Sunday, November 24, 2013

LAPTOP IMECHANGIA KATIKA MAUAJI YA KUTISHA ILALA BUNGONI JIJINI DAR

Christina Newa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mauaji yaliyofanywa na mchumba wake Gabriel Munisi.
Yamkini wengi wanapotamka neno ‘penzi’ lenye herufi tano tu, hudhani ni dogo lisilo na uzito katika maisha ya binadamu.
Lakini kama umeshawahi kusikia kuwa mapenzi yanaua, basi uhalisia unaoonyesha  madhara, uzito na machungu ya mapenzi...ndiyo huu hapa.
Desemba mwaka jana ni wakati, Gabriel Munisi alipokutana na Christina Newa. Awali lilikuwa penzi, ambalo Christina aliamini litampa faraja, kicheko na kuyabadili maisha yake.
 Hata hivyo, ndoto yake hiyo ilibadilika muda mfupi tu wa penzi hilo baada ya mpenzi wake, Munisi, kuanza kuonyesha ukali uliopitiliza, wivu na maneno makali.
 “Gaby alikuwa anaishi kwa kasumba, hajiamini, mkorofi na aliyependa kunitishia kwa kutumia silaha mara kwa mara,” anasema Christina.
Ukali wa Munisi haukupungua licha ya Christina kujaribu kumbadili hata kumshauri aonane na daktari wa masuala ya saikolojia ambaye anaweza kumtibu.
 “Nilimwona si wa kawaida. Nilipomshauri kuhusu tiba, alikubali na akampigia simu daktari mmoja aliyekuwa hospitali ya Bugando ambaye alikubali kuwa, inawezekana Gaby ana matatizo ya kisaikolojia na wakakubaliana kuwa ataanza tiba,” anasema.
Christina baada ya kuona penzi lake na Munisi limekithiri kwa  misuguano, mifarakano na vitisho, alishauriana na familia yake, kisha wakaamua kuwa aende kusoma katika Visiwa vya Cypruss, ili kujiongezea maarifa lakini pia atakuwa mbali na Munisi ambaye alikuwa sasa anaonekana kuwa tishio. 
Munisi alionekana kuwa tishio mara baada ya kumtakia hadharani Christina kuwa endapo atamchezea ataisambaratisha familia yake akianzia na Goba, anakoishi mama yao, Ellen Eliezer, kisha Zanzibar anakoishi mdogo wake, Alpha Newa na kumalizia Ilala, inakoishi familia hiyo.
Kwa maelezo ya Christina, kosa kubwa ambalo lilionyesha kumuudhi zaidi Munisi, ni kitendo chake cha kuondoka nchini bila kumuaga. Hata hivyo Munisi hakukata tamaa bali alihakikisha anapata mawasiliano ya Christina akiwa huko visiwani Cypruss.
“Tuliwasiliana tukiwa kule na tukazungumza. Kwa sababu ilikuwa  ni kipindi cha likizo akaniambia atakuja kunipokea uwanja wa ndege. Nilidhani atakuwa amebadilika kwa kipindi hiki,” anasema.
Cha ajabu, Munisi baada ya kumpokea Christina, alimkataza kwenda nyumbani kwao na badala yake alimlazimisha waende, Mwanza, Kitangiri, anakoishi.
Chanzo:Mwananchi

No comments:

Zilizosomwa zaidi