Tuesday, November 19, 2013

MWAKYEMBE ATUA KUSAKA DAWA ZA KULEVYA UWANJA WA NDEGE WA KILIMANJARO (KIA)

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Waziri  wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amewaonya maofisa wa umma wanaofanya kazi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kukifanya kiwanja hicho kuwa njia ya kupitishia dawa za kulevya.
Akizungumza wakati akikagua uwanja huo jana, Waziri Dk. Mwakyembe alisema maofisa wa wanaojishughulisha na biashara hiyo haramu wakiwamo maofisa wa uhamiaji, siku zao za mwisho zinakaribia.
“Ninatambua wafanyabiashara ya dawa haramu za kulevya sasa wanatumia KIA kama njia ya kusafirishia kwenda ughaibuni. Nawataka waache, serikali itachukua hatua kali dhidi yao,” alisema.
Alisema KIA ilikuwa ikifanya vizuri katika biashara, lakini kama mwelekeo huu wa biashara ya dawa za kulevya unaweza kuachwa kuendelea hivi hivi unaweza kuharibu mafanikio yaliyokwishapatikana.
Hata hivyo, alisema taarifa mbalimbali zilizopo zinaonyesha kwamba baadhi ya Watanzania wamekamatwa ughaibuni wakiwa na hati feki za kusafiria, nyingi zikiwa zimetokea KIA.
“Kama serikali, tunafanya uchunguzi kuhusu suala hili na kama itathibitika kuwa waliokamatwa walitumia uwanja huu basi maofisa wote waliokuwa zamu wakati huo watafukuzwa kazi.
Alisema jukumu la Kampuni ya Maendeleo ya Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kadco) na wafanyakazi wake kutunza na kulinda hadhi ya uwanja huo, ambao hadi sasa umeweza kupata tunu mbili za kimataifa kwa mwaka huu.
“Pia ni jukumu lenu kuhakikisha wahalifu hawatumii uwanja huu kwa biashara haramu. Wote ambao wanaona hawawezi kufuata sheria na kanuni zinazoendesha uwanja huu wa ndege wanatakiwa kutafuta sehemu nyingine ya kufanya kazi.
“Ni aibu sana kusikia kwamba Watanzania wanakaguliwa kama mtu anayetoka gerezani kwa sababu tu wapo baadhi ya watu wanaopaka matope taswira nzuri ya viwanja vyetu vya ndege,” alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kadco, Balozi Gumbo Kibelloh, alisema vita dhidi ya dawa haramu za kulevya inaendelea na kwamba Kadco na vyombo vya usalama vimeimarisha ulinzi.
“Kuanzia Machi mwaka huu, watu watano wamekamatwa KIA kuhusiana na tuhuma za dawa za kulevya,” alisema na kuongeza kwamba Machi 2, 2013, Idd Chuma alikamatwa wakati akijaribu kusafirisha kilo sita za dawa aina ya kokaine kwa kutumia ndege ya Qatar Airways.
Alisema Mei 11, raia mmoja wa Nigeria Ike Joachim, aliyetarajia kwenda Ethiopia, alikamatwa akiwa na kete nane za dawa za kulevya uwanjani hapo.
Kwa mujibu wa Kibelloh, Juni 23, mwaka huu, Ramadhan Ramadhan alikamatwa na kilo 11 za marijuana na akijaribu kwenda Uturuki wakati Nusura Mtinge, alikamatwa na kilo 14 za bangi wakati akijaribu kwenda Uturuki kwa kutumia ndege ya nchi hiyo.
Alisema Septemba 22, mwaka huu, Farida Ismail, alikamatwa na kilo 7.7 za marijuana wakati akijaribu kwenda Uturuki.
Alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja, uwanja huo wa ndege ulikuwa ukifanya kwa kuongeza idadi ya ndege zinazotua na kuruka kutoka hapo.
Alisema idadi ya wasafiri wanaotumia uwanja huo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 25.

No comments:

Zilizosomwa zaidi