuta yanayokusanywa huwekwa kwenye madumu na kuuzwa.


 
 
 
Waenda kwa miguu wakipita pembezoni mwa magari ya kubeba mafuta na kushuhudia kinachoendelea.

 Kwa kawaida madereva wa magari ya mafuta huona kila kitu kinachoendelea lakini kwa usalama wao hulazimika kubaki kimya wakati mafuta yakimiminwa kwa vile inasemekana dereva anayejaribu kushuka ili kuwazuia anaweza kuambulia kipigo kikali.
Vibaka hawa wanapomimina mafuta, hushuhudiwa na madereva wa teksi wakiwa katika makundi jambo linaloashiria kuwa uhalifu huu umezoeleka.
Ni ajabu na kweli, Vibaka hawa hawafanyi uhalifu huu jirani na eneo la uhamiaji ingawa hufanya jirani na kituo cha polisi na ofisi za halmashauri zilizo jirani na barabara katika eneo la Nakonde bila kuchukuliwa hatua zozote zile.

Vibaka hawa walishuhudiwa wakifungua vizibo kwenye kila gari la kubeba mafuta na kumiminia kwenye mifuko ya plastiki ambapo  uwingi wa mafuta yaliyopatikana ulitofautiana kutoka gari moja hadi jingine ikizingatiwa kuwa magari haya yalikuwa yanarudi Tanzania baada ya kupeleka mafuta Zambia.

Kuna wakati walionekana kumimina mafuta mengi kwenye gari moja kiasi cha kujaza mifuko miwili. Kwa hesabu ya kawaida kuanzia asubuhi hadi jioni ni wazi wanakusanya mafuta mengi zaidi.

No comments:

Zilizosomwa zaidi